Maswali ya Kujitathmini ya Kipindi cha 11
Kwa kuwa sasa umekamilisha kipindi hiki, jibu maswali yafuatayo ili kubaini jinsi ulivyojifunza. Unaweza kudhibitisha majibu yako ukilinganisha na vidokezo ulivyoandika katika Maswali ya Kujitathmini yaliyo mwishoni mwa Moduli hii.
Swali la Kujitathmini 11.1(linatathmini Matokeo ya Somo la 11.1)
Unahitajika kuandika habari iliyoonyeshwa hapa ili kuituma pamoja na ilani ya rufaa kwa mama aliye na hali ya kuvuja damu baada ya kuzaa. Mkurufunzi mwenzako mchanga amekuuliza umweleze ulichoandika. Eleza dondoo lako la rufaa ili mwenzako aweze kuelewa. Jumuisha maneno yote yaliyoandikwa kwa herufi kubwa.
“Nataka kumpa rufaa Mebrihit. Yeye ni mama aliye na usawa wa kiwango cha juuna anatokwa nadamu kupita kiasi. Naamini kuwa ana hali ya kimsingi ya kuvuja damu baada ya kuzaa. Nilikuwa mwangalifu ili kumkinga dhidi ya jeraha nilipomsaidia kuzaa. Kumpapasa huashiria kuvuja damu baada ya kuzaa kunakohusiana na mikazo, hali ambayo nakisia kuwa imesababishwa na matatizo ya miometriamu.”
Answer
Unaweza kumwelezea mkurufunzi mwenzako dondoo lako la rufaa namna hii:
"Nataka kumpa rufaa Mebrihit. Yeye amekuwa na zaidi ya mimba 5 (usawa wa kiwango cha juu) na akatokwa na damu ya zaidi ya mililita 500 (kuvuja damu kupita kiasi) katika saa 24 za kujifungua (hali ya kimsingi ya kuvuja damu baada ya kuzaa ). Nilikuwa makini ili kumkinga na jeraha lolote (jeraha) wakati wa kuzaa. Ninapoliguza fumbatio lake (kupapasa), nilihisi kuwa uterasi yake ni laini na haijajikaza vyema baada ya kuzaa (kuvuja damu baada ya kuzaa kunakohusiana na mikazo). Nashuku kuwa misuli ya pembezo za uterasi yake (miometriamu) haikazani vyema ili kuweza kuifunga mishipa ya damu katika sehemu ambapo plasenta ilitengana na uterasi.
Mwisho wa jibu
Swali la Kujitathmini la 11.2 (linatathmini Malengo ya Somo la 11.2 na 11.3)
Unamchunguza mwanamke mjamzito aliye chini ya utunzaji wako ili kubaini iwapo ana hatari ya kuvuja damu baada ya kuzaa.
- a.Ni maswali gani utakayomuuliza na ni nini utayokumbuka kuchunguza kama sehemu ya ziara zako za utunzaji wa wakati wa ujauzito?
- b.Ni uchunguzi na huduma zipi za dharura utakazomtolea wakati wa leba na kuzaa?
Answer
Uliza maswali haya na pia ufanye mambo haya. Unaweza kutaja mengine zaidi.
- a.Utunzaji wa wakati wa ujauzito: Maswali ya kuuliza na mambo ya kubaini:
- Je, amezaa kwa mara ya kwanza (primipara) au tayari amezaa mara mbili au zaidi (maltipara)? Kina mama maltipara wako katika hatari ya juu zaidi ya kupata hali ya kuvuja damu baada ya kuzaa inayohusiana na mikazo.
- Ikiwa mama ni maltipara, je, mtoto wake wa awali alikuwa mzito sana (zaidi ya kilogramu 4) au alipata mapacha? Mojawapo ya mambo haya yanaweza kupanua uterasi kupita kiasi.
- Je, mama huyu anakumbuka ikiwa alikuwa na kiowevu kingi zaidi cha amnioni katika ujauzito wake wa hapo awali (polihidrominiosi)? Zaidi ya lita 3 inaweza kupanua uterasi kupita kiasi.
- Je, umefanya uchunguzi wa kutumia picha kubaini kama ana anemia? (Fanya uchunguzi wa kutumia picha kuchunguza anemia katika utunzaji wa baada ya kuzaa pia). Ikiwa ana anemia, umemshauri kuhusu lishe bora?
- Je, mpango wa usafirishaji wa kijamii uko tayari iwapo rufaa ya dharura itahitajika?
- b.Wakati wa, na baada ya kuzaa: Hatua za dharura za kuchukua na mambo ya kuchunguza:
- Hakikisha kuwa anakojoa mara nyingi. (Kibofu kitupu hakitatizi mikazo ya kawaida ya uterasi) Pia anafaa kukojoa punde tu baada ya kuzaa.
- Tumia patografu ili kufuatilia jinsi leba inavyoendelea. Patografu hii inakuwezesha kutambua kwa haraka dalili zozote zinazoweza kupelekea hali ya kuvuja damu baada ya kuzaa. (Kwa mfano, kizuizi kinaweza kusababisha kupasuka kwa uterasi).
- Usimshauri mama huyu kusukuma mtoto nje kabla ya seviksi kupanuka hadi mwisho. Toa usaidizi wa kuvuta kichwa na mabega ya mtoto taratibu ili kuzuia majeraha.
- Mshauri na umsaidie mama huyu kunyonyesha haraka iwezekenavyo. (Mama ataanza kujitolea oxytocin yake itakayochochea uterasi kujikaza.)
- Hakikisha kuwa plasenta imetengana kabisa na kuwa ni nzima. Isugue uterasi kila dakika 15 katika saa 2 za kwanza ili kuwezesha uterasi kujikaza vizuri.
Mwisho wa jibu
Swali la Kujitathmini 11.3 (linatathmini Malengo ya Somo la 11.4)
Gelila alizaa dakika 40 zilizopita. Ulimpa miligramu 600 za misoprostol kwa njia ya mdomo muda tu baada ya kuzaa lakini plasenta bado haijatoka. Amekojoa. Baada ya dakika 10 plasenta yake inatoka na unahakikisha kuwa ni nzima, lakini Gelila anaanza kuvuja damu kwa wingi. Utafanya nini?
Answer
Fanya mambo haya:
- Paza sauti mara moja kuwaita familia na majirani wa Gelila. Washauri kuandaa usafirishaji iwapo ataendelea kuvuja damu kwa wingi na ni sharti aende katika kituo cha afya kilicho karibu.
- Chunguza kiwango chake cha kuvuja damu. Hali hii isipopungua kwa haraka, chukulia kuwa ni kuvuja damu baada ya kuzaa kunakohusiana na mikazo.
- Ikiwa alipata miligramu 600 ya misoprostol baada ya kuzaa, mpe kipimo cha pili cha miligramu 400 ya misoprostol kupitia rektamu au chini ya ulimi ili kuwezesha uterasi kujikaza. Ikiwa alipewa oxytocin hapo awali, mpe UI 10 nyingine kwa kumdunga sindano ndani ya misuli.
- Mlaze Gelila chali huku miguu yake ikiwa katika kipeo cha juu ya kichwa, mfunike kwa blanketi na uhakikishe kuwa ana joto.
- Ikiwa umefunzwa kufanya haya, mdunge sindano iliyo na viowevu vya vena kabla ya rufaa.
- Isugue uterasi ili kuiwezesha kujikaza. Ikiwa hatua hii haifaulu, jaribu kufinya uterasi yake kwa kutumia mikono miwili. Ikiwa damu itakoma kuvuja na uterasi ianze kuwa dhabiti, ondoa shinikizo pole pole. Ikiwa damu haitakoma kuvuja, endelea na utaratibu wa kutoa rufaa na umfikishe mama huyu katika kituo cha afya haraka iwezekanavyo.
- Andamana na Gelila hadi katika kituo hicho cha afya. Chunguza dalili zake kuu na uendelee kumtilia viowevu ndani ya mshipa. Hakikisha kuwa mtoto wake pia analetwa hospitalini na kuna watu wanaofaa wa kumtunza na kumtolea damu.
- Nakili kila hatua uliyochukua katika dondoo zako za rufaa. Jumuisha pia historia ya Gelila na habari za kina kuhusu utambulisho wake.
Mwisho wa jibu
Muhtasari wa Kipindi cha 11