10.3.3 Athari kwa mama

Athari za kuraruka kwa uterasi kwa mama hutegemea mambo matatu. Mambo haya ni kiasi cha damu iliyopotea, muda uliopita baada ya mraruko kutokea, na ikiwa kaviti ya fumbatio na mfumo wake wa mzunguko wa damu vimeambukizwa.

Kiasi cha damu iliyopotea

Kuraruka kwa uterasi ni kero linalorarua misuli ya uterasi na mishipa ya damu. Ikiwa mraruko huo utahusisha mishipa mikuu ya damu, hasa ateri za uterasi, damu inayopotea ni nyingi sana. Pasipofanyika utatuzi wa dharura haraka, upotezaji huo wa damu unaweza kusababisha kufariki kwa fetasi. Mama naye atakumbwa na mshtuko kutokana na upotezaji wa damu na kisha afariki. Mraruko ukitokea katika eneo la uterasi ambapo mishipa mikuu ya damu haijahusishwa, mwanamke ana nafasi kubwa ya kuongoka.

Muda uliopita baada ya mraruko kutokea

Wakati mwingine, wanawake hawatokwi na damu sana wala kuwa na hali inayohatarisha maisha. Wanawake hawa hubaki nyumbani kwa saa na hata siku kadhaa baada ya uterasi kuraruka. Hata hivyo, jinsi mwanamke anavyokawia kutibiwa kwa ajili ya uterasi iliyoraruka, ndivyo kiwango cha kupoteza damu , kutofanya kazi kwa figo na maambukizi yanayoenea mwilini mwake yanavyoendelea kuongezeka.

Kuwepo kwa maambukizi

Uterasi iliyoraruka hutoa mwingiliano wa moja kwa moja kati ya njia ya uzazi na kaviti ya fumbatio. Viungo vingine vya ndani vinaweza kujeruhiwa na kuvuja ndani ya fumbatio. (Sehemu za matumbo, rektamu na kibofu zinaweza kujeruhiwa.) Kutokana na haya, viini huenea kwa urahisi kwenye kaviti ya fumbatio. Viini hivi huingia kwenye mzunguko wa damu kupitia kwenye mishipa ya damu iliyoraruka. Ukuaji wa maambukizi kwenye kaviti ya fumbatio huitwa peritonitisi. Maambukizi yanayosambazwa mwilini kwenye mzunguko wa damu huitwa septisemia. Wakati mwingine, mwanamke hustahimili mraruko wa kwanza, bali hatibiwi kwa zaidi ya saa 6. Hatari ya kutokea kwa moja au matatizo haya yote yapo juu sana. Kwa hivyo, unafaa kutambua mapema kuwa mraruko umetokea. Ni lazima umpe mwanamke huyu rufaa haraka. Hatua hizi mbili ni muhimu sana kwa kuokoa maisha ya mama huyo.

Matatizo yanategemea kiasi cha damu iliyopotea, muda uliopita baada ya uterasi kuraruka na hali ya maambukizi yoyote yale. Mwanamke aliye na uterasi iliyoraruka anaweza kukumbwa na baadhi au matatizo haya yote.

Mshtuko utokanao na upotezaji wa damu

Mshtuko utokanao na upotezaji wa damu unaua kwa haraka sana. Mama huwa anahisi dalili hizi:

  • Kupoteza fahamu, kizunguzungu, udhaifu au kuchanganyikiwa
  • Kukwajuka kwa ngozi, na jasho baridi
  • Mpwito wa haraka wa ateri (zaidi ya mipigo 100 kwa dakika) au haraka sana hadi kutoweza kunakiliwa
  • Shikiniko la damu linaloshuka kwa kasi au lisiloweza kunakiliwa
  • Kupumua kwa haraka (zaidi ya pumzi 30 kwa dakika)
  • Wakati mwingine kupoteza fahamu
  • Kupungua sana au kutokuwepo kwa mkojo

Mshtuko wa sepsisi

Mshtuko wa sepsisi hutokea iwapo mraruko au kutokwa na damu kumesababisha septisemia. Ishara zinafanana na zile za mshtuko utokanao na upotezaji wa damu, bali pamoja na kiwango cha juu sana cha joto mwilini (zaidi ya sentigredi 38).

Matatizo mengine

  • Peritonitisi: maambukizi kwenye kaviti ya fumbatio.
  • Kutofanya kazi kwa figo kutokana na kiasi kidogo cha damu.
  • Takribani visa vyote viletwavyo hospitalini hudhibitiwa na histerektomi. (Katika histerektomi, uterasi huondolewa) Kwa hivyo mwanamke hawezi kupata watoto zaidi.
  • Je, ni nini kinachofanyika kwa fetasi uterasi inapoelekea kuraruka na punde baada ya kuraruka?

  • Kabla ya mraruko, kiwango cha mpigo wa moyo kiko zaidi ya mipigo 160 kwa dakika au chini ya mipigo 120 kwa dakika. Baada ya mraruko, uterasi hujifunga kwenye mwili wa fetasi. Damu humiminika kwenye kaviti ya fumbatio na fetasi kufariki haraka ila upasuaji wa haraka uitoe.

    Mwisho wa jibu

10.3.2 Ishara Zinazoonyesha kuwa uterasi imeraruka

10.4 Utatuzi wa uterasi iliyoraruka