Nyenzorejea ya 1: Kitu ambacho waandishi na wasomaji wafanisi wanatakiwa kukijua
Usuli/ welewa wa somo wa mwalimu
Lugha wanayotarajiwa kujifunzia usomaji na uandishi
Kama wanafunzi wanatakiwa wajifunzie kusoma na kuandika katika lugha ambayo si lugha ya nyumbani, hali hii itafanya kazi iwe ngumu zaidi. Katika hali hii, walimu wanatakiwa waanze na kazi za kuongea na uundaji wa msamiati katika lugha hii ya nyongeza, kwa kutumia vitendo na picha. Pindi tu watakapokuwa na uelewa wa baadhi ya yanayosemwa wanaweza kutarajiwa kutumia uelewa huo kwa usomaji na uandishi.
Msimbo wa maandishi
Wanafunzi wanahitaji kuelewa jinsi herufi kwenye ukurasa unavyowakilisha sauti fulani na jinsi zinavyoungana katika kuwasilisha maana kwa njia ya maneno. Hii ndiyo sababu ya umuhimu wa walimu kwa kiasi fulani kuzingatia ‘foniksi’ – herufi inayowakilisha sauti fulani – wanapowafundisha wasomaji wa kiwango cha mwanzo. Kwa kuchukua mfano toka katika lugha ya Kiswahili, kama mwalimu ungeweza kutumia picha ya mbwa pamoja na herufi tofauti za m b w a na kisha neno m b w a chini yake. Kwanza waulize wanafunzi wanaona nini katika picha (mbwa), kisha onesha kila herufi na kuitamka; kisha tamka neno zima. Baadaye pima welewa wa wanafunzi kwa kuonesha herufi ambazo hazijaunganishwa na kuwaambia waunde manenokwa kutumia kila moja ya sauti. Baadaye, waambie wakuambie maneno mengine yanayoanza na sauti m. Pia wapatie mifano yako mwenyewe.
Kanuni za uandishi
Wanafunzi wanahitaji kuelewa jinsi maneno yanavyoungana kuunda maana katika sentensi, aya, na matini ndefu (mf.kitabu kizima cha hadithi) na jinsi matini zinavyoandikwa kwa njia nyingi na kwa madhumuni mbalimbali (mf. Mapishi ni tofauti na jinsi hadithi inavyoandikwa). Katika miaka ya mwanzo, wanafunzi wanaanza kujifunza jinsi uandishi unavyopangiliwa, lakini hili ni jambo wanalojifunza zaidi katika masomo yao. Wanafunzi wanatakiwa wasome kitabu chote ili waweze kuona jinsi maneno yalivyoungana na jinsi hadithi au dai linavyoendelezwa. Hii ndiyo maana hakutoshi kushughulikia sauti tu.
Jinsi ya kusoma michoro, pichavivuli, vielelezo na jinsi ya kutengeneza mahusiano baina ya maumbo haya na maneno ya maandishi
Wanafunzi wanahitaji kufundishwa jinsi kugundua yale yaliyopo katika michoro, pichavivuli na vielelezo. Unaweza kuwasaidia kwa kuwauliza maswali kama vile ‘babu ameshika nini?’ ‘Kiboko ana nini mgongoni mwake?’
Kuhusu dunia na jinsi inavyojiendesha
Kadiri mwalimu anavyowasaidia wanafunzi kupanua maarifa yao ya jumla ya dunia na jinsi inavyofanya kazi, ndivyo hivyo inavyowarahisishia wanafunzi kusoma kuhusu kile kigeni na kile wasichokijua kwa sababu wanaweza kuunganisha kati ya kile ambacho tayari wana uzoevu nacho au wameshajifunza na hii taarifa mpya.
Zaidi ya yote, ni muhimu wanafunzi wafurahie kusoma na kuandika – hata wanapokutana na changamoto.
Somo la 3