Somo la 2
Umeme hutoa zaidi ya mwanga. Fikiria kuhusu vifaa vya kisasa tunavyotumia. Tunapata joto kutokana na umeme (majiko, pasi n.k). Tunapata mwendo (mashine ya kukatia nyasi, feni n.k). Redio na televisheni zinatupa sauti. Baadhi ya wanafunzi pia wanaweza wakawa wanajua usumaku unaweza kuwa unahusika kwa njia moja au nyingine na umeme.
Unahitaji kufikiria juu ya namna unavyoweza kuonyesha haya matokeo ya umeme kwa wanafunzi. Njia mojawapo ingekuwa ni kuwafanya wanafunzi wawe wachunguzi katika jamii yao, watengeneze orodha ya matokeo yote ya umeme wanayoyaona kuwazunguka. Au wangeweza kukata picha za vifaa vya umeme kutoka kwenye magazeti makuukuu kwa ajii ya kuzionyesha. Je unaweza kufikiria njia nyingine zinazoweza kuwafanya wanafunzi watambue matumizi ya umeme?
Katika Shughuli 2, wanafunzi wako watembelee vituo vya umeme walivyovianzisha darasani ili kuona matokeo ya umeme, huu ni mfano mzuri wa kutumia makundi kwa mzunguko. Utahitaji kufikiri namna ya kuwaambia wanafunzi waandike kile walichojifunza kwenye shughuli hii-watatengeneza mabango kwa kila kundi? Utaliambia kila kundi kuwasilisha mawazo yao darasani? Soma Uchunguzi kifani 2 kuona mwalimu mmoja alivyofanya shuguhli hii.
Baada ya shughuli, waulize wanafunzi wako kama walifurahia aina hii ya kufanya kazi. Ungewezaje kuiboresha kipindi kijacho?
Uchunguzi kifani ya 2: Kufanya kazi za makundi kwa mzunguko
Bibi Kikwete, mwalimu mzoefu wa sayansi katika shule ya msingi, aliamua kujaribu kazi za makundi kwa kuzunguka akitumia vipindi viwili na makundi kumi ya wanafunzi. Aliandaa vituo kumi vya kufanyia kazi kuonyesha matokeo ya umeme: vituo viwili kwa ajili ya shughuli za ‘joto’, viwili kwa ajili ya ‘mwendo’, viwili kwa ajili ya ‘sauti’, viwili kwa ajili ya ‘usumaku’ na viwili kwa ajili ya ‘mwanga’.
Siku moja kabla ya somo, alitengeneza kadi kumi za kufanyia kazi (Angalia Nyenzo rejea 4: Kadi za kufanyia kazi ) na akaweka kifaa kwa kila kituo cha kufanyia kazi katika boksi la viatu. Aliteua kiongozi kwa kila kundi na kupanga nao mkutano kabla ya somo ili wajiandae vizuri.
Akirejea somo, Bibi Kikwete alifurahishwa na jinsi somo lilivyoenda. Makundi yalitoka kituo kimoja hadi kingine kila dakika kumi, na viongozi walihakikisha kila mmoja alishiriki. Aliwambia wanafunzi waandae mihtasari yao wenyewe juu ya vitu walivyojifunza kutokana na somo hilo na kutoa maoni ya uzoefu wao wa kazi za makundi kwa mzunguko.
Alifurahishwa na kiasi ambacho wanafunzi walijifunza, lakini alifurahishwa zaidi na namna walivyoongelea kiukomavu mbinu ambayo aliitumia.
Shughuli ya 2: Makundi ya kazi ya mzunguko
Soma kadi za kufanyia kazi ( Nyenzo rejea 4), ambazo zinakupa maelezo juu ya vituo vya kufanyia kazi, ambavyo kila kimoja kinafafanua tukio moja la umeme. Angalia vifaa vinavyohitajika, na amua ni vituo vingapi utakuwa navyo kwa kila kadi. Andaa vifaa na vipe utambulisho sahihi.
Gawa darasa lako kwenye makundi yanayoendana na idadi ya vituo vya kufanyia kazi. (Kama una darasa kubwa na kituo kimoja tu kwa kila tukio, unaweza kufanya shughuli na nusu ya darasa kwanza).
Lieleze darasa jinsi ya kuandaa kila kituo na soma kadi za kazi kwa kila kituo na wanafunzi.
Kwa kila kundi chagua kiongozi. Wakusanye viongozi na wambie kuwa wanahusika na kuhakikisha kuwa makundi yao yanafanya kazi katika mpangilio mzuri na kila mtu kwenye kundi anashiriki. Unaposema ‘basi’ viongozi waondoke na makundi yao kuelekea kituo kingine hadi wamalize vituo vyote vitano.
Waambie viongozi warudi kwenye makundi yao na waanze kufanya kazi.
Baada ya dakika kumi sema ‘basi’. Kila kundi linaweka kifaa taratibu na linaenda kwenye kituo kingine. Fanya hivi tena baada ya dakika kumi, na kuendelea, hadi kila mmoja aone vituo vyote vitano.
Hakikisha kuwa kila kundi linaandika lilichokiona kwenye kila kituo.
Mwishoni, waambie kila kundi liwasilishe lilichokiona na mawazo yake juu ya moja kati ya vituo vitano.
Somo la 1