Somo la 3

Walimu lazima wawe mifano mizuri kwa wanafunzi wao. Wanafunzi wako wanaweza kuhamasika zaidi katika usomaji kama wanakuona wewe ukisoma. Kila siku jaribu kutenga muda (angalau mara tatu kwa wiki) kwa ajili yako na wanafunzi wako wa kusoma kimya darasani. Unaweza kuchukua mfano huu kutegemeana na umri wa wanafunzi wako. Kwa mfano, wanafunzi wenye umri mdogo wangeweza kuangalia kitabu cha picha na wenzao au kumsikiliza mtu akiwasomea katika vikundi vidogo.

Usomaji Kimya Endelevu au Usomaji wa Kina (Sustained Silent Reading) huwasaidia wanafunzi wazoee kujitegemea katika usomaji na kwa kasi yao wenyewe (ambayo inaweza kuwa ya haraka sana au taratibu sana kuliko baadhi ya wanadarasa wenzao). Mlengo ni kwenye hadithi yote (au sura yote kama hadithi ni ndefu sana) na kwenye miitikio binafsi ya wanafunzi kuhusiana na kile wanachosoma. Usomaji Kimya Endelevu unaweza kufanywa kutumia kitabu cha kusoma darasani, idadi mbalimbali ya vitabu ambavyo wanafunzi wamevichagua katika maktaba ya darasa au ya shule, au kwa kutumia magazeti (kama wanafunzi wanaweza kuyatumia) – angalia Nyenzo-rejea 4: Usomaji Kimya Endelevu .

Uchunguzi kifani 3 na Shughuli Muhimu zinaonesha njia za kutathmini maendeleo ya wanafunzi kama wasomaji. (Angalia pia Nyenzo-rejea Muhimu: Kutathmini ujifunzaji .)

Uchunguzi kifani ya 3: Uzoevu wa walimu kuhusu Usomaji Kimya Endelevu

Chama cha Usomaji Tanzania kilipanga warsha iliyofanyikia Dar es Salaam, ili kuwapatia walimu utangulizi kuhusu Usomaji Kimya Endelevu. Ilielezwa kuwa moja ya malengo makuu ya Usomaji Kimya Endelevu ni kujenga ‘utamaduni wa kusoma’ miongoni mwa wanafunzi.

Walimu walialikwa kushiriki katika Usomaji Kimya Endelevu na kisha kutafakari uzoevu wao. Kila mwalimu alichagua kitabu au gazeti na kusoma kimya kwa dakika 20. Baada ya kusoma, walikuwa na dakika kumi za mjadala na wenzao watatu kuhusu kile walichokisoma na jinsi walivyoipokea ile matini. Waliporudisha vitabu na magazeti yao waliandika majina yao kwenye kitabu cha rejesta na, pembeni mwa majina yao, waliandika maoni mafupi kuhusu matini hiyo.

Walimu hawa waliamua kuwa Usomaji Kimya Endelevu ni muhimu kwa ajili ya kujenga umakinikaji na nidhamu ya mtu, kwa kujifunza msamiati mpya na mawazo mapya na kutoa maudhui ya kujadiliana na wanafunzi. Walifikiri kuwa wanafunzi wataifurahia shughuli hii na kuona fahari watakapokuwa wamemaliza kukisoma kitabu. Baadhi ya walimu waliamua kujaribu kuendesha zoezi hili kwa kutumia kikundi kidogo kimojakimoja na kuzunguka darasani kwa sababu walikuwa na vitabu vichache tu darasani.

Shughuli muhimu: Usomaji kimya endelevu

Kusanya vitabu vinavyosisimua, magazeti na hadithi ambazo zinalingana na kiwango cha wanafunzi wako. Washirikishe wanafunzi na jumuiya katika kukusanya matini zinazofaa au tumia vitabu ambavyo wanafunzi wametengeneza darasani (angalia Nyenzo-rejea 4 ). Tenga dakika 15–20 kila siku au mara tatu kwa wiki kwa ajili ya Usomaji Kimya Endelevu. Waambie wanafunzi wachague matini ya kusoma kwa ukimya. Jisomee mwenyewe wakati wanafunzi wakiwa wanasoma. Mwishoni, kama hawakumaliza kusoma vitabu vyao, waambie watumie alama zilizopo kitabuni ili watakaposoma tena iwe rahisi kujua walipoishia.

Mwambie kila mwanafunzi atoe au achangie kwenye rekodi ya usomaji (angalia Nyenzo-rejea 4).

Kila wiki, watake wanafunzi, katika vikundi vidogo, waambiane kuhusu walichokuwa wanakisoma.

Zungukia vikundi kusikiliza wanayosema wanafunzi. Kagua rekodi zao za usomaji.

Je, wanafunzi wamefurahia shughuli hii na wanasonga mbele katika usomaji wao?

Unawezaje kusaidia zaidi?

Nyenzo-rejea ya 1: Kitu ambacho waandishi na wasomaji wafanisi wanatakiwa kukijua