2.3.2 Kuchunguza kwa kupapasa fumbatio

Kupapasa inamaanisha kuchunguza fumbatio kwa kugusagusa sehemu mahususi kwa mikono yako au kuisongesha kwa njia fulani ukitumia kiwango fulani cha nguvu. Mwambie mwanamke alale chali, akunje miguu yake magotini kisha akanyage kitanda kwa nyayo. Anafaa awe katika hali ya kuweza kuzungushwa. Wakati mwingine inakupasa usimame mbele ya miguu yake kisha upapase fumbatio lake ukielekea kichwani mwake. Wakati mwingine inakupasa usimame nyuma yake ukielekea upande wa miguu yake.Wakati mwingine inakupasa usimame nyuma yake.

  • Je unaweza kukumbuka umuhimu wa kupapasa mwanamke aliye katika leba? (Umuhimu huu ni sawa na ule wa wakati wa ujauzito. Rejelea moduli ya Utunzaji katika Ujauzito, Kipindi cha 11).

  • Kupapasa husaidia kutambua ukubwa wa fetasi, jambo ambalo husaidia kuchunguza kutanguliza kwa fetasi, yaani sehemu ya mtoto inayo “tangulia”kwenye seviksi wakati wa kuzaa. Kupapasa pia husaidia kutambua hali ya fetasi katika mwili wa mwanamke. (Kwa mfano, fetasi imeelekea mbele au nyuma?)

    Mwisho wa jibu

Aina nne za kupapasa zinajulikana kama manevazaLeopold. Ni sharti uzifanye kwa utaratibu unaofaa.

Maneva ya kwanza yaLeopold - Kupapasa fandasi

Kupapasa fandasi ni kugusagusa sehemu ya juu ya uterasi yenye umbo kubwa. (Sehemu hii ya fumbatio huitwa fandasi). Wakati wa utunzaji katika ujauzito, unafaa kupima urefu wa uterasi kutoka kwenye mfupa wa kinena wa mama hadi kwenye fandasi. Linganisha kipimo hiki na umri wa fetasi ili kutambua kama mtoto anakua vyema. Papasa fandasi ya mwanamke aliye katika leba ili kubaini jinsi mtoto anavyolala uterasini. Papasa pande zote za uterasi ukitumia viganja vya mikono yote miwili. Weka vidole vyako pamoja (Mchoro 2.4) Ipapase uterasi ili kutambua kama sehemu ya juu ya uterasi ni gumu na ya duara ama ni nyororo na isiyo na umbo maalum. Ikiwa uterasi ni nyororo na isiyo na umbo maalum na haisukumiki baada ya kuifinya kidogo, basi matako ya mtoto yako kwenye fandasi (Mchoro 2.4) na kichwa “kinaelekea chini.” Hali hii huitwa kutanguliza kichwa. Aina mbali mbali za kutanguliza kichwa zimeelezwa kwenye Kipindi cha 8. Aina inayotokea mara nyingi huitwa kutanguliza veteksi. Mtoto huzaliwa kwa urahisi zaidi ikiwa ametanguliza veteksi.

Mchoro 2.4 Kupapasa fandasi – maneva ya kwanza. Mtoto ametanguliza kichwa (Rejeleo: Shirika la Afya Duniani, 2008, Managing Prolonged and Obstructed Labour, Figure 7.4, page 115)

Ukigusa uterasi na kuhisi umbo gumu la duara kwenye fandasi, basi hicho ni kichwa cha mtoto. Ikiwa leba imeshaanza, mtoto yuko katika hali ya kutanguliza matako. (Katika hali hii, matako ndiyo sehemu inayotangulia.) Inashauriwa kumpa rufaa mwanamke aliye na mtoto ambaye ametanguliza matako, kwa sababu utaratibu wa kuzaa unaweza kuwa mgumu na kuwa katika hatari kubwa ya kuwa na matatizo. Ikiwa utahisi kama fandasi ni “tupu”, mtoto anaweza kuwa amelala kihanamu au kukingama uterasini.

Maneva ya pili ya Leopold: kupapasa pembeni

Maneva ya pili husadia kugundua hali ya fetasi: je, mtoto yuko katika hali ya longitudo (sambamba), mshazari (kukingama), au kihanamu (mlalo) uterasini? Hali ya longitudo ni ya kawaida (Michoro 2.4 na 2.5). Pendekeza rufaa ya dharura kwa mwanamke aliye na hali ya kihanam. Haiwezekani mtoto kuzaliwa kupitia ukeni akiwa katika hali hii. Daktari atafanya upasuaji wa kuzaa ili kuzalisha mtoto.

Mchoro 2.5 Kupapasa pembeni – maneva ya pili.(a) Sehemu ya nyuma ya fetasi imeelekea upande wa mbele wa mama. (b) Sehemu ya nyuma ya fetasi imeelekea upande wa nyuma wa mama. (Rejeleo: Shirika la Afya Duniani, 2008, Managing Prolonged and Obstructed Labour, Figures 7.4 and 7.5, pages 115 and 116)

Weka mikono yako kwenye sehemu za kando za katikati ya fumbatio. Sukuma polepole kwa mkono wako mmoja huku ukiimarisha mkono mwingine kushikilia uterasi. Kisha sukuma taratibu kwa mkono mwingine huku ukiimarisha ule wa kwanza. Ukihisi umbo gumu la duara, yaani kichwa cha mtoto katika upande mmoja, na fandasi ni tupu, basi mtoto yuko katika hali ya kihanamu. Mhamishe kwa dharura mama yeyote aliye katika leba na ambaye mtoto yuko katika hali ya kihanamu.

Maneva ya pili pia husaidia kubani kama mtoto ameelekea ndani au nje. Baini kwa kugusa kama umbo ni la kawaida. Ukihisi umbo kubwa nyoofu chini ya mkono mmoja, inawezekana kuwa ni mgongo wa mtoto. Mtoto huyu ameelekea upande wa ndani (Mchoro 2.5a). Ikiwa mtoto ataanza katika hali hii, itakuwa rahisi kwake kufanya miendo sabakuu akizaliwa. Ulijifunza kuhusu miendo hii katika Kipindi cha 1 (Mchoro 1.3). Ukihisi “vibonge” visivyo na umbo maalum, pengine vibonge hivyo ni miguu, magoti, na viwiko vya mtoto. Mtoto huyu ameelekea upande wa nje (Mchoro 2.5b). Ni vigumu zaidi kwa mtoto aliyeanza katika hali kuzunguka anaposhukia ukeni.

Maneva ya Leopold ya tatu: kupapasa nyonga kwa ndani

Maneva ya tatu husaidia kuthibitisha ulichohisi hapo awali kuhusu hali ya fetasi. Je, mtoto ametanguliza kichwa au matako?

  • Hali ya kutanguliza kichwa nini?

  • Katika hali ya kutanguliza kichwa, kichwa cha fetasi huelekea chini huku matako yakiwa kwenye fandasi (upande wa juu wa uterasi)

    Mwisho wa jibu

Tazama upande wa miguu ya mwanamke kisha uweke mikono yako katika sehemu ya chini ya fumbatio lake. Tumia vidole kufinya kwa utaratibu ukielekea ndani, juu ya mfupa wa kinena (Mchoro 2.6). Hisi kwa kupapasa sehemu inayaotangulia ikifungamana na seviksi. Ikiwa utahisi umbo gumu na la duara, basi sehemu inayotanguliza ni kichwa. Ikiwa ni laini na isiyo na umbo maalum, mtoto anaweza kuwa ametanguliza matako.

Mchoro 2.6 Kupapasa pelvisi kiundani. Maneva ya tatu husaidia kubaini sehemu inayotanguliza. Watoto hawa wote wametanguliza kichwa, lakini (a) yuko na kisogo kinachoelekea juu, na (b) yuko na kisogo kilichoelekea chini. (Rejeleo: Shirika la Afya Duniani, 2008, kama kwenye Mchoro wa 2.5)

Ulijifunza kuhusu majina ya mielekeo, kama vile juu na chini, katika Kipindi cha 3 cha moduli ya Utunzaji wa Wajawazito kabla ya Kuzaa, Sehemu ya 1.

Tumia maneva hii kuthibithisha ulichohisi katika maneva ya pili. Ikiwa mgongo wa mtoto umeelekea upande wako, basi kisogo chake kinaelekea juu. Kisogo ni sehemu ya nyuma ya fuvu la fetasi, kwa mtoto aliye katika hali ya juu (Mchoro 2.6a). Hali ya juu imeelekea upande wa mbele wa mama. Mtoto anayezaliwa akiwa katika hali ya kisogo kuelekea chini (Mchoro 2.6) anaweza kuwa na ugumu katika wakati wa kuzaliwa.

Maneva ya nne ya Leopold: Mshikamano wa Pawlick

Maneva ya nne pia huitwa aina ya kushika ya Pawlick. Tumia maneva hii kubaini ikiwa kichwa cha fetasi (katika hali ya kutanguliza kichwa) kimeteremka hadi pelvisi ya mama na kufungamana kwenye seviksi. (Ulijifunza kuhusu kufungamana katika Kipindi cha 1). Ili kukadiria kiwango cha kufungamana kwa kichwa seviksini, shika kichwa cha fetasi kwa vidole vyako (Mchoro 2.7). Ikiwa vidole vyote vitano vinaweza kushika kichwa kikiwa juu kiasi kwenye mfupa wa kinena wa mama, inaashiria kuwa kichwa kingali hakijafungamana seviksini. Ikiwa unaweza kushika kichwa kwa upana wa vidole viwili tu, basi kimefungamana.

Mchoro 2.7 Aina ya kushika ya Pawlick– maneva ya nne husaidia kubaini kama sehemu inayotanguliza imefungamana. (Rejeleo: Shirika la Afya Duniani, 2008 kama katika Mchoro 2.4)

2.3.1 Kuchunguza fumbatio

2.3.3 Kupima kima cha mdundo moyo