Somo la 1
Madimbwi na vilindi vya mito ya maji hushikilia mfumo wa uhai ulio changamano na wenye kuwiana. Chunguzi za mifumo ikolojia hiyo zinaweza kupangwa kwenye wazo elekezi (angalia Nyenzo-rejea Muhimu: Utumiaji wa mawazo elekezi na kupeana mawazo ili kupata majibu wakati wa kuchunguza hoja ). Halafu wanafunzi wanaweza kuongeza mawazo yao kwa kutumia rangi tofauti.
Katika Shughuli 1 tunakushauri uanze na mradi wa wazi –kutengeneza dimbwi la muda mfupi shuleni. Dimbwi hilo linaweza kukaliwa na mimea na wanyama walioazimwa toka kwenye chanzo cha mahali hapo. Itakuwa
bora zaidi kama utalihusisha darasa lako katika majadiliano kuhusu jinsi utakavyokusanya uhai toka madimbwini; na utakavyoutunza kwa usalama kwenye ‘dimbwi’ la muda. Wanafunzi watafanya chunguzi sahihi za uhai katika dimbwi la shule kwa muda wa wiki chache. Kwa kuleta uhai asili kwa muda karibu na darasa, tayari utakuwa una nyenzo ya kuendeleza chunguzi kuelekea kwenye tafakuri pana ya kisayansi.
Mara nyingi walimu hawajisikii amani wanapofanya kazi za wazi kama hizi. Lakini ni kazi ambayo ‘inamlenga zaidi mwanafunzi’; inajenga mawazo na utashi wa mwanafunzi. Ni yumkini utashangazwa na shauku ya wanafunzi wako na ubora wa juu wa kazi watakayoitoa. Kumbuka kwamba hakuna
‘majibu sahihi’ katika kazi ya wazi kama hii. Kuna uchunguzi sahihi na kuna tafakuri nzuri na ya wazi ambayo husaidia kuunda mihtasari yenye kuleta mantiki.
Uchunguzi-kifani 1 unaeleza jinsi tatizo mahsusi la kimazingira la mahali hapo linavyoweza kuwa msingi wa kazi kama hiyo. Je, una matatizo yanayofanana na hili katika eneo lako? Hii ni fursa nzuri kumwomba mtaalam wa mahali hapo kutembelea darasa lako na kuzungumza kuhusu
tatizo hilo; kumbuka kutenga muda kwa ajili ya kuandaa maswali pamoja na wanafunzi wako kabla ya kutembelewa na mtaalam (angalia
Nyenzo-rejea Muhimu: Kutumia jumuia/mazingira ya mahali hapo kama nyenzo ).
Uchunguzi kifani ya 1: Uchunguzi wa mmea shambulizi
Bongile Mpuntsha anafundisha kijijini, katika bonde la Nxarhuni (Afrika Kusini) ambako kuna maboma ya kuzuia maji (kingo) ili kushikilia mto kwa ajili ya kilimo. Lakini kuna tatizo kubwa kwenye maji. Mmea wa kigeni – gugu maji unakua kwa kutapakaa na kwa kutodhibitika; hali ya kuwa unaziba maji.
Bongile anatumia tatizo hili kama msingi wa kazi ya kisayansi. Anaanza kwa kuchunguza sampuli halisi (kielelezo) ya mmea huo. Hizi chunguzi za awali zinarekodiwa kwenye wazo elekezi la pamoja la darasa (angalia Nyenzo-rejea Muhimu: Utumiaji wa mawazo elekezi na kupeana mawazo ili kupata majibu wakati wa kuchunguza hoja ). Wanafunzi walijadili wazo elekezi, ambalo liliwaongoza kwenye chunguzi zaidi. Kisha, kutokana na yale waliyoyachunguza, walifanya kazi ya kujibu swali muhimu: Ni vigezo na mabadiliko gani yanayosababisha mmea huu mvamizi kufanikiwa namna hii?
Ni dhahiri kuwa wanafunzi wanaweza kufikiri kisayansi, endapo watapewa fursa. Bongile ameshangazwa na kufurahishwa na mihtasari yao. Yote haya yalijadiliwa na kuandikwa kwenye wazo elekezi katika rangi ya pili (angalia Nyenzo-rejea 1: Uelekezaji wa wazo).
Shughuli ya 1: Dimbwi la muda mfupi la mradi wa darasa
Jenga na imarisha dimbwi kwa kutumia Nyenzo-rejea 2: Maoni kuhusu dimbwi la muda mfupi ipo kwa ajili ya kukusaidia. Kwa hakika ni bora zaidi ikiwa maoni yatatoka kwa wanafunzi wenyewe. Kumbuka kwamba sote tunajifunza kwa kiasi kikubwa kutokana na makosa yetu –hususan wanasayansi, ambao mara nyingi hutakiwa kubadili maoni yetu kadri mradi unavyoendelea.
Pamoja na wanafunzi wako, fikirini kuhusu njia za kurekodi taarifa zihusuzo wanyama na mimea iliyomo katika dimbwi lenu. Labda mnahitaji orodha ya kukagulia au jedwali kwa ajili ya kuandika majina ya mimea na wanyama wote waliomo humo?
Ni kwa namna gani kazi ya kuchunguza inaweza kugawanywa na kuwa shirikishi miongoni mwa wanafunzi? Kurekodi kutafanyika namna gani? Je, utaweka kitabu cha kuandikia karibu na dimbwi?
Utakapokuwa na kiwango cha kutosha cha chunguzi, jaribu kuunda wazo elekezi kwa chunguzi hizo. Wazo hili litaungwaje? Unaweza kutumia kipande kikubwa cha gazeti/karatasi, ukuta au ubao wa kuandikia.
Kisha, waambie wanafunzi wako, wawili wawili au katika makundi madogo madogo, watafakari kuhusu mihtasari ambayo inaweza kuongezwa kwenye wazo elekezi kwa kutumia rangi tofauti. Unaweza kuandika herufi za mwanzo za majina ya wanafunzi pembeni ya mihtasari yao kama namna ya kuthamini kazi yao.
Sehemu ya 4: Mimea na wanyama wanavyobadilika kulingana na mazingira ili kuishi