Somo la 1
Tunapotafiti na kufahamu juu ya kitu kipya, tunakipanga miongoni mwa vitu vyote tunavyovifahamu. Tunajenga taswira yetu kubwa (mfumo wa mpangilio) katika vichwa vyetu. Ndivyo akili ya mtu inavyofanya kazi.
Fikiria jinsi tunavyopangilia mawazo yetu ya familia. Tunaweza kuwakilisha jambo hili kwa mchoro uitwao kielelezo cha familia, ambamo watu
huwekwa mahali pao katika taswira pana (ya familia). Nyenzo-rejea 1: Kielelezo cha familia ya Kiafrika inaonesha mfano hasa wa kielelezo cha familia. Unaweza kuandaa kielelezo cha familia yako, au kile cha mtu mashuhuri, na kuwashirikisha wanafunzi mkizungumzie.
Ndivyo na elimu-viumbe ilivyo. Ukiwa mwalimu, unapaswa kuwasaidia wanafunzi wako kujenga taswira kubwa ya kufaa kuhusu viumbe hai na jinsi vinavyohusiana. Kuna mfumo wa mpangilio ambao wanasayansi wamekubaliana kwa muda mrefu. Nyenzo-rejea 2: Uainishaji wa sasa wa viumbe hai uliokubaliwa inaonesha jinsi wana-elimuviumbe wanavyopangilia viumbe hai katika makundi makubwa na baadhi ya migawanyiko ya makundi hayo.
Njia bora ya kuanza kuwasaidia wanafunzi kupanga mawazo yao kuhusu viumbe hai ni kuanza na vitu vilivyo katika mazingira yenu –vitu ambavyo wanafunzi wanavifahamu na wanaweza kuvichunguza kwa urahisi. Uchunguzi Kifani 1 unaonesha jinsi mwalimu mmoja alivyofanya jambo hili na darasa lake na Shughuli 1 inaonesha jinsi ya kutengeneza onesho darasani kwako. Kama wanafunzi wako wanaweza kuanza kuainisha (kuchangua) vitu hivi katika makundi, watakuwa wanatenda kama wanasayansi.
Uchunguzi kifani ya 1: Taswira kubwa ya viumbe hai
Wanafunzi wa Amaka Ukwu katika Nguru, Nigeria, walishangaa kukuta meza mpya mbili darasani. Bila kusema lolote, Mwalimu Ukwu aliweka kwa uangalifu kadi za kusimama mahali mahususi mezani. Kadi iliyoandikwa ‘Si viumbe hai’ meza ya kushoto na ‘Viumbe hai’, ‘Mimea’ na ‘Wanyama’ kwenye meza ya kulia.
Bi. Ukwu alitoa muda wa dakika tano kwa darasa kwenda nje kutafuta mifano mbalimbali ya vitu visivyo hai. Alizungumzia vitu walivyoleta na aliwasaidia kuweka vitu vinavyofanana katika kundi moja kwenye meza ya
‘Si Viumbe hai’. Bi. Ukwu alihakikisha vitu vya mfupa, mti, kabati na karatasi vilikuwa sehemu iliyokuwa karibu na meza za vitu hai. Kwa nini alifanya hivyo?
Kisha, kila mwanafunzi alipewa kadi ndogo ya kusimama na kutakiwa achore mmea au mnyama yoyote na kuandika jina lake nyuma. Ni lazima awe tofauti na wa wengine. Kadi hizi zililetwa mbele na kuchanguliwa, zikaoneshwa na kujadiliwa. Bi. Ukwu alihakikisha kwamba vitu vilivyofanana vilikuwa pamoja. (Alizingatia mchoro mpangilio kutoka Nyenzo-rejea 2 lakini alichagua kutowachanganya wanafunzi wake kwa kuwaambia mambo mengi mapema.)
Bi Ukwu alikamilisha somo kwa kuwataka wanafunzi wavitazame vitu visivyo hai na kuvigawa baina ya vile ambavyo mwanzoni vilikuwa hai na vile ambavyo havijawa hai hata mara moja. Wanafunzi walifanya kazi katika vikundi na walifanya majadiliano hai juu ya vitu vilivyokuwepo.
Shughuli ya 1: Kukusanya ushahidi wa maisha yaliyotuzunguka
Waambie wanafunzi wako kuwa watakuwa wanaandaa onesho la vitu visivyo hai na vilivyo hai vinavyowazunguka. Eleza kuwa haitakuwa sawa kuonesha wanyama na mimea halisi. Wasiue wala wasiharibu kitu chochote chenye uhai. Badala yake, kama wapelelezi, watafute dalili na ushahidi wa kitu chochote kilicho hai –kwa mfano, manyoya, samadi, majani na mbegu. Wape
wanafunzi siku kadhaa za kuleta vitu kwa ajili ya maonesho. Sasa zungumzia makundi utakayokuwa nayo (wanyama, mimea na kadhalika), kitu gani kinapambanua kila kundi na mahali gani kitu kilipo katika maonesho. Kisha wanafunzi wanaweza kutayarisha lebo kwa ajili ya maonesho.
Katika somo lifuatalo la sayansi, chagua vitu sita katika maonesho –vitatu vilivyo hai na vitatu visivyo hai –na uvioneshe kwenye meza nyingine.
Wakusanye wanafunzi wako kuzungukia meza na waulize ni vipi kati ya vitu sita ni hai na vipi si hai. Kwa njia ya maswali makini na mjadala huna budi kuweza kuunda orodha ya sifa saba za vitu vyenye uhai. Nyenzo-rejea 3: Sifa-pambanuzi saba za kawaida za vitu vilivyo hai inakupa mawazo kwa ajili ya kazi hii juu ya sifa-pambanuzi za mimea na wanyama.
Sehemu ya 1: Kuainisha viumbe hai