Maswali ya Kujitathmini ya Kipindi cha 7
Kwa kuwa umekamilisha Kipindi hiki cha somo, jibu maswali haya ili utathmini kujifunza kwako. Linganisha majibu yako na Muhtasari juu ya Maswali ya Kujitathmini mwishoni mwa Moduli hii.
Kwanza soma Uchunguzi Kifani 7.1 kisha ujibu maswali yanayofuata.
Uchunguzi Maalum 7.1 Mtoto hawezi kupumua
Atsede, mwanamke wa umri wa miaka 25, aliletwa katika Kituo chako cha Afya. Alikuwa katika leba nyumbani kwake kwa muda wa saa 38. Muda tu baada ya kufika kwako, akazaa mtoto mvulana aliyetimiza umri kamili wa ujauzito. Ulimtathmini na kugundua haya: hakujaribu kupumua, hakusongesha miguu wala mikono yake, mwili wake wote ulikuwa umefunikwa na mekoniamu yenye kiowevu cha amnioni, bado hakujaribu kupumua ulipompanguza na kumpa mguso wa kumsisimua.
Maswali ya kujitathmini 7.1 (yanatathmini Malengo ya Masomo 7.2 na 7.3)
- a.Je, mtoto huyu ana asifiksia? Iwapo ndiyo, asifiksia imefika kiwango kipi?
- b.Je, hatua zako za mara moja ni zipi? Utafanya nini baadaye?
- c.Je, matatizo ya kuzaliwa kwa mtoto huyu mchanga yangezuilika, na iwapo ndiyo, kivipi?
Answer
- a.Mtoto huyu ana asifiskia kali. Unaona dalili nyingi za hatari. Hakujaribu kupumua. Hakusongesha mikono wala miguu yake. Alikuwa amefunikwa na mekoniamu na mguso wa kumsisimua haukusaidia.
- b.Hatua itakayofuata ni kumpanguza haraka na kumfunika gubigubi. Ondoa mekoniamu kwenye mdomo na pua lake kwa sirinji aina ya balbu na kitambaa safi. Sikiliza mpigo wa moyo wa apeksi. Ikiwa mpigo huu uko chini ya mipigo 60 kwa dakika, singa moyo. Singa moyo na kupitisha hewa safi kwa zamu kwa kiwango cha takriban pumzi 40 kwa dakika.
- c.Matatizo ya kuzaliwa kwa mtoto huyu mchanga yangeweza kuzuiliwa. Mtaalamu wa uzazi angemsaidia Atsede mapema katika leba yake. Mhudumu angechunguza ishara za kuathirika kwa fetasi na kumpa rufaa kwa utunzaji wa dharura. Saa 38 ni nyingi sana kungoja.
Mwisho wa jibu
Swali la kujitathmini 7.2 (linatathmini lengo la Somo 7.4)
Orodhesha vifaa vya kimsingi unavyopaswa kuwa navyo ili kumhaisha mtoto mchanga asiyeweza kupumua.
Answer
Unahitaji vifaa hivi vya kimsingi kwa kumhaisha mtoto mchanga asiyeweza kupumua:
- Vitambaa viwili safi vya kitani au pamba: kimoja cha kumpanguza na kingine cha kumfunika baadaye
- Sindano ya plastiki aina ya balbu ya kuondoa vinyeso kwenye mdomo na pua hasa kama kuna mekoniamu
- Mfuko wa ambu na barakoa za kumpa hewa safi moja kwa moja hadi mapafuni mwake
- Mtu aliyehitimu katika uwanja wa uhaishaji wa mtoto mchanga (kama wewe)
- Kifaa cha kutoa joto (taa) ili kumpa joto, ikiwezekana
Mwisho wa jibu
Swali la kujitathmini 7.3 (linatathmini Malengo ya Somo la 7.1, 7.2, 74, 7.5 na 7.6)
Je,ni kauli ipi isiyo sahihi? Eleza kisicho sahihi kwa kila kauli.
- A.Mtoto mchanga akilia mara tu baada ya kuzaliwa ni isahara kuwa asifiksia ilitokea kabla ya kuzaa.
- B.Sinosisi inamaanisha kuwa mtoto amefunikwa na mekoniamu.
- C.Mpigo wa moyo wa apeksi unaweza kugunduliwa kwa kusikiliza kifua cha mtoto kwa stethoskopu.
- D.Mbadilishano wa gesi mapafuni hutendeka dioksidi ya kaboni inapoingizwa huku oksijeni ikitolewa nje.
- E.Sindano ya vitamin K kwa watoto wachanga huzuia maambukizi ya macho.
- F.Kiwango kilichopendezwa cha kuwapa watoto wachanga hewa safi ni pumzi 40 kwa dakika.
Answer
A si sahihi. Mtoto mchanga akilia mara tu baada ya kuzaliwa huwa ishara kuwa asifiksia haijatokea au haikutokea kabla ya kuzaliwa.
B si sahihi. Sinosisi inamaanisha kuwa ngozi ina rangi ya samawati kutokana na upungufu wa oksijeni (asifiksia).
C ni sahihi. Mpigo wa moyo wa apeksi unaweza kugunduliwa kwa kusikiliza kifua cha mtoto kwa stethoskopu.
D si sahihi. Mbadilishano wa gesi mapafuni hutendeka dioksidi ya kaboni inapotolewa nje huku oksijeni ikiingizwa.
E si sahihi. Sindano ya vitamini K kwa watoto wachanga ni ya kuzuia kutokwa na damu. Lihamu ya tetrasiklini inayopakwa machoni huzuia maambukizi ya macho.
F ni sahihi. Kiwango kilichopendekezwa cha kuwapa watoto hewa safi ni pumzi 40 kwa dakika.
Mwisho wa jibu
Swali la kujitathmini 7.4 (linatathmini lengo la Somo 7.4)
Je, njia zilizopendekezwa za kumsisimua mtoto mchanga ni zipi? Je, ni njia zipi zilizo hatari na zisizoruhusiwa?
- Mpige kofi kwa mgongo.
- Fikicha fumbatio kwa upole juu na chini.
- Finya ngome ya mbavu.
- Sukuma mapaja kwenye fumbatio.
- Papasa nyayo za mtoto kwa vidole vyako.
- Panua msuli wa mkundu.
- Mwekee vishinikizo moto au baridi, au umwogeshe kwa maji moto au baridi.
- Tingisha kiungamwana.
Answer
Ni njia mbili tu zilizopendekezwa kumsisimua mtoto kwa upole:
- Fikicha fumbatio kwa upole juu na chini.
- Papasa nyayo za mtoto kwa vidole vyako.
Hizo njia zingine zote ni hatari. Usizitumie.
Mwisho wa jibu
Swali la kujitathmini 7.5
Kisanduku7.1 ni muhtasari wa baadhi ya hatari za kiafya zinazotokea sana kwa watoto wachanga na utunzaji muhimu wa mara moja kwa uzuiaji wa matatizo hayo. Baadhi ya majedwali yameachwa na mapengo ili uyakamilishe.
Hatari ya kiafya kwa mtoto mchanga | Utunzaji muhimu wa mara moja kwa Mtoto mchanga |
---|---|
Maambukizi ya macho | |
Damu kutoka yenyewe | |
Hipothemia | |
Hipoglisimia |
Answer
Kisanduku 7.1 lililokamilishwa ndilo hili.
Hatari ya kiafya kwa mtoto mchanga | Utunzaji muhimu wa mara moja kwa Mtoto mchanga |
---|---|
Maambukizi ya macho | Weka lihamu ya tetrasiklini |
Damu kutoka yenyewe | Dunga sindano ya miligramu 1 ya vitamini K kwenye msuli |
Hipothemia | Mgusano wa ngozi kwa ngozi na mama, blanketi, na kofia |
Hipoglisimia | Unyonyeshaji wa mapema au chakula mbadala cha kutosha |
Mwisho wa jibu
Muhtasari wa Kipindi cha 7