1.3.1 Awamu ya kwanza ya leba

Wakati wa awamu ya kwanza ya leba, seviksi hufunguka pole pole kiasi cha kuwezesha mtoto kutoka kwenye uterasi. Kwa muda mrefu wakati wa ujauzito, hakuna chochote kinachoweza kuingilia au kutokea kwenye seviksi kwa sababu uwazi huo mdogo huwa umezibwa na utetelezi.

Wakati wa ujauzito, seviksi huwa ndefu na imara, kama kidole gumba cha mguu (Mchoro 1.1a) Uterasi ikikazana, seviksi hupanuka huku sehemu ya chini ya uterasi ikifupika. Pembezo za seviksi huvutwa nyuma na juu pole pole. Utaratibu huu hujulikana kama kufitika (Mchoro 1.1b na c)

Mchoro 1.1 Kufitika kwa seviksi. (a) Kabla ya leba kuanza, seviksi haijafitika. (b) 60% ya seviksi imefitika. (c) Seviksi imefitika kabisa.

Seviksi hupanuka (kipenyo huongezeka pole pole), hali inayoitwa kupanuka kwa seviksi. Kila mara inapokazana, uterasi huvuta juu sehemu ndogo ya seviksi na kuipanua. Katikati ya mikazo seviksi hulegea. Awamu ya kwanza imegawanywa katika awamu mbili: awamu fiche na awamu wazi. Awamu hizi zinatambuliwa kulingana na kiwango ambacho seviksi imepanuka.

Awamu fiche

Awamu fiche ni kipindi kati ya mwanzo wa mikazo inayofuata utaratibu hadi seviksi inapopanuka kwa kiasi cha sentimita 4. Katika awamu hii, mikazo inaweza kuwa chungu au isiyo chungu, na seviksi hupanuka pole pole. Awamu fiche huisha wakati seviksi inapoanza kupanuka kwa haraka zaidi. Ongezeko hili la kasi huashiria mwanzo wa awamu wazi.

Awamu wazi

Awamu wazi huanza wakati seviksi imepanuka zaidi ya sentimita 4. Mikazo hii hutokea kwa utaratibu maalum, mara nyingi na huwa chungu. Seviksi hupanuka haraka zaidi. Kipenyo cha seviksi kinaweza kuongezeka kwa kati ya sentimita 1.2 na 1.5 kwa saa. Kima cha kupanuka kinafaa kuwa sentimita 1 kwa kila saa. Katika awamu hii, nakili data katika patografu. (Utajifunza nakili data hii katika Kipindi cha nne katika moduli hii)

Seviksi huendelea kupanuka hadi kufika kipenyo cha sentimita 10, yaani kupanuka kabisa. Seviksi iliyopanuka kabisa ni pana vya kutosha kupitishia mtoto (Mchoro 1.2). Seviksi ikiwa na kipenyo kiasi hiki, huwezi kuihisi juu ya kichwa cha fetasi ukichunguza seviksi kwa vidole vilivyovalishwa glavu. (Uchunguzi wa uke umeelezwa baadaye katika Moduli hii na umeonyeshwa jinsi ya kuchunguza katika vikao vya mazoezi)

Mchoro 1.2 Seviksi iliyopanuka kabisa ina kipenyo cha sentimita 10.

1.3.2 Awamu ya pili ya leba