Somo la 2
Baadhi ya wanafunzi wanakulia katika nyumba ambazo zina utajiri wa chapa na maumbo: maboksi ya bidhaa za dukani, pakiti na makopo, vitabu kwa ajili ya watoto na watu wazima, magazeti hata kompyuta/ngamizi. Wengine wana vifaa hivi kwa uchache nyumbani kwao. Changamoto yako kama mwalimu ni kulipatia darasa lako mazingira yenye utajiri wa chapa . Njia moja ya kufanya hivi ni kukusanya vifaa vyovyote popote vinapopatikana. Vifaa vya kufungashia (maboksi ya mbao, pakiti na makopo) mara nyingi vinaandikwa sana na hata wanafunzi wadogo mara nyingi hutambua maneno muhimu kwa zile bidhaa ambazo zinatumika sana nyumbani. Kwa wasomaji wazoevu, magazeti ambayo wanajumuiya wameshamaliza kuyasoma yanaweza kutumiwa kwa shughuli nyingi darasani.
Sehemu hii inatalii njia za kutumia chapa kama hizi katika kusaidia kujifunza kusoma.
Uchunguzi kifani ya 2: Kutumia orodha ya vitu vya dukani kwa shughuli za kujifunza kusoma na kuandika
Precious Muhaji hufundisha Kiingereza kwa wanafunzi 45 wa Darasa la 4 lililopo Lushoto katika Milima ya Usambara. Hawajazoea sana Kiingereza lakini wanatambua herufi na baadhi ya maneno ya Kiswahili yaliyopo kwenye vifaa vya kuhifadhia bidhaa ndogondogo za nyumbani.
Precious alimwomba jirani yake maboksi/makasha, pakiti na makopo matupu. Alivileta vitu hivi shuleni ili kuvitumia katika shughuli za kujifunza kusoma na kuandika.
Mchezo unaopendwa na wanafunzi wake ni mchezo wa ‘ugunduzi wa maneno’. Precious alilipanga darasa katika vikundi tisa vya wanafunzi watanowatano na kukipa kila kikundi boksi, pakiti au kopo lilelile. Aliwaambia wanafunzi waandike namba kuanzia 1 mpaka 5 na kisha aliuliza maswali matano (angalia Nyenzo Rejea 3: Maswali ya mfano ya kuuliza kuhusu vitu vya nyumbani ). Wanafunzi walilinganisha majibu wenyewe na waliamua kuhusu jibu la kikundi. Precious alijadili yale maswali na darasa zima. ‘Mshindi’ alikuwa ni kikundi kilichomaliza cha kwanza na kuweza kutoa majibu sahihi zaidi.
Wakati mwingine Precious alikikaribisha kila kikundi ili kiweze kuuliza swali linalohusiana na ugunduzi wa neno.
Ili kuwahamasisha wanafunzi wafikiri kwa makini, wakati mwingine aliuliza swali kuhusu mchoro wa kifaa kinachohifadhia bidhaa na ujumbe uliopo kwenye tangazo.
Precious aligundua kuwa wanafunzi wengine hawakushiriki, hivyo wakati mwingine walipocheza mchezo huu, alimwambia kila mwanafunzi aandike maneno manne kutoka kwenye kontena la kuhifadhia bidhaa za dukani kabla ya kurudi kwenye viti vyao vya kawaida. Wakiwa wamesharudi kwenye viti vyao alimwambia kila mmoja amsomee mwenzake orodha yake. Aligundua wanafunzi sita ambao walihitaji msaada zaidi na alifanya nao kazi baada ya saa za shule kwa nusu saa, kwa kutumia vitu vilevile na kuwapatia muda wa kufanya mazoezi ya kubainisha herufi na maneno.
Precious aligundua kuwa kuzoea herufi na maneno katika vifaa vya kuhifadhia bidhaa huwasaidia wanafunzi kubainisha herufi na maneno haya katika matini nyingine walizozisoma, kama vile hadithi. Kwa kunakili maneno kutoka katika vitu hivyo, wanafunzi pia hujifunza kuandika herufi na maneno kwa kujiamini zaidi na kwa usahihi zaidi.
Shughuli ya 2: Kutumia orodha ya bidhaa za dukani kwa shughuli za usomaji na uandishi
Leta makopo/mikebe, pakiti au maboksi ya kutosha darasani ili kila kikundi cha wanafunzi watanowatano au sitasita kipate kitu kimojawapo cha kukifanyia kazi au liambie darasa lako likusaidie katika ukusanyaji wa vitu hivi.
Andika maswali ubaoni kuhusu maneno na picha zinazoonekana kwenye pakiti, kopo au boksi ( angalia Nyenzo Rejea 3 ). Ama waambie wanafunzi wayasome au uwasomee.
Ama chezesha mchezo wa ugunguzi wa maneno katika vikundi (angalia Uchunguzi Kifani 2) au waambie wanafunzi waandike majibu wenyewe. Panga muda wa ziada wa mazoezi na wa kutoa msaada zaidi kwa ajili ya wanafunzi ambao hawawezi shughuli hii.
Katika somo linalofuata, waambie wanafunzi wafanye kazi katika vikundi vilevile wabuni maandishi na taarifa zinazoonekana kwa ajili ya kifaa cha kweli au picha ya bidhaa za dukani.
Kiambie kila kikundi kioneshe na kuzungumzia kuhusu ubunifu/mchoro wao kwa wanafunzi wote darasani.
Wanafunzi wamejifunza nini kwa kusoma orodha ya bidhaa za dukani na kwa kuchora na kuonesha vifaa vyao wenyewe vya kuhifadhia bidhaa hizo? Linganisha mawazo yako na mapendekezo yaliyopo katika Nyenzo Rejea 3 .
Somo la 1