6.2 Udhibiti tendeti katika hatua ya tatu ya leba (UTATL)

Mkunga anapotumia udhibiti tendeti katika hatua ya tatu ya leba (UTATL), hatari ya matatizo kama yalivyoorodheshwa katika Kisanduku 6.1 hupunguzwa. Neno ’’udhibiti tendeti’’ linaashiria kuwa hautasubiri hadi plasenta ijitoe yenyewe. Badala yake, unafaa kusaidia kwa namna iliyopangwa kwa utaratibu kama ifuatavyo:

 • Punde mtoto anapozaliwa, mlaze juu ya fumbatio la mama, huku miili yao ikiguzana. Wafunike wote kwa blanketi.
 • Ifinye kamba kitovu ya mtoto katika sehemu mbili ukitumia klempu, kisha ukate katikati, kama ulivyojifunza katika Kipindi cha 5.
 • Fuata hatua zilizo katika Kisanduku 6.2. Kitengo kinachofuata kinaelezea hatua hizi kwa kina.

Kisanduku 6.2 Hatua 6 za UTATL kwa mpangilio maalum

 1. Chunguza kama uterasi ina mtoto wa pili.
 2. Kwa muda wa chini ya dakika 1, mpe mama dawa ya kudungwa ndani ya uterasi, ambayo ni kemikali aina ya homoni inayofanya uterasi kukazana kwa nguvu zaidi.
 3. Tumia njia ya kuvuta kitovu taratibu.
 4. Ipapase uterasi punde tu baada ya plasenta kutolewa.
 5. Ichunguze plasenta. Hakikisha kuwa plasenta yote imetoka, wala hakuna sehemu yake iliyosalia ndani ya uterasi.
 6. Chunguza uke, periniamu na sehemu ya nje ya uke wa mama ili kutambua kama kuna mchibuko au damu inayovuja.

Hatua ya 1 Chunguza kama uterasi ina mtoto wa pili

Chunguza kama uterasi ina mtoto wa pili punde tu baada ya mtoto kuzaliwa. Papasa uterasi kupitia fumbatio la mama. Hakikisha kuwa uterasi haina mtoto wa pili. Kwa kutumia mikono, chunguza kama uterasi imerejea kimo kama cha umri wa wiki 24 za ujauzito. Baada ya kufanya hivi, nenda katika hatua ya 2. Chunguza kwa makini sana kwa sababu dawa unayompa mama kaatika hatua ya 2 hufanya uterasi ikazane kwa nguvu sana. Iwapo mtoto yuko ndani ya uterasi, anaweza kujeruhiwa. Iwapo kuna mtoto wa pili ndani ya uterasi, mpe mama dawa ya kukazisha uterasi baada ya mtoto huyu kuzaliwa.

Hatua ya 2 Mpe mama dawa ya kukazisha uterasi ili kuiwezesha kukazana

Dawa hizi za kukazisha uterasi mara nyingi hutumika katika taaluma ya ukunga:

 • misoprostol (tembe)
 • oxytocin (dawa ya kudungwa)
 • ergometrine (dawa ya kudungwa)

Dawa hizi huisaidia uterasi kukazana kwa nguvu na utaratibu maalum baada ya mtoto kuzaliwa. Dawa hizi husaidia katika kutolewa kwa plasenta na pia kuzuia damu kuvuja kwa wingi kutokana na uterasi isiyokazana. Dawa hizi tatu zinapatikana hata katika maeneo ya mapato ya chini, kama vile vijijini mwa Afrika. Hata hivyo, misoprostol inaweza kuwa dawa pekee unayoweza kutumia. Oxytocin ndiyo dawa iliyopendekezwa na Shirika la Afya Duniani, lakini haiwezi kutumika kwa sababu:

Vituo vya afya husambaziwa friji na sanduku la barafu ambazo hutumiwa kusafirishia dawa vijijini, kama ilivyoelezwa kwenye Moduli ya Chanjo

Ni sharti oxytocin na ergometrine zihifadhiwe katika kiwangojoto cha nyusi 2 -8. Dawa hizi haziwezi kutolewa katika nyumba zisizokuwa na friji au una sanduku la kubeba la barafu. Ni sharti pia dawa hizi zikingwe kutokana na mwangaza.

Vipimo vya dawa za kukazisha uterasi

Chini ya dakika moja baada ya mtoto kuzaliwa na umefinya kamba kitovu kwa klempu kisha kukata kamba kitovu, mpe mama mojawapo ya dawa zifuatazo:

 • misoprostol mikrogramu 600 (µg), yaani, tembe 3 za 200 µg za kunywewa kwa maji.

AU

 • oxytocin vipimo 10 vya kimataifa (IU) zinazodungwa ndani ya misuli ya paja la mama. Dawa hizi hujulikana kama dawa za kudungia ndani ya misuli.

AU

 • ergometrine miligramu (mg) 0.4–0.5 inayodungwa ndani ya misuli ya paja la mama.

Uterasi huwa ngumu inapokazana ifaavyo. Mabadiliko haya hutokea dakika 2 -7 baada ya kundunga dawa hii. Dawa hizi hutenda kazi kwa muda tofauti.

Ergometrine haipendekezwi kutumiwa na Wahudumu wa Afya Ugani.

Manufaa na mathara ya dawa za kukazisha uterasi

Misoprostol haina nguvu za kutenda kazi kama oxytocin. Misoprostol ina madhara zaidi ya ziada Hata hivyo, katika hali nyingi mle vijijini, ni sharti utumie misoprostol kwa sababu ni lazima oxytocin ihifadhiwe ndani ya friji au sanduku la barafu. Mshauri mama kuwa dawa hii huzuia kuvuja kwa damu, hata ingawa nafaa kutarajia madhara machache ya ziada. Dawa zote za kukazisha uterasi zina madhara ya ziada. Hata hivyo, misoprostol husababisha madhara kwa wanawake wengi zaidi. Yafuatayo ndiyo madhara ya misoprostol:

 • Mama anaweza kuanza kutetemeka saa 1 baada ya kupewa msoprostol . Kutetema huisha baada ya saa 2-6. Ishauri familia kumpa mama blanketi na chai ya “atmit” au iliyoashwa joto.
 • Ingawa ni nadra kupata kiwangojoto cha juu cha mwili, kinaweza kuanza mama anapokoma kutetema. Kiwangojoto cha juu hakiashirii ugonjwa kila kinapotambulika. Kiwangojoto cha juu huisha masaa 2-8 baada ya dawa hii kupeanwa.
 • Kuharisha hudumu kwa chini ya siku 1.
 • Kichefuchefu na kutapika huisha baada ya saa 2-6.
 • Je, manufaa makuu zaidi ya misoprostol ni yapi ikilinganishwa na dawa zingine za kukazisha uterasi.

 • Misoprotol ni tembe, hivyo hauhitaji sirinji na sindano. Misoprotol haihitaji kuhifadhiwa ndani ya friji, hivyo inaweza kutumika katika sehemu ambapo dawa zingine haziwezi kuhifadhika.

  Mwisho wa jibu

Oxytocin ndiyo dawa ya kukazisha misuli iliyopendekezwa iwapo kuna friji. Oxytocin hutenda kazi zaidi kuliko dawa zingine, na ina madhara machache zaidi. Oxytocin ni homoni inayopatikana kiasilia katika mwili wa mwanamke. Oxytocin huhusishwa kuanzia mwanzo wa mikazo ya uteras wakati wa leba, na pindi inavyoendelea. Mpe mama oxytocin ya kutengenezewa viwandani akishazaa. Dawa hii huiwezesha uterasi kuendelea kukazana taratibu, kama katika njia ya kiasili. Hata hivyo, hali hii haidumu kwa muda mrefu, hivyo ni sharti oxytocin ihifadhiwe ndani ya friji na kukingwa dhidi ya mwangaza.

Ergometrine haitumiki mara nyingi kwa sababu hii ni dawa ya kukazisha misuli yenye nguvu zaidi. Dawa hii inaweza kusababisha kufungika kwa seviksi kabla ya plasenta kutolewa. Ergometrine huchukua muda mrefu zaidi kufanya kazi kuliko oxytocin. (Baada ya kudungwa ndani ya misuli, ergometrine huchukua dakika 6-7 kufanya kazi.) Ergometrine husababisha mishtuko ya uterasi ambayo hukazana upesi huku mikazo hii ikidumu kwa muda, kinyume na mikazo ya kiasili. Hata hivyo, athari ya ergometrine hudumu kwa muda mrefu, saa 2-4.

Usitumie ergometrine katika Huduma ya Afya Ugani.Usimpe mama mwenye prieklampsia, eklampsia au shinikizo la damu. Ergometrine hufinya mishipa ya damu huku ikisababisha ongezeko la shinikizo la damu.

Hatua ya 3 Tumia njia ya kuvuta kitovu taratibu kwa msukumo pinzani.

Uterasi huwa ngumu inapokazana ifaavyo. Badiliko hili hufanyika dakika 2-3 baada ya kudunga dawa uterasini. Baada ya hatua hii, tumia njia ya kuvuta kitovu taratibu kwa msukumo pinzani ili kuitoa plasenta (Mchoro 6.2 na Kisanduku 6.3).

Unapotumia njia ya kuvuta kitovu taratibu, kumbuka KILA MARA kusuma fumbatio kwenda upande pinzani. Jambo hili hufanywa ili kuzuia kugeuka kwa uterasi. (Uterasi inapogeuka hupinduka hata sehemu yake ya ndani kuja juu kisha kutokezea ukeni.)

Mchoro 6.2 Kuvuta kitovu taratibu. Mkono wa kiume huvuuta kambakitovu iliyobanwa kwa klempu, kisha kuivuta. Wakati huo huo, mkono wa kushoto husukuma kwa msukumo pinzani kwenye sehemu ya chini ya fumbatio, juu ya mfupa wa kinena. (Rejeo: Shirika la Afya Duniani, 2008, {1} Moduli ya Elimu ya Ukunga: Kidhibiti Kuvuja Damu baada ya Kuzaa, Mchoro 1.18, uk 33)

Kisanduku 6.3 Jinsi ya kutumia njia ya kuvuta kitovu taratibu kwa msukumo pinzani

 1. Subiri hadi mishipa ya damu iliyo katika kambakitovu cha mtoto mzawa zisite kudunda. Ibane kambakitivu karibu na msamba, kisha uishika kambakitovu kwa mkono mmoja.
 2. Uweke mkono wa pili juu ya mfupa wa kinena wa mama. Lisukume fumbatio kwa msukumo pinzani ili kuiimarisha uterasi.
 3. Ikaze kambakitovu taratibu ukisubiri mkazo dhabiti wa uterasi. (Kwa kawaida, mikazo hutokea kila baada ya dakika 2-3.)
 4. Mhimize mama kusukuma sawa na mkazo dhabiti wa uterasi. Ivute kambakitovu taratibu ukiielekeza chini ili kuitoa plasenta. Endelea kuisukuma uterasi kwa msukumo pinzani.
 5. Mkazo mmoja unapokoma, ishike kambakitovu taratibu ukisubiri mkazo mwingine.
 6. Katika mkazo unaofuata, rudia utaratibu wa kuvuta kitovu taratibu kwa msukumo pinzani.
 7. Iwapo plasenta haishuki baada ya kuivuta kambakitovu taratibu kwa sekunde 30-40, usiendelee kuivuta kambakitovu.

Plasenta inapotoka, ishike kwa mikono yote kwenye vulva. Hii ni ili kuzuia membreni kuraruka, jambo ambalo linaweza kupelekea sehemu za membreni kusalia ndani ya mwili wa mama. Ishike plasenta kwa mikono yote miwili kisha uigeuze taratibu hadi membreni zipindika (Mchoro 6.3). Ivute plasenta taratibu ili kuiondoa kabisa.

Mchoro 6.3 Kutolewa kwa plasenta

Kutolewa kwa plasenta huashiria mwisho wa awamu ya tatu ya leba. Sasa uterasi inafaa kuwa ngumu, ya duara na inayoweza kusonga uterasi inapopapaswa. Unafaa kuihisi ikiwa katikati mwa kitovu cha mama na mfupa wa kinena. Uke haufai kuwa ukivuja damu. Kibofu kinafaa kuwa kitupu.

Hatua ya 4 Papasa uterasi

Ipapase uterasi punde tu baada ya plasenta kutolewa ili kuikazisha na kusitisha damu kuvuja. Wanawake wengi huhitaji kupapaswa uterasi ili kuisaidia kukazana (Mchoro 6.4).

Mchoro 6.4 Ipapase uterasi punde tu baada ya mtoto kuzaliwa. Baada ya kufanya hivyo, ipapase kila baada ya dakika 15 kwa saa 2, kisha uipapase kila baada ya dakika 30. Mwonyeshe mwanamke huyu jinsi ya kujipapasa mwenyewe, au apapaswe na jamaa zake.

Hatua ya 5 Ichunguze plasenta na tando za fetasi

Ichunguze plasenta kwa makini kuhakikisha kuwa hakuna sehemu iliyosalia ndani.

 • Kumbuka anatomi ya plasenta kutoka Moduli ya Utunzaji wa kabla ya Kuzaa, Kipindi cha 5. Je, sehemu ya juu ya mama ni upande wa juu ambapo kambakitovu hutokezea, au ni upande wa chini wa plasenta?

 • Sehemu ya juu ya plasenta ni upande wa chini, iliyo mkabala na sehemu ambapo kambakitovu hutokeza.

  Mwisho wa jibu

Kipande cha sehemu ya juu ya mama (Mchoro 6.5) kinaweza kuwa kinakosekana. Au unaweza kuona membreni ambazo zimeraruka zilizo na mishipa ya damu. Vipande hivyo vya plasenta husalia ndani ya uterasi. Mpendekezee mama rufaa ya dharura.

Mchoro 6.5 Chunguza sehemu ya chini(sehemu ya juu ya mama) ya plasenta kuthibitisha kuwa haijararuka.
Mchoro 6.6 Sehemu ya juu ya plasenta ni ile inayokabiliana na mtoto.
 • Eleza ni kwa nini unafaa kumpendekezea rufaa mwanamke aliye na plasenta ambayo ina vipande vilivyosalia ndani ya uterasi.

 • Vipande vya plasenta vilivyosalia ndani ya uterasi huongeza hatari ya kuvuja damu baada ya kuzaa.

  Mwisho wa jibu

Sehemu za duara zisizo na umbo maalum zilizo chiniya plasenta huitwa ndewe. (Baadhi ya vitabu vya masomo huziitakotilidoni. )Kinyume na matarajio, sehemu ya juu ya plasenta ni nyororo na ng’avu. Kitovu hujipandikiza upande huu, kisha kusambaa kama mishipa ya rangi ya sanawati nzito mfano wa mizizi ya mti (Mchoro 6.6).

Chunguza ili kuthibitisha kuwa plasenta ni nzima

 1. Ishike plasenta mikononi mwako, huku sehemu ya mama ikielekea juu. Hakikisha kuwa ndewe zote zipo na kuwa zimeshikana.
 2. Ishike kambakitovu kwa mkono mmoja, kisha uinin’ginize plasenta na membreni.
 3. Uweke huo mkono mwingine ndani ya membreni. Vitandaze vidole vyako kuchunguza kama membreni ni nzima (Mchoro 6.7).
Mchoro 6.7 Zitandaze membreni kuchunguza kama ni nzima
 1. Hakikisha kuwa kambakitovu imejipandikizana na plasenta kwenye sehemu ifaayo. Chunguza sehemu ya mwisho ya kambakitovu iliyokatwa kisha utafute ateri mbili na veni moja (Mchoro 6.8).
Mchoro 6.8 Sehemu ya mwisho ya kambakitovu iliyokatwa ina ateri mbili na veni moja.
 1. Itupe plasenta kwa namna inayofaa. Izike mahali ambapo haiwezi kufukuliwa na wanyama au uiangamize kwa kuchoma iwapo una vifaa vya kuchoma.
 2. Iwapo membreni zimeraruka, chunguza sehemu ya juu ya uke na seviksi ya mwanamke. Vaa glavu zilizotakaswa na utumie fosepu za sponji kuondoa vipande vyovyote vya membreni.

Iwapo vipande vya plasenta au membreni zimesalia ndani ya uterasi, mama huyu yuko hatarini.

Picha 6.9 Chunguza sehemu ya juu ya plasenta. Mfano wa plasenta umeonyeshwa. Ndewe zake zinafaa kuwa nzima. Hakuna dalili ya kuraruka plasenta inapotandazwa mkononi mwa mhudumu wa afya.

Hatua ya 6 Chunguza ili kutambua mikato, miraruko au kuvuja damu

Mchoro 6.10 Jeraha kubwa ukeni linaweza kusababisha kuvuja damu baada ya kuzaa.

Istilahi ya kimaumbile iliyo katika kifungu hiki ilielezwa na kufafanuliwa katika Kipindi cha 3 cha Moduli ya Utunzaji wa kabla ya Kuzaa, Sehemu ya 1 (Mchoro 3.2). Ili kuidhibti awamu ya tatu ya leba, fuata hatua zifuatazo:

 1. Kwa utaratibu, tenganisha labia kisha uichunguze sehemu ya chini ya uke na perineamu. Tafuta mejaraha yanayofaa kuzibwa ili kuzuia damu zaidi kuvuja (Mchoro 6.10)
 2. Kwa utaratibu, itakase vulva na perineamu kwa maji yaliyochemshwa na kupoeshwa au kiowevu hafifu cha antiseptiki.
 3. Finyilia padi au kitambaa safi kwenye sehemu inayovujia damu kwa dakika 10. Iwapo damu itaendelea kuvuja baada ya muda huu, mpendekezee mwanamke huyu rufaa mara moja. Endelea kufinya kwenye kidonda.
 4. Mfuatilie mwanamke huyu kwa dakika 15. Kadiria dalili zake muhimu, ipapase uterasi yake kuhakikisha imekazika na pia uchunguze kubaini damu inayovuja kuzidi kiasi.
 • Ni kwa nini ni muhimu kukamilisha hatua zote 6 za utaratibu wa UTATL? Utaratibu huu ni upi?

 • Ni muhimu kukamilisha hatua hizi katika utaratibu unaofaa. Utafiti unaonyesha kuwa iwapo UTATL inatumiwa vyema, inaweza kuounguza hatari ya kuvuja damu baada ya kuzaa kwa 60%. Kisanduku 6.2 kinaorodhesha hatua 6 kwa utaratibu maalum.

  Mwisho wa jibu

6.1.2 Matatizo katika awamu ya tatu ya leba

6.3 Usaidizi katika matatizo baada ya kutumia UTATL