Somo la 2

Kujifunza namna ya kushiriki katika midahalo kunawasaidia wanafunzi (na walimu) kueleza maoni yao, kusikiliza maoni ya wenzao na kufikiri kwa umakinifu. Unapochagua mada za midahalo darasani kwako, hakikisha unachagua mada ambazo ni muhimu kwa wanafunzi wako ili waweze kueleza maoni yao.

Katika Shughuli ya 2 utawaeleza wanafunzi wako sheria na kanuni za kufanya mdahalo na kuwasaidia wanapojitayarisha kufanya mdahalo huo. Katika Uchunguzi-kifani 2, mdahalo unahusu kushirikishwa darasani. Kwa watoto wadogo, unaweza kuendesha majadiliano rahisi au mdahalo kuhusu masuala kama kutopigana.

Nyenzo-rejea 3: Muundo wa hotuba za midahalo na Nyenzo-rejea 4: Sheria na kanuni za kuendesha midahalo utakupa mwongozo. Unaweza pia kuziona sheria na kanuni hizi kuwa za manufaa kama ni mwanachama wa chama cha kuendesha midahalo.

Uchunguzi kifani ya 2: Kutayarisha na kuendesha midahalo

Baada ya mwalimu Mariam Uledi na wanafunzi wake kuandika juu ya ‘kutengwa/kutoshirikishwa’, walijadili hasa kuhusu watoto ambao hawakuwa shuleni kwa sababu kadhaa. Baadhi ya wanafunzi hawa walikuwa walemavu, wengine hawakuwa na wazazi na walikuwa ndio wanaolea/wanaosimamia familia na wengine hawakuja shuleni kwa kuwa walikuwa masikini kiasi cha kutoweza kununua sare ya shule.

Mariam alianzisha wazo la kufanya midahalo katika darasa, na kuwasilisha mada yenye kichwa kinachosema: ‘ Darasa hili linaamua kuwa “vijana wote walio nje ya shule”, waliotengwa kwa sababu ya vizingiti vya kujifunza, lazima warudishwe shuleni.’

Aliwaweka wanafunzi 36 katika vikundi sita, na akawataka nusu ya vikundi kujadili mawazo yanayounga mkono mada ya mdahalo na nusu kujadili mawazo yanayopinga mada ya mdahalo.

Baadaye aliwapa mwongozo wa kutayarisha hotuba yao (Angalia Nyenzo-rejea 3). Kila kikundi kiliandika hotuba yake, ama ya kuunga mkono au ya kupinga mada ya mdahalo, na kumchagua msemaji kutoka katika wanachama wa darasa. Mwalimu Mariam aliziangalia hotuba zao wakati wa muda wa chakula, na akawashauri wazungumzaji jinsi ya kuziboresha. Wakazirekebisha zaidi nyumbani.

Mdahalo ulifanyika siku iliyofuata. Mariamu alifurahishwa na kiwango cha juu cha ushiriki wa wanachama wote wa darasa. Hoja ilipita, na wanafunzi walianza kuwasiliana na watoto ambao hawakuwa mashuleni, na kufanya kazi na walimu wao na mwalimu mkuu ili kuwarejesha shuleni. Mariam aligundua kuwa mdahalo umeleta nafasi nzuri kwa wanafunzi kuendeleza na kueleza hoja zao na kushughulikia suala muhimu la kijamii.

Shughuli ya 2: Kufanya mdahalo wa hoja; kueleza maoni

Wafafanulie wanafunzi kuhusu kushiriki katika mdahalo

Changiana mawazo kuhusu mada zinazowafurahisha na wasaidie kujieleza katika muundo wa hoja. Amua mada za mdahalo (Angalia Nyenzo-rejea 3 ).

Fafanua sheria na taratibu za kufanya mdahalo, kwa kutumia taarifa iliyomo katika Nyenzo-rejea 4.

Andika sheria kuu na kanuni/taratibu ubaoni ili wanafunzi wazinakili kwa ajili ya marejeo katika siku za usoni.

Watake wanafunzi watayarishe hotuba za mdahalo katika vikundi na mchague msemaji mmoja kuwasilisha majadiliano yao.

Unaweza kuwasaidia kwa kuwaeleza taarifa ya utangulizi ili waitumie katika hotuba zao.

Hakikisha kama vikundi viko tayari kuanza mdahalo (labda mwishoni mwa wiki) na fuata sheria na kanuni/taratibu.

Watake wanafunzi wakueleze walichojifunza kutokana na tajiriba hii na itumie taarifa hiyo kupanga masomo ya siku za usoni na nafasi za kujadili mawazo.

Kwa watoto wadogo, unaweza kufanya mdahalo na mada zinazohusu shule, kama kwa mfano ni lazima wawe na kanuni za darasa. Unaweza kuwasaidia kujifunza namna ya kupeana nafasi ya kuzungumza na kusikiliza maoni ya wengine.