Sehemu ya 2: Kuchochea hamasa katika usomaji wa hadithi

Swali Lengwa muhimu: Unawezaje kuwahamasisha wanafunzi wapende kusoma hadithi na vitabu?

Maneno muhimu: usomaji wa kushirikishana; majibu ya ubunifu; kusoma kimya; mianzo na miisho; kuchochea hamasa.

Matokeo ya ujifunzaji

Mwishoni mwa sehemu hii, utakuwa umeweza:

  • kutumia njia ya kushirikishana katika usomaji wa hadithi kwenye ufundishaji wako ili kusaidia wasomaji wanaoendelea;
  • kutumia shughuli zinazolenga mianzo na miisho mbadala katika usomaji;
  • kutalii njia mbalimbali za kukuza Usomaji Kimya Endelevu katika darasa lako.

Utangulizi

Inawezekana zaidi kwa wanafunzi kujifunza kusoma kwa ufanisi kama wanafurahia kusoma na kuandika mara nyingi iwezekanavyo. Ukiwauliza rafiki zako wanafurahia nini katika kusoma, majibu yao yanaweza kutofautiana kuanzia kwenye kurasa za magazeti ya michezo mpaka kwenye mapishi, riwaya za mapenzi, hadithi za upelelezi au wasifu –au wanaweza wasisome kabisa! Kama walivyo rafiki zako, wanafunzi mbalimbali wanaweza kufurahia kusoma aina tofauti za matini. Watavutiwa na kile wanachosoma kwa njia mbalimbali. Kazi yako ni kuwahamasisha wanafunzi wote katika darasa lako wasome kwa ufanisi na wafurahie usomaji.

Sehemu hii inalenga kuwasaidia wanafunzi wapate raha katika usomaji na wavutiwe na hadithi.

Nyenzo­rejea ya 4: Kujiandaa kwa matembezi ya kijumuiya – kipindi hicho wanafunzi watagundua chapa za kimazingira