Somo la 3

Matangazo katika mabango, redio, televisheni na skrini ya kompyuta, magazeti na majarida, katika maduka au katika barua za posta, hujaribu kutufanya tutende kwa njia fulani - hasa kutumia pesa. Ni muhimu kwako na kwa wanafunzi kwelewa jinsi matangazo yanavyojaribu kufanya hili ili wewe na wanafunzi wako muyasome kwa umakinifu na pia mtambue namna ya ujanja unaotumika katika matangazo hayo.

Mwitiko wa wanafunzi katika Shughuli Muhimu zitakuonesha kama wameanza kwelewa au hawajaanza kwelewa jinsi ya kusoma matangazo kwa umakinifu.

Uchunguzi kifani ya 3: Kujifunza kusoma matangazo kwa umakinifu

Wakati mwalimu Stella Mapuga aliposhiriki katika programu ya maendeleo ya walimu, alivutiwa na shughuli za kusoma kwa umakinifu. Yeye na wenzake walilinganisha matangazo ya bidhaa ileile katika magazeti kwa ajili ya wasomaji tofauti (vijana au wazee, au watu waliotoka katika ‘jamii’ au makundi ya vipato tofauti). Waligundua kuwa picha na maneno yaliyotumika katika kutangaza bidhaa yalikuwa tofauti katika magazeti tofauti na kwamba baadhi ya bidhaa yalitangazwa katika gazeti moja tu kati ya magazeti hayo. Walimu waliangalia lugha iliyotumiwa na watangazaji. Waliangalia pia picha au michoro katika matangazo hayo. Rafiki yake na mwalimu Stella alilalamika kuwa wanawake waliotumiwa walikuwa vijana na wenye umbo la kuvutia! Mwishowe, walijadili jinsi matangazo yalivyochanganya maneno na picha katika ukurasa na walimu waliona nini kwanza walipoangalia matangazo.

Mhadhiri wao alipowauliza walichojifunza, walimu walisema wamejifunza kuangalia matangazo kwa umakinifu zaidi siku za usoni. Walijifunza kuwa wasanifu wa matangazo huteua maneno na picha ili kuwahimiza wasomaji kununua bidhaa. Wasanifu hawa huteua maneno na picha zenye ukubwa tofauti na huziweka katika ukurasa katika njia ambayo inawahimiza wasomaji kuona zaidi baadhi ya maneno au picha.

Baadhi ya walimu walisema kuwa wana hamu ya kuwaonesha wanafunzi wao jinsi matangazo yanavyojaribu kushawishi wasomaji kuchukua hatua-hasa hatua ya kununua - na kuwahamasisha kuwa wateuzi.

Shughuli muhimu: Kusoma matangazo kwa umakinifu

Tayarisha shughuli hii na iwasilishe kwa wanafunzi kwa kufuata hatua kama zilivyo kwenye Nyenzo-rejea 3: Usomaji wa matangazo kwa umakinifu. Unahitaji kukusanya maandishi ya matangazo mbalimbali au andika baadhi uliyokwishaona katika maduka ya mitaani au sokoni.

Wape matangazo hayo vikundi na watake wajadili maswali yafuatayo:

Ni bidhaa gani inayotangazwa?

Ni nani mlengwa wa kununua bidhaa au huduma hiyo?

Watangazaji wanajaribuje ‘kuuza’ bidhaa au huduma? Rejelea mawazo yaliyo katika orodha ya ubaoni

Nani haihussishwi katika tangazo hili?

Ungetaka kuwauliza maswali gani watangazaji?  

Baada ya dakika kama 15, viulize baadhi ya vikundi kutoa majibu yao.

Kwa kazi za nyumbani, watake wanafunzi kutafuta tangazo, waliweke katika daftari zao na waandike majibu ya maswali (1-5) yanayohusu tangazo hilo.

Baada ya kusahihisha kazi zao za nyumbani, panga na fundisha somo jingine ambapo wanafunzi watapanga na kutengeneza matangazo yao wenyewe. Angalia Nyenzo-rejea 4: Utengenezaji wa matangazo kwa mapendekezo ya jinsi ya kutathmini na kupanga shughuli hiyo.

Nyenzo-rejea ya 1: Uulizaji wa maswali – kuwahimiza wanafunzi kufikiri kwa umakinifu kuhusu hadithi