Utangulizi

Utunzaji katika Leba na Kuzaa

Utangulizi wa Moduli ya Utunzaji katika Leba na Kuzaa

Shirika la Afya Duniani (SAD) linadokeza kuwa zaidi ya watoto milioni 133 huzaliwa kila mwaka duniani kote, ambapo asilimia 90 yao huzaliwa katika mataifa yenye mapato ya wastani na ya chini. Kila mwaka, takriban watoto milioni 8 hufa kabla ya kufikisha umri wa miaka 5. Idadi kubwa ya vifo hivi hutokea katika kipindi cha uzaliwani (yaani muda mfupi kabla na baada ya kuzaliwa). Kima cha vifo vinavyotokea katika uzaliwani kimekadiriwa kuwa takriban vifo milioni 7 kila mwaka (visa milioni 3.5 vya kuharibika kwa mimba na milioni 3.5 katika kipindi cha siku 7 za kwanza). Idadi hii ni zaidi ya ujumuisho wa vifo vinavyosababishwa na VVU/UKIMWI (milioni 2.1), kifua kikuu (milioni 1.6) na malaria (milioni 1.3), hali inayopelekea vifo vya watu milioni 5 kote duniani. Karibu robo ya watoto milioni 7 wanaokufa katika kipindi cha uzaliwani hutokea katika kipindi cha leba na kuzaa. Visababishi vya vifo vya kipindi cha uzaliwani na vinavyotokana na kuzaa katika mataifa yanayostawi hulingana kwa karibu (kuvuja damu, matatizo ya shinikizo la damu katika ujauzito, ekilamsia, maambukizi na leba iliyofungana).

Maisha ya wanawake wengi walio katika leba na kuzaa pamoja na watoto wao yanaweza kuokolewa katika mataifa yanayostawi iwapo watahudumiwa na wakunga waliohitimu. Kote duniani, idadi ya wanawake wanaozalishwa na wakunga waliohitimu katika mataifa yanayostawi iliongezeka kutoka takriban 50% mwaka wa 1991 hadi 60% mwaka wa 2006. Malengo ya ulimwengu mzima yaliyowekwa katika kikao maalum cha Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa mnamo mwaka wa 1999 yalikuwa 80% kufikia mwaka wa 2005, 85% kufikia 2010 na 90% kufikia 2015. Hii inaonyesha kuwa mafanikio yalikuwa chini sana ya malengo yaliyowekwa, hivyo kuna haja kubwa ya juhudi zaidi. Hususan, maeneo yenye idadi ndogo zaidi ya wanawake wanaozalishwa na wakunga waliohitimu yalikuwa Afrika Mashariki (34%), magharibi mwa Afrika (41%) na Kusini ya Kati mwa Asia (47%). Pia, vifo vingi zaidi katika kipindi cha uzaliwani na vya wanawake vinavyotokana na kuzaa pia vilitokea katika maeneo haya.

Katika maeneo mengi ya kusini wa Sahara, idadi kubwa ya wanawake wajawazito huzalia nyumbani bila kuhudumiwa na wakunga waliohitimu. Pengine hii ndiyo sababu wanawake wengi huhangaikia nyumbani kutokana na matatizo ya leba iliyofungana (fistula, nafasi iliyo kati ya njia ya uzazi na viungo vingine vya ndani). Hali hii pia hupelekea vitengo vya kuzalia vya hospitali za mashambani kujaa wanawake walio na matatizo yanayosababishwa na leba iliyofungana.

Idadi kubwa ya visababishi vya vifo vinavyotokana na kuzaa na vya uzaliwani, ikijumuisha leba iliyofungana, eklamsia na kuvuja damu baada ya kuzaa, haviwezi kutabirika. Kwa hivyo, ni uwepo wa wataalam wa afya wanaosaidia wakati wa dharura katika leba na kuzaa ambao hupelekea mabadiliko makuu ya hatma ya afya mama na mtoto. Kwa kuzingatia jambo hili, pendekezo la kisasa ni kuwa kila mama anafaa kuhudumiwa na mtu aliyehitimu, iwe ni katika kituo cha afya au nyumbani. Lengo la kufanya hivi ni kuwazalisha kina mama wengi iwezekanavyo kwa njia ya kawaida, na kuwapa rufaa wanawake na watoto wanaokubwa na matatizo.

Moduli hii ya Utunzaji wa Leba na Kuzaa imeandikwa kukujuza kuhusu kanuni na utendaji wa kimsingi wa utunzaji wa kitaalam wa kuzalisha katika kiwango cha nyumbani na Kituo Kidogo cha afya. Moduli hii ina vipindi 11 vya masomo. Utajifunza kwanza kwa kina jinsi ya kutambua leba halisi, awamu mbalimbali za leba, matayarisho na maarifa ya kuzalisha kwa njia ya kawaida na kumsaidia mama katika awamu zote nne, na mbinu za kufuatilia jinsi leba inavyoendelea ukitumia chati inayojulikana kama patografu. Sehemu ya mwisho ya Moduli hii inatoa utangulizi wa mbinu za kimsingi za kumfufua mtoto mzawa, kutambua na kudhibiti hali za mtoto aliyetanguliza vibaya na kuzaa pacha, na pia kutambua na kusuluhisha hali za dharura za leba iliyofungana, kupasuka kwa uterasi na kuvuja damu baada ya kuzaa. Kanuni na mbinu zote zilizofundishwa katika moduli hii zitaimarishwa na kufafanuliwa katika mafunzo yako ya ujuzi wa kiutendaji. Kuunganisha nadharia na utendaji wa utunzaji wa leba na kuzaa ni hatua itakayokusaidia kuimarisha afya na uwezo wa kuishi wa wanawake walio katika leba na watoto katika jamii yako.