Somo la 1
Sehemu hii inahusika na utangulizi wa dhana ya hesabu za sehemu. Kwa kujaribu kufanya kazi na vikundi vya ukubwa tofauti, utaweza kufikiria ni kitu gani ambacho kinafaa katika mazingira uliyo nayo na kwa kila kazi ya mazoezi. Kwa taarifa zaidi, angalia Nyenzo-rejea: Kutumia kazi ya vikundi darasani kwako.
Uchunguzi-kifani 1 na Shughuli 1 zinatumia nyenzo rahisi – tunda, karatasi na na mistari ya hesabu za sehemu– ili kuwasaidia wanafunzi waelewe dhana ya hesabu za sehemu kwa urahisi zaidi.
Pia, kwa kutumia vikundi na kuwaambia wanafunzi wajadili mahitimisho yao, utakuwa umewaonesha hesabu mbalimbali za sehemu. Welewa wa namba za sehemu ni msingi wa kufikiri kuhusu kugawanya (‘kugawana kwa’ sehemu sawa ni welewa wa kwanza wa kufahamu kugawanya), uwiano, urari na desimali.
Unaweza kwanza kutaka kuamsha welewa wako mwenyewe wa namba za sehemu kwa kuangalia Nyenzo-rejea 1: Namba za Sehemu.
Uchunguzi kifani ya 1: Kutumia kazi za vikundi ili kutalii nanba rahisi za sehemu
Bwana Umaru nchini Naijeria alianza somo lake la namba za sehemu kwa wanafunzi wake wa darasa la 5 la shule ya msingi kwa kukata chungwa katika sehemu mbili zilizo sawa na kisha kwenye sehemu nne zilizo sawa, na kuwaambia wanafunzi waandike sehemu hizo – nusu na kisha robo. Alianza kwa namba sehemu rahisi, akionesha kila sehemu kwa kukunja vipande vya karatasi katika mstatili. Alisisitiza kuwa nusu mbili zinaunda kitu kizima, n.k.
Baadaye alijadiliana na wanafunzi jinsi watu wanavyogawana vitu katika maisha halisi. Kwa kuwa darasa lake lilikuwa kubwa, aliligawa katika vikundi vidogo vitatu. Alichora duara, mstatili na mraba ubaoni na kumwambia kila mwanafunzi achague umbo mojawapo na kulichora mara sita. Aliwaambia waweke kivuli katika maumbo yao na kuonesha;
nusu
nusu mbili
robo
robo mbili
robo tatu
robo nne
Kila mwanafunzi katika kikundi aliwaonesha wenzake kile alichokifanya. Mwalimu aliwauliza kama wangeweza kuona ruwaza yoyote katika picha zao na baadhi ya wanafunzi walisema kwamba robo mbili ni sawa na nusu moja n.k. Walishirikishana jambo hili na wanakikundi wengine pamoja na darasa zima.
Ingawa darasa lake lilikuwa kubwa, Bwana Umaru aligundua kuwa mkabala wake wa kufanya kazi katika vikundi ulimaanisha kuwa wanafunzi wote walipata welewa wa awali wa namba sehemu zinazolingana kutoka kwenye michoro yao na kushirikiana na wengine. Pia aliona kuwa walikuwa wamejiandaa vema kwa ajili ya somo ambalo alikuwa amelipanga baada ya somo hili.
Shughuli ya 1: Kutumia michoro ya michoroti ya sehemu
Wapange wanafunzi katika vikundi vya wanafunzi wanne wanne. Kipatie kila kikundi makaratasi manne yenye urefu sawa ambayo yamechorwa michoroti (angalia Nyenzo-rejea 2: Michorotiya Sehemu). Katika kila kikundi, mwambie mwanafunzi mmoja akunje mstari katika sehemu mbili zilizo sawa; mwingine sehemu nne 4, na mwingine katika sehemu 8. Mtu mmoja katika kikundi asikunje karatasi.
Kwa kutumia michoroti, vikundi vinaweza kukubaliana:
Nusu (½) ngapi zinaunda kitu kizima?
Robo (¼) ngapi zinaunda nusu (½)?
Moja ya nane (⅛) ngapi zinaunda robo (¼)?
Kisha ungeweza kuwaambia wajaribu namba sehemu ambazo ni ngumu zaidi, mfano.
Kuna moja ya nane (⅛) ngapi katika nusu (½)?
Kuna moja ya nane (⅛) ngapi katika robo tatu (¾)?
Wazungukie wanafunzi wanapokuwa wakifanya kazi, ili kuwasaidia. Washirikishe wanafunzi baadhi ya majibu yao ili kuonesha mwenendo wa namba sehemu.
Sehemu ya 5: Mazoezi ya hesabu za sehemu