Maswali ya Kujitathmini ya Kipindi cha 8

Kwa kuwa umekamilisha Kipindi hiki cha somo, jibu maswali haya ili kutathmini ulivyojifunza. Linganisha majibu yako na Muhtasari juu ya Maswali ya Kujitathmini mwishoni mwa Moduli hii.

Swali la Kujitathmini 8.1 (linatathmini malengo ya Somo la 8.1, 8.2 na 8.4)

Je, ni maelezo yapi yaliyosahihi na yasiyosahihi? Andika maelezo sahihi kwa yale unayoona kuwa si kweli.

 • A.Fandasi: sehemu ya juu iliyo ya mviringo, ambayo ndiyo kaviti pana zaidi ya uterasi.
 • B.Mlalo wa kutanguliza matako wenye matako na miguu ya mtoto karibu na seviksi: ambapo miguu imekunjwa kwenye kiungo cha nyonga na magoti na kukunjwa chini ya mtoto.
 • C.Mlalo wa kutanguliza matako wenye matako juu ya seviksi: ambapo ni vigumu sana kuushughulikia mlalo huo wa kutanguliza matako kiasi kwamba ni lazima umweleze mama huyo bayana kuhusu jinsi uzazi huo utakavyokuwa mgumu.
 • D.Mlalo wa kutanguliza matako wenye mguu au miguu juu ya seviksi: ambapo mmoja au miguu yote imejinyoosha kiasi kwamba mtoto anatanguliza miguu ("miguu kwanza").
 • E.Haipoksia: mtoto anapopata oksijeni nyingi kupindukia.
 • F.Mimba ya zaidi ya mtoto mmoja: ambapo mama amekuwa na watoto wengi hapo awali.
 • G.Pacha wa monozaigoti: pacha wanaotoka kwenye ova moja iliyotungishwa (zaigoti). Wanaweza kuwa wa jinsia tofauti, lakini wanatumia plasenta moja.
 • H.Pacha daizaigoti (zaigotipacha): hutoka kwenye zaigoti mbili. Wana plasenta tofauti na wanaweza kuwa wa jinsia moja ua tofauti.

Answer

 • A.ni kweli. Fandasi ni sehemu ya juu iliyo ya mviringo, ambayo ndiyo kaviti pana zaidi ya uterasi.
 • B.ni kweli. Mlalo wa kutanguliza matako wenye matako na miguu ya mtoto karibu na seviksi ni ambapo miguu imekunjwa kwenye kiungo cha nyonga na magoti, na kukunjwa chini ya mtoto.
 • C.si kweli. Mlalo wa kutanguliza matako wenye matako juu ya seviksi ndiyo aina ya mlalo wa kutanguliza matako inayotokea sana na ni ambapo miguu ya mtoto imenyooshwa kuelekea juu (Picha 8.4).
 • D.ni kweli. Mlalo wa kutanguliza matako wenye mguu au miguu juu ya seviksi ni ambapo mmoja au miguu yote imejinyoosha kiasi kwamba mtoto anatanguliza miguu ("miguu kwanza").
 • E.si kweli. Haipoksia ni ambapo mtoto anakosa hewa na hua katika hatari ya kuharibika ubongo au kifo.
 • F.si kweli. mimba ya zaidi ya mtoto mmoja ni ambapo uterasi ina zaidi ya fetasi moja.
 • G.si kweli. Pacha wa monozaigoti hutoka kwenye ova moja iliyotungishwa (zaigoti). Huwa wa jinsia moja na hutumia plasenta moja.
 • H.ni kweli. Pacha wa daizaigoti (Zaigotipacha) hutoka kwenye zaigoti mbili tofauti, hutumia plasenta tofauti na wanaweza kuwa wa jinsia moja ua tofauti.

Mwisho wa jibu

Swali la Kujitathmini 8.2 (linatathmini malengo ya Somo la 8.1 na 8.2)

Je, tofauti kuu kati ya mlalo wa kawaida na usio wa kawaida wa fetasi ni zipi? Tumia istlahi sahihi za kitiba zilizo katika herufi nzito kwenye maelezo yako.

Answer

Katika mlalo wa kawaida, veteksi (sehemu ya juu kabisa ya kichwa cha fetasi) huwa ya kwanza kufika kwenye ukingo wa pelvisi ya mama. Kisogo (sehemu ya nyuma ya fuvu la kichwa cha fetasi) huangalia sehemu ya mbele ya pelvisi ya mama (kwenye simfisisi ya kinena).

Mlalo usio wa kawaida hutokea wakati ambapo veteksi haipo kwenye nafasi yake ya kawaida au mlalo mbayaukitokea. (Katika hali ambapo veteksi haipo kwenye nafasi yake ya kawaida katika mlalo wa kutanguliza veteksi, kisogo cha fetasi huangalia upande wa nyuma wa mama badala ya simfisisi ya kinena. Katika mlalo mbaya, sehemu yoyote ile isipokuwa veteksi hutangulia.) Kwa mfano, mlalo wa kutanguliza matako (matako kwanza), mlalo wa kutanguliza uso (uso kwanza), mlalo wa kutanguliza paji la uso (paji la uso kwanza), na mlalo wa kutanguliza bega (fetasi kulala kingamo).

Mwisho wa jibu

Swali la Kujitathmini 8.3 (linatathmini malengo ya Somo 8.3 na 8.5)

 1. Orodhesha matatizo yanayotokea sana kutokana na milalo mibaya au fetasi kutokuwa katika nafasi yake ya kawaida mwishoni mwa ujauzito.
 2. Je, ni hatua ipi utakayochukua ukigundua kuwa fetasi iko katika mlalo mbaya ilhali leba haijaanza?
 3. Je, ni nini usichopaswa kujaribu kufanya?

Answer

 1. Matatizo yanayojikeza sana kutokana na milalo mibaya au fetasi kutokuwa katika nafasi yake ya kawaida ni: kupasuka kwa mapema kwa membreni, leba kuanza kabla ya muda kutimia, leba kukaa sana au kuzuiliwa, uterasi kupasuka, kutokwa na damu baada ya kuzaa, kuathirika kwa fetasi pamoja na mama kunakoweza kusababisha kifo.
 2. Mpe mama huyo rufaa aende katika kituo cha juu cha afya. Huenda akahitaji huduma ya dharura ya uzazi.
 3. Usijaribu kumgeuza mtoto. Ni daktari au mkunga aliyehitimu tu anayepaswa kujaribu kumgeuza mtoto. Mgeuze mtoto kwenye kituo cha afya tu.

Mwisho wa jibu

Swali la Kujitathmini 8.4 (linatathmini malengo ya Somo la 8.4 na 8.5)

Mwanamke mjamzito amehamia kwenye kijiji chako. Tayari amefikisha majuma 37 ya ujauzito. Hujawahi kumuona. Anakueleza kuwa alizaa pacha miaka mitatu iliyopita na anataka kujua ikiwa ana pacha tena.

 1. Je, utachunguzaje kua ana pacha?
 2. Je, ukitambua ana pacha, utafanya nini ili kupunguza hatari wakati wa leba na kuzaa?

Answer

 1. Jinsi ya kuchunguza ikiwa ujauzito huu ni wa pacha:
  • Je, uterasi ni kubwa zaidi ya inavyotarajiwa katika kipindi hicho cha ujauzito?
  • Je, utersi ina umbo lipi? Je, ni mviringo, ambayo ni ishara ya pacha? Au ina umbo la moyo, ambayo ni ishara ya mimba ya mtoto mmoja?
  • Je, unahisi zaidi ya kichwa kimoja?
  • Je, unasikia midundo miwili ya moyo iliyo na tofauti ya angalau mipigo 10? (Watu wawili wasikize kwa wakati mmoja).
  • Ikiwa unaweza kukifikia kituo cha afya cha juu na bado hauna uhakika, mpeleke mwanamke kwa ukaguzi wa mawimbi sauti ya tiba.
 2. Jinsi ya kupunguza hatari katika uzazi wa pacha:
  • Chunguza na uhakikishe kuwa mama huyo hana anemia.Mhimize apumzike na kuweka miguu yake juu ili kupunguza hatari ya ongezeko la shinikizo la damu au kuvimba kwa miguu na nyayo zake.
  • Kuwa macho ili kugundua na kukabiliana na ongezeko la hatari ya ugonjwa wa ujauzito.
  • Tarajia kuwa leba yake itaanza kabla ya muda kamili kutimia. Mpeleke kwenye kituo cha afya kabla ya leba kuanza. Enda naye ikiwezekana.
  • Wasiliana na kituo hicho cha afya mapema ili waweze kutarajia rufaa kutoka kwako.
  • Hakikisha kuwa usafiri unaweza kumpeleka katika kituo cha afya patokeapo hitaji.

Mwisho wa jibu

Muhtasari wa Kipindi cha 8