2.3.5 Kuchunguza uke

Utachunguza uke kwa sababu zifuatazo:

  • Kubaini ikiwa leba halisi imeanza na awamu iliyofikia. Seviksi imepanuka kiasi gani?
  • Kukadiria jinsi leba inavyoendelea. Je, upesi wa kupanuka kwa seviksi ni gani na fetasi imeshuka umbali upi katika uzazi?
  • Kutambua sehemu ya fetasi inayotangulia na hali ya fetasi.
  • Kutambua kufinyangika kwa mifupa ya fuvu. Je, mifupa ya fuvu imepishana kufuatia shinikizo toka misuli ya uzazi?
  • Kadiria ukubwa wa pelvisi ya mama na iwapo ni kubwa kiasi cha kupitisha fetasi.
  • Chunguza rangi ya kiowevu cha amnioni.

Kipindi hiki hulenga sababu ya kwanza tu. Sababu hizo zingine za kuchunguza uke zimeelezwa katika vikao vinavyokuja.

Kukadiria kiwango cha kupanuka kwa seviksi

Nawa mikono yako vizuri kwa kutumia sabuni na maji safi kwa muda wa dakika mbili. Kisha vaa glavu safi. Mwelezee mama yale unayodhamiria kufanya. Uke huchunguzwa kwa kutumia vidole viwili vilivyovalishwa glavu. Fanya uchunguzi wote unaohitaji kabla haujaondoa vidole ukeni. Baada ya kuviondoa, usivirudishe ukeni tena.

  • Eleza kwa nini havirudishwi ukeni?

  • Ukirudisha vidole vyako ukeni unaweza, kusababisha maambukizi.

    Mwisho wa jibu.

Usichunguze uke kwa zaidi ya kila saa 4, isipokuwa kuwepo sababu mwafaka kufanya hivyo. (Mfano wa sababu mwafaka ni kuthibitisha ikiwa awamu ya pili ya leba imeanza.)

Mwagize mama alale chali, akunje miguu yake kwenye magoti, aweke nyayo zake bapa na apanue magoti. Safisha pembeni mwa uke kwa utaratibu ukutumia shashi safi iliyotumbukizwa kwenye kiowevu cha antiseptiki. Tenganisha midomo ya uke kwa kutumia vidole viwili vya mkono usio tumika (mkono unaotumika ni ule unaotumia kuandikia). Tumbukiza vidole vyako viwili (kidole cha shahada na cha kati) katika malai ya antiseptiki kisha uviingize ukeni taratibu. Fuata mkondo wa uke, upande wa juu na nyuma. Mwagize mama avute hewa kwa nguvu na ajaribu kutulia. Mwanamke aliyetulia hatatiziki sana na utaratibu huu.

Kupanuka kwa seviksi ni ongezeko la kipenyo cha uwazi wa seviksi, linalokadiriwa kwa sentimita. Kupanuka hufanyika baada ya seviksi kufitika (seviksi inapojitandazia kwenye uterasi, inajulikana kama iliyofitika. Mchoro 1.1) Unapaswa kufanya mazoezi ya kukadiria kwa usahihi kipenyo cha uwazi wa seviksi. Zoezi 2.1 litakusaidia.

Zoezi 2.1 Jifunze kupima utanuzi wa seviksi

Chukua takriban dakika 20 kufanya zoezi hili. Unahitaji kipande cha karatasi gumu au kadi nyembamba, rula, bikari (ya kuchorea duara), penseli na makasi.

  1. Chora duara 10 katika karatasi gumu. Duara ya kwanza iwe na kipenyo cha sentimita 1. Ongeza kipenyo cha kila duara kwa ukubwa wa sentimita 1: sentimita 1, sentimita 2, hivyo hivyo, hadi sentimita 10.
  2. Wacha mpaka mpana kati ya kila duara kisha ukate kadi iwe miraba 10 yenye ukubwa sawa.
  3. Toa undani wa kila duara ukitumia makasi.
  4. Andika kiasi cha kipenyo cha kila duara kwenye kadi.
  5. Chagua duara moja kisha uingize kwenye shimo hili kidole kimoja au viwili (vinavyotumika kuchunguza uke). Je, vidole vyote viwili vinatoshea? Kisha, funga macho yako na ujaribu kukadiria kiasi cha kipenyo cha duara kwa kipimo cha sentimita.
  6. Jaribu kukadiria kipenyo cha kila duara ukiwa umefunga macho yako. Kisha, thibitisha kama uko sahihi. Rudia zoezi hili mara kadhaa.
  • Ukirejelea Kipindi cha 1 cha somo, seviksi ina kipenyo kiasi gani wakati leba inapoendelea kutoka (a) hatua fiche hadi hatua wazi katika awamu ya kwanza? (b) hatua wazi katika awamu ya kwanza hadi awamu ya pili?

  • (a) sentimita 4; (b) sentimita 10 (imepanuka kabisa)

    Mwisho wa jibu

2.3.4 Kukadiria mikazo

2.3.6 Kuchunguza sehemu ya nje ya uzazi na uke