Somo la 2

Mara nyingi watu huwaza kwamba mwalimu lazima atumie lugha ya ziada tu darasani ili wanafunzi waweze kuwa na ufasaha katika lugha hiyo. Hili si wazo baya na linatekelezeka vizuri katika hali fulani. Hata hivyo, hali halisi katika madarasa mengi hapa Afrika ni kwamba:

hakuna wasemaji wazawa au wasemaji wajuzi (walimu au walimu) wa lugha ya ziada shuleni;

wanafunzi wana nafasi finyu sana kutumia lugha ya ziada nje ya darasa;

walimu wengi zaidi hubadilisha msimbo kwa kiasi kingi (hutumia lugha hizi kwa kuzichanganya wanapozungumza);

iwapo lugha ya ziada tu ikitumika wanafunzi hawaelewi wakati mwingi, hasa katika miaka ya mwanzo ya kujifunza lugha mpya.

Wanafunzi wanapojifunza lugha ya ziada kwa miaka michache tu, na kama hawana nafasi ya kuitumia nje ya darasa, wanaweza tu kuelewa na kutunga sentensi zinazohusiana na mambo ya kawaida ya kila siku. Aghalabu hawajawa tayari kuitumia kujadili fikira na dhana. Ili kupanua ujifunzaji ujumuishe kujadili fikira, inafaa kutumia mkabala wa utumizi wa lugha mbili.

Uchunguzi kifani ya 2: Kujadili mawazo katika lugha ya nyumbani

Huko Kibaha, Zawadi Nyangasa aliongoza darasa la 7,kipindi cha Kiingereza, katika somo lililojikita kwenye hadithi juu ya mfalme na mshona-viatu. Alitaka wafikiri juu ya hulka ya busara ya kweli na ujanja, na madhumuni ya elimu.

Alisoma hadithi kwa sauti kwa wanafunzi, akisita mara kwa mara kuuliza maswali kuona kama wameelewa.

Maswali na majibu mengi yalikuwa katika Kiingereza, lakini kulikuwa na nyakati ambapo alitumia lugha ya kwanza kuelezea dhana au kuhusisha na maisha ya wanafunzi (taz. Nyenzo-rejea 2: Mfano wa somo .)

Baada ya kusoma hadithi, aliwataka wanafunzi kujadili maswali yafuatayo, katika vikundi vidogo vya watu wanne hadi sita. Aliwahimiza kutumia lugha yao ya mama.

Unafikiri mshona-viatu alikuwa mtu mwenye elimu? Alikuwa mwenye busara? Mjanja? Mwenye furaha? Ni sababu zipi zimekufanya useme hivyo?

Ni mambo yapi muhimu tunayojifunza shuleni? Kwa nini ni muhimu?

Walitoa taarifa baadaye katika lugha yao ya mama, na walikuwa na mjadala wa kijumla juu ya maswali. Aliandika madondoo ubaoni, pia katika lugha ya mama.

Shughuli ya 2: Watu wazima ninaoheshimu

Soma Nyenzo-rejea 3: Usalama na fikiria juu ya vipengele vya usomaji ambavyo vinaweza kusababisha matatizo kwa darasa lako.

Soma kara na wanafunzi wako, huku ukijadili maneno au dhana zisizo za kawaida.

Waulize juu ya mienendo ya watu wazima.

Je, wanatenda kama wale walioelezwa katika aya tatu za kwanza za kara, au kama wale walioelezwa katika aya ya nne?

Mienendo ya watu wazima inawasaidia kama vijana? Kama inawasaidia au haiwasaidii kwa nini?

Fanya majadiliano haya katika lugha ya nyumbani/lugha mama. Kama itahimiza mjadala mzito zaidi, waruhusu wanafunzi wafanye majadiliano katika vikundi vidogo na kisha watoe taarifa baada ya kama dakika 15.

Watake wachague mtu mzima wanayemfahamu na kumheshimu na kuandika maelezo ya mtu huyu, kwa kutumia lugha watakayoiteua. (Taz. Nyenzo-rejea 4: Baba yangu ni nani ?) Wanaweza kufanya kazi wawiliwawili au vikundi vya watu watatu ay wanne.

Kusanya kazi zao na uwape mrejesho. Wanaweza kuwa na hisia-bia zilizo nzito, kwa hiyo uwajibu kwa uungawana kuhusiana na maudhui, badala ya kulenga makosa ya kisarufi, n.k. (Taz. Nyenzo-rejea muhimu: Kutathmini kujifunza.)