Somo la 2

Katika ufundishaji wa lugha ni muhimu kuzingatia maana ya lugha, kwa kukazia umuhimu wa mawasiliano, lakini wakati huohuo, kukazania ukuzaji wa uwezo wa kisarufi wa wanafunzi. Shughuli 2 inatoa mfano wa jinsi ya kutumia shairi la kusifu lililoandikwa kwa Kiingereza kufanyia kazi na wanafunzi kwa upande wa vitenzi na vielezi. Aina hii ya kazi inaweza kufanywa kwa kutumia matini za viwango mbalimbali, kwa kuzingatia viwango vya miundo mbalimbali. Vilevile, hakikisha kwamba unazingatia maana ya kipande cha maandishi, ingawa usitumie maana hiyo kwa urahisi tu kama nyenzo ya kufundishia sarufi. Ukiwa na wanafunzi wa umri mdogo, mkazo uwe kwenye maana na ufurahishaji.

Kwa kawaida hadithi hutumia njeo iliyopita, wakati maelezo aghalabu hutumia njeo iliyopo. Haya ni mazingira mazuri ya kuwapatia wanafunzi wako mazoezi ya njeo.

Kama hufundishi Kiingereza, fikiri kuhusu mada ya kisarufi ya lugha unayofundisha iliyo ngumu kwa wanafunzi, na utumie Shughuli 2 kulingana na lugha hiyo.

Uchunguzi kifani ya 2: Kujadili sarufi katika warsha ya walimu

Katika warsha iliyofanyika Tanga, walimu walikuwa na majadiliano changamfu kuhusu sarufi. Bwana Thomas Changae alishuhudia kuwa alisoma kwamba sarufi ni mifupa au kiunzi cha lugha na maneno mengine ni nyama. Vyote viwili mifupa na nyama vinachangia katika maana. Walimu walikubaliana kwamba wanafunzi wanahitaji kuendeleza welewa wao wa jinsi miundo ya lugha inavyofanya kazi, lakini pia walilalamika kuhusu wanafunzi kutopenda masomo ya sarufi.

Bi Susan Mkari alisema alijaribu kuhusisha shughuli ambazo zilikazia kwenye miundo ya lugha wakati wanafunzi wake wa Darasa la 6 wanaposoma hadithi na mashairi ya kuvutia. Kwa mfano, baada ya kufanya marudio ya njeo kuu za kitenzi cha Kiingereza, aliwaambia wanafunzi kutoa maoni yao kuhusu sababu za mwandishi wa hadithi au shairi kutumia njeo iliyopita, ya sasa au ya wakati ujao. Kisha, aliwaambia wanafunzi kuamua njeo ipi ya kitenzi au njeo zipi wanazihitaji katika kuandika hadithi au shairi lao wenyewe ili kuleta mvuto zaidi kwa wasomaji wao.

Kwa kuwa Kiingereza ni lugha ya ziada kwa wanafunzi, Bi Mkari hutengeneza chati kubwa nyuma ya kalenda za zamani. Hii huwapa wanafunzi taarifa kuhusu njeo mbalimbali za vitenzi kuhusu wakati uliopo, uliopita na ujao. (Angalia Nyenzo-rejea 3: Chati za njeo za kitenzi kwa mfano rahisi ambao unaweza kutumia na wanafunzi wako.) Anawahimiza wanafunzi wake kusoma chati hizi wanapoandika.

Shughuli ya 2: Mchezo wa ugunduzi wa kitenzi na kielezi

Toa nakala za Nyenzo-rejea 4: Shairi la kusifu . Mahali ambapo mashine za kutolea nakala hazipo, nakili shairi ubaoni au sehemu ya nyuma ya kalenda.

Mara wanafunzi watakaposoma shairi na kulielewa, waache wafanye kazi kwenye makundi kwa kutafuta vitenzi vyote vilivyomo katika shairi. Wakumbushe wanafunzi kwamba vitenzi vingi ni maneno ‘yanayoonesha kutenda’. Waambie kila kundi kuripoti mbele ya darasa kuhusu vitenzi katika ubeti mmoja (angalia Nyenzo-rejea 5: Vitenzi na vielezi katika shairi ).

Waulize wanafunzi vitenzi viko katika njeo gani. Katika ubeti wa 1 na 2, vitenzi viko katika njeo iliyopo; baadhi ya vitenzi katika ubeti wa 3 viko katika njeo ijayo na vingine katika ubeti wa 4 viko katika njeo iliyopita. Kwa wanafunzi wa kiwango cha juu zaidi, jadili kwa nini njeo hizi zilitumika.

Waulize kuna tofauti gani kwenye maana inayosababishwa na utumiaji wa njeo tofauti na athari yake kwa shairi?

Unaweza kutumia mashairi na hadithi nyingine kwa njia zinazofanana na hizi.