1.4.6 Kuzungukia nje (kurejea)

Baada ya kichwa cha mtoto kutoka, leba husita kwa muda mfupi. Wakati huu leba inaposita, sharti mtoto azunguke. Uso wa mtoto huzunguka kutoka kutazama uti wa mgongo wa mama hadi kutazama sehemu ya ndani ya mojawapo ya mapaja ya mama (Mchoro 1.3, mchoro wa 6). Mwendo huu huitwa kuzungukia nje kwa sababu sehemu moja ya mtoto tayari iko nje ya mwili wa mama. (Mwendo huu pia huitwa kurejea). Ni muhimu mtoto kuzunguka hivi ili kuwezesha mabega yake kutoshea kwenye pande zote na chini ya mfupa wa kinena wa mama.