Somo la 3

Ufanyaji wa swali unaweza kurekebishwa ili kila mwanafunzi achangie. Kwa mfano, wanafunzi wote wanaweza kujadili kitu kinachofanya swali liwe rahisi au gumu kulifanya. Sababu inaweza kuwa kutofautiana kwa zile

nduni za juujuu –kwa mfano kutumia namba kubwa, desimali au sehemu badala ya namba nzima mara nyingi kunafanya swali liwe gumu kulifanya.

Wakati mwingine, kutunga swali kwa kuzingatia ‘muktadha’ kunaweza kulifanya liwe rahisi, lakini wakati mwingine kunaweza kuwasumbua wanafunzi kwa upande wa zile nduni za msingi za swali, hivyo wanaweza wasione kwa urahisi jinsi walivyotakiwa kulijibu.

Wanafunzi wanapoanza kuona nduni za msingi za swali, wanaweza pia kuanza ‘kuona kwa kupitia nduni hizo’ nduni za juujuu, hivyo wakaelewa kazi inayotakiwa kufanyika. Kwa jinsi hiyo wanafunzi watafanya kazi yoyote yenye nduni hizohizo za msingi kwa kujiamini. Angalia

Nyenzo-rejea 2 ili uone vipengele vya kuzingatia wakati wa kutunga na kufanya maswali pamoja na darasa lako.

Uchunguzi kifani ya 3: Tunga swali liwe rahisi, tunga swali liwe gumu

Margareta alikuwa anasomesha wanafunzi wake mada ya kugawanya. Aliandika maswali ya kugawanya ubaoni:

Asha ana machungwa12, na watoto 3. Kama akiwagawia machungwa hayo

sawasawa, kila mtoto atapata machungwa mangapi? Gawanya 117 kwa 3.

Halima ana shilingi 5,000 kwa ajili ya nauli ya kuendea kazini. Hutumia shilingi 1,500 kila siku kwa ajili ya teksi. Siku moja, hakuwa na fedha za kutosha kwa ajili ya teksi. Alikwenda kazini kwa siku ngapi? Alihitaji shilingi ngapi za teksi za kuongezea kwa ile siku moja aliyoishiwa fedha?

Aliwaambia wanafunzi katika vikundi wajaribu kufanya maswali haya kwa pamoja. Baada ya dakika kumi, Margareta aliwauliza wanafunzi wake ni maswali yapi yalikuwa rahisi sana kujibu au magumu zaidi kujibu. Kwa pamoja walitengeneza orodha mbili ubaoni –‘Mambo yanayofanya maswali yawe magumu’ na mambo yanavofanya maswali yawe rahisi’.

Margareta aliviambia vikundi vitafute ni njia ngapi wangeweza kuzitumia kufanya maswali ambayo walikuwa wamepewa. Alisema angekizawadia kikundi ambacho kingepata njia nyingi zaidi kwa kukipatia cheti cha

‘washindi wa hisabati’ kikiwa na majina yao na kukibandika kwenye ukuta wa darasa.

Shughuli muhimu: Wanafunzi wanaandika kazi zao wenyewe

Tengeneza orodha ubaoni wewe na darasa lako kuhusu ‘vitu ambavyo vinafanya maswali yawe magumu’ na ‘vitu vinavyofanya maswali yawe rahisi zaidi’.

Waambie wanafunzi wako, katika vikundi, waandike maswali matatu yao wenyewe. Lazima wafanye swali moja liwe rahisi, jingine gumu zaidi na jingine gumu kuliko yote.

Baada ya dakika kumi, viambie vikundi vibadilishane maswali waliyoandika na vikundi vingine na wafanye maswali waliyopewa na hivyo vikundi vingine.

Viambie vikundi vitoe ripoti. Je, maswali yaliyokuwa ‘magumu sana’ yalikuwa kweli ni magumu zaidi kuliko maswali ‘rahisi’? Kitu gani kilifanya maswali yawe magumu au rahisi? Pitia tena orodha zako ubaoni –kuna chochote ambacho wanafunzi wanataka kubadili au kuongeza sasa kuhusu kuyafanya maswali yawe magumu au rahisi?

Waambie watunge maswali yanayohusiana na jamii zao husika kwa ajili ya kazi ya nyumbani mf. kuhusu idadi ya miti, gharama za teksi.

Siku inayofuata, shirikishaneni maswali haya darasani na waambie wanafunzi wayafanye.

Nyenzo-rejea ya 1: Kwa nini ni muhimu kufanya maswali