Somo la 1
Utambulishaji wa dhana ya ulinganifu na uakisi unahitaji maandalizi makini. Kufahamu kuwa umbo lina ulinganifu, ikiwa pande zote ziko sawa wakati mstari wa kioo unapochorwa, huchunguzwa vizuri zaidi kwa kutumia shughuli za vitendo. Unahitaji kufikiri kuhusu njia ya kuwapanga wanafunzi wako ili waweze kushiriki kikamilifu. Njia mojawapo ya kutambulisha mada hii ni kwa kutumia michoro, picha na vitu bapa kama majani. Ili kuona mistari ya ulinganifu, unahitaji kujaribu: kuangalia kipande cha karatasi kilichoinuliwa wima kwenye mstari wa ulinganifu –angalia upande mmoja, kisha mwingine; kuweka kipande cha karatasi juu ya kitu, kando ya mistari ya ulinganifu, halafu kugeuza karatasi juu yake ili kufunika nusu nyingine;
Kushika vioo vidogo vya mikononi kwenye mstari wa ulinganifu. Wanapoangalia vitu au taswira asilia, wanafunzi wako wanahitaji kuelewa kwamba tunachokiangalia ni ‘makisio tu’ ya ulinganifu. Kwa mfano, upande wa kushoto wa uso wa mtu ni yumkini usiwe sawa ‘kabisa’ kama wa upande wa kulia. Hata hivyo, kwa kutumia mifano halisi kutoka katika mazingira ya mahali hapo kama vile mitindo ya vitambaa au vitu asilia, utawahamasisha wanafunzi wako zaidi.
Uchunguzi kifani ya 1: Utumiaji wa kazi za vikundi katika kuchunguza ulinganifu
Bi Bwalya, mwalimu wa shule ya msingi kutoka Juba, Kusini mwa Sudan, alitaka kuwatambulisha wanafunzi wake katika dhana ya ulinganifu.
Aligawa darasa lake katika makundi ya wanafunzi wanne wanne, na alitoa kwa kila kundi vipande vinne vya karatasi ambavyo alivikata katika maumbo yafuatayo –mstatili, mraba, pembepacha na pembetatu sawa. Alimwambia mwanafunzi mmoja kutoka katika kila kundi achukue mstatili na kuukunja kwa namna ambayo pande mbili zilingane sawa.
Wanafunzi waliobaki katika makundi, wanaweza kutoa maoni na ushauri. Aligundua kwamba baadhi ya makundi walipata namna moja tu ya kukunja mstatili wakati wengine walipata namna mbili. Bi Bwalya aliliambia kila kundi lioneshe walichokifanya.
Kisha, alimwambia mwanakikundi mwingine kutoka katika kila kundi achukue mraba na kurudia zoezi hilo. Darasa lilikubaliana kwamba kulikuwa na namna nne za kukunja mraba. Aliliambia darasa: ‘Mistari hii inaitwa mistari ya ulinganifu. Mstatili una miwili, wakati mraba una minne.’
Alichora jedwali ubaoni kwa kuonesha maumbo na kuwaambia wanafunzi wajaze idadi ya mistari ya ulinganifu.
Kisha, aliwaambia waeleze maana ya ‘kitu linganifu’ na ‘mstari wa ulinganifu’ kwa maneno ambayo kila mmoja hapo darasani angeelewa. Baadaye, waliongeza istilahi hizi kwenye kamusi zao za hisabati.
Kwa ajili ya kazi za nyumbani, aliwaambia wakusanye vitu kutoka nyumbani au wawapo njiani kurudi nyumbani ambavyo wanafikiri vina mistari ya ulinganifu kwa uchunguzi katika somo litakalofuata.
Shughuli ya 1: Kuchunguza ulinganifu katika vitu asilia
Kabla ya somo, kusanya baadhi ya vitu asilia ambavyo vina ulinganifu unaokaribiana: vitu hivi vinaweza kujumuisha majani, maua au mboga mboga. Unaweza hata kutumia wanyama wa mahali hapo (lakini ni lazima uhakikishe kwamba wanaangaliwa vizuri) au unaweza kutumia picha zao (unaweza kuwaambia wanafunzi wakusaidie kuleta picha zao). Nyenzo rejea 1: Mifano ya ulinganifu unaopatikana kwenye vitu asilia ina picha zinazofaa na unaweza kutaka kukusanya picha zaidi kutoka magazetini na kwenye majarida, au mitindo ya vitambaa vya mahali hapo.
Gawa darasa katika makundi madogo madogo ya watu watano watano au sita sita, na liambie kila kundi litafakari kuhusu violwa au taswira na kujaribu kubainisha mistari yote yenye ulinganifu. Shirikisha mawazo yao kwa darasa zima (Angalia Nyenzo rejea Muhimu: Kutumia kazi za vikundi darasani kwa ajili ya kupanga jinsi ya kufanya zoezi hili).
Yaambie makundi yako yafikirie vitu vingine kutoka katika maisha ya kila siku ambavyo vina ulinganifu. Washauri kwamba wanaporudi nyumbani wajaribu kutafuta mifano mingine na ama waandike vitu hivyo au walete sampuli kielelezo kama inawezekana.
Katika somo litakalofuata, liambie kila kundi litengeneze bango lenye vitu sita tofauti walivyovipata ambavyo vina mistari ya ulinganifu na wachore mstari/mistari ya ulinganifu kwenye vitu hivyo. Wanaweza kuchora au labda kuchomeka baadhi ya vitu.
Onesha mabango mbele ya darasa zima ili wayaona na kujadili mawazo yako baada ya siku moja au zaidi ili kujenga kumbukumbu zao.
Sehemu ya 4: Kuchunguza ulinganifu