1.2.2 Damu tetelezi na kuvuja kwa kiowevu cha amnioni

Mara nyingi wakati wa ujauzito, uwazi mwembamba ulio seviksini huwa umezibwa na utetelezi. Katika siku chache za mwishoni mwa ujauzito, seviksi inaweza kuanza kufunguka. Wakati mwingine utetelezi huu na matone ya damu hutoka ukeni. Mchanganyiko huu wa damu na utetelezi huitwa damu tetelezi. Damu tetelezi hii inaweza kutoka yote kwa mara moja kama kizibo, au kuvuja pole pole kwa siku kadhaa. Ukiona damu tetelezi, fahamu kwamba seviksi inaanza kulainika, kuwa nyembamba na kuanza kufitia (kufunguka). Usidanganyike kati ya damu tetelezina mchozo wa kawaida (unyevunyevu kutoka ukeni) ambao wanawake wengi huwa nao wiki mbili kabla ya leba kuanza. Mchozo huo mara nyingi huwa ni utetelezi mwangavu wala si mwekundu kutokana na damu.

Leba halisi inaweza kuanza iwapo damu tetelezi ipo au haipo, ama kiowevu cha amnioni kinavuja au hakivuji. Kiowevu cha amnioni ni majimaji yaliyo kwenye membreni zinazozingira mtoto. Katika sehemu nyingi za Afrika, watu hufikiria kuwa leba haiendelei ikiwa hawajaona kuvuja kwa kiowevu cha amnioni ama kabla au baada ya leba kuanza. Fikira hii si kweli. Si lazima damu tetelezi na kiowevu cha amnioni kutoka ili leba ianze au iendelee.

Ikiwa leba haijaanza wala kuendelea sana katika kipindi cha saa 6 baada ya “maji kupasuka”, mhamishe mwanamke hadi kituo cha juu cha afya haraka iwezekanavyo.

Mfuko wa maji unapopasuka (kupasuka kwa membreni za fetasi), kiowevu cha amnioni kinaweza kububujika kutoka ukeni au kuvuja polepole. Kwa wanawake wengi, mfuko huu hupasuka katika vipindi vya kwanza vya leba. Ikiwa membreni ya fetasi itapasuka kabla ya leba kuanza, leba inafaa kuanza punde. Ikiwa leba haitaanza katika kipindi cha saa 6 baada ya mfuko wa maji kupasuka, maambukizi yanaweza kuingia kwenye uterasi. Hatari hii ya maambukizi huongezeka pindi wakati unapopita baada ya membreni kupasuka. Ulijifunza kuhusu kupasuka kwa membereni kabla ya wakati katika Kipindi cha 17 cha moduli ya Utunzaji wa katika Ujauzito. Kumbuka kuwa “kabla ya wakati” inarejelea kupasuka kwa membreni ya fetasi kabla ya leba kuanza. Katika muktadha huu “kabla ya wakati” hairejelei wakati wa kupevuka kwa mtoto, ambao unaweza kuwa kabla ya, wakati wa, au baada ya kupasuka kwa mfuko wa maji.

Ni kawaida kwa membreni za fetasi kupasuka baada ya leba kuanza. Walakini, hata katika kauli ya kawaida kama hii, jitahadhari na hatari zinazoambatana na kuvuja kwa kiowevu cha amnioni.

  • Hebu waza tena juu ya ulichosoma kuhusu kupasuka kwa membreni kabla ya wakati unaofaa. Ni hatari gani zinaweza kutokea ikiwa maji yatavuja wakati mwanamke yuko katika leba?

  • Matatizo yanayoweza kutokea membrani za fetasi zinapopasuka wakati wa leba ni:

    • Maambukizi: “mlango” wa uterasi umefunguka nawe unachunguza pelvisi kwa vidole baada ya kuvaa glavu mikononi ili kubaini jinsi leba inavyoendelea. Usipozingatia usafi unaweza kusambaza maambukizi kwenye uterasi (utajifunza mengi zaidi katika vikao vya masomo vitakavyofuata katika Moduli hii). Hatari hii huenea zaidi iwapo kipindi cha leba kitarefuka.
    • Kitovu kinaweza kutoka (kusukumwa nje kabla ya mtoto huku maji yakibubujika kupitia kwenye seviksi). Isitoshe, kitovu kinaweza kunaswa katikati mwa pembezo ya endometria na mtoto ambaye amesita kuelea kwenye kiowevu cha amnioni. Ikiwa kitovu kimefinywa, mtoto anaweza kupata hipoksia (kiwango kidogo cha oksijeni). Mtoto anaweza kufariki ama ubongo wake kuathiriwa iwapo damu itakwama kwenye kitovu.

    Mwisho wa jibu

1.2.1 Mikazo tosha ya uterasi ni nini?

1.2.3 Tofautisha kati ya leba halisi na leba bandia