Somo la 1

Aina ya hadithi na shughuli za usomaji wa hadithi ambazo wanafunzi wanazifurahia huenda zikatofautiana kufuatana na umri wao na ujuzi wao wa lugha iliyotumika katika hadithi hiyo. Wanafunzi wadogo zaidi na wanafunzi ambao ndio wameanza kujifunza lugha ya ziada wanafurahia wakisomewa hadithi mara kadhaa –hasa kama wana fursa ya kushiriki katika usomaji. Kwa kusoma hadithi mara nyingi na kuwatia moyo wanafunzi wasome sehemu za hiyo hadithi pamoja na wewe, unawasaidia wazoee maneno mapya na wajiamini kama wasomaji.

Lengo la Shughuli 1 ni kuandaa na kufundisha somo la kushirikishana katika usomaji. Madhumuni ya shughuli hii ni kuongeza kujiamini kwako na ujuzi kama msomaji, na kuwafanya wanafunzi wapende kusoma vitabu.

Uchunguzi kifani ya 1: Kutumia uzoevu wa hadithi za utotoni ili kuandaa shughuli za darasani

Wakati Jane Dlomo alipofikiri kuhusu enzi za utoto wake huko Rasi ya Mashariki ya Afrika Kusini, alikumbuka ni kwa kiasi gani alivyofurahia hadithi za bibi yake. Vitu viwili vilimjia akilini: kwanza kabisa, jinsi gani alivyofurahia kusikiliza hadithi zilezile na tena zaidi na zaidi na pili, jinsi gani yeye na kaka na dada zake walivyofurahia kujumuika kwenye hadithi. Wakati mwingine bibi yake aliuliza, ‘Mnafikiri kulitokea nini baadaye?’ Wakati mwingine aliwataka watoto kuonesha vitendo.

Jane aliamua masomo yake ya usomaji kwa Darasa la 4 nne yawe karibu na jinsi alivyofanya bibi yake katika hadithi. Pia aliamua kuwajaribishia shughuli ambazo zingewahusisha wanafunzi washirikiane naye katika usomaji.

Alipomwambia rafiki yake Thandi kuhusu uamuzi wake, Thandi alipendekeza kuwa washirikiane kupata vitabu vya hadithi vinavyofaa, kufanya mazoezi ya kusomeana hadithi kwa sauti na katika kufikiria njia za kuwashirikisha wanafunzi katika usomaji. Walimu wote wawili waligundua kuwa kushirikishana katika maandalizi kuliwasaidia katika kujiamini zaidi darasani. (angalia Nyenzo-rejea 1: Maandalizi kwa ajili ya usomaji wa kushirikishana ).

Nyenzo-rejea Muhimu: Kutumia usimulizi wa hadithi darasani inakupa mawazo zaidi.

Shughuli ya 1: Kushiriki kwa pamoja raha iliyo katika kitabu kizuri cha hadithi

Soma Nyenzo-rejea 1 na fuata hatua zifuatazo hapa chini: Andaa kazi ya mazoezi mengine kwa baadhi ya wanafunzi ili wayafanye wakati mnapofanya usomaji wa kushirikishana kikundi cha wanafunzi 15 au 20.

Toa maelezo ya usuli kuhusu mada ya hadithi kabla ya kuisoma hiyo hadithi.

Unaposoma, waoneshe wanafunzi vielelezo na waulize maswali kuhusiana na vielelezo hivyo. Tumia sauti yako na vitendo ili kuvuta usikivu wa wanafunzi.

Waalike wanafunzi wajiunge katika usomaji kwa kurudia maneno au sentensi kadhaa ulizoandika ubaoni na kwa kuonesha vitendo.

Mwishoni, jadilini hadithi hii na wanafunzi wako. (Angalia Nyenzo-rejea 2: Maswali ya kutumia katika usomaji wa vitabu.)

Ulijisikiaje kuhusu usomaji wako wa hadithi? Je, wanafunzi waliifurahia hadithi? Unajuaje? Unaweza kufanya nini ili kuboresha stadi zako za usomaji?

Sehemu ya 2: Kuchochea hamasa katika usomaji wa hadithi