11.2.1 Visababishi vya kuvuja damu kunakohusiana na mikazo

Hali yoyote inayotatiza mikazo ya uterasi huongeza hatari ya kuvuja damu kupita kiasi. (Hali hizi ni plasenta iliyosalia, mabaki ya tishu za plasenta, au kusalia kwa tando za amanioni au kuganda kwa damu ndani ya uterasi.) Ikiwa plasenta imejitenga lakini ingali imebakia uterasini, hata kama ni kipande kidogo, uterasi haiwezi kujikaza. Hata kipande kidogo cha plasenta au donge la damu lililosalia ndani ya uterasi linaweza kufanya uterasi kutojikaza. Uterasi isipojikaza, mishipa ya damu ya mama itaendelea kuvuja. Mwanamke atapoteza damu haraka.

Tatizo kuu la kuvuja damu baada ya kuzaa ni kuwa huwezi kubashiri ni nani atakayevuja damu kupita kiasi baada ya kuzaa. Hali hii ngumu husababishwa na ukweli kwamba thuluti mbili ya wanawake waliokabiliwa na tatizo hili hawana vipengele vya hatari vinavyojulikana. Hivyo basi, ni sharti ukumbuke kuwa wanawake wote wamo katika hatari ya kukumbwa na tatizo hili. Kukinga kuvuja damu baada ya kuzaa ni sehemu ya lazima katika kila tukio la kuzaa. Ufuatao ndio muhtasari wa vipengele vikuu vya hatari vinavyojulikana.

Kutatizwa kwa uwezo wa uterasi kujikaza

Mhudumu hawezi kubashiri wala kuzuia uterasi isiyoweza kujikaza. Hata hivyo, ukifahamu vipengele vinavyopelekea uwezekano wa kuvuja damu, unaweza kujitayarishia dalili hizi zinazoweza kutokea za hali ya kuvuja damu baada ya kuzaa inayohusiana na mikazo:

 • Kizuia privia ya plasenta au kutengeka mapema kwa plasenta: Katika hali zote mbili, nyuzi za misuli ya miometriamu huwa zimejeruhiwa katika sehemu ya plasenta.
 • Plasenta iliyosalia: Plasenta yote au kipande chake husalia ndani ya uterasi. Plasenta iliyosalia uterasini hutatiza mikazo ya kawaida ya misuli katika sehemu ya plasenta.
 • Kutengeka nusu kwa plasenta: Sehemu ya plasenta hutengeka kutoka katika pembezo za uterasi huku sehemu nyingine ikisalia imebandikika humo.
 • Kibofu kilichojaa: Uterasi imekaribiana na kibofu. Kibofu kikijaa kinaweza kutatiza mikazo ya kawaida ya uterasi katika wakati wote wa leba na baada ya kuzaa.
 • Usawa wa ujauzito: Mwanamke aliyewahi kupata mimba zaidi ya mara tano. Misuli ya miometriamu inaweza kukosa uwezo wa kujikaza kwa udhabiti kwa sababu imejikaza mara nyingi.
 • Mimba nyingi:Ni sharti uterasi ipanuke ili kutoa nafasi ya watoto wawili au zaidi (Kipindi cha 10). Baada ya kuzaa, uterasi iliyopanuka sana inaweza kuchukua muda mrefu kabla ya kujikaza kabisa.
 • Polihidramniosi: Kiowevu kingi cha amanioni (zaidi ya lita 3) kinachomzingira mtoto kinaweza kupanua uterasi kupita kiasi kama vile katika mimba nyingi.
 • Mtoto mkubwa: Mtoto mwenye uzito zaidi ya kilogramu 4.0 anaweza kupanua uterasi kupita kiasi.
 • Leba iliyodumu kwa muda mrefu: Leba inapochukua zaidi ya saa 12 (Kipindi cha 9), misuli ya miometriamu inaweza kuchoka. Muda mrefu wa mikazo hufanya misuli kukosa kujikaza vyema (utepetevu wa uterasi).

Anemia katika mama

Anemia ni ukosefu wa seli nyekundu za damu kufuatia kiwango cha chini cha hemoglobini. Anemia humweka mama katika hatari ya kupata hali ya kuvuja damu baada ya kuzaa, kwa kuwa damu yake haiwezi kuganda haraka kama vile katika mtu asiye na anemia. Kupoteza damu ni hatari mno kwa mtu mwenye anemia. (Ulijifunza jinsi ya kutambua na kudhibiti anemia wakati wa ujauzito katika kipindi cha Somo cha Moduli ya Utunzaji wa Wakati wa Ujauzito.)

Udhibiti duni wa awamu ya tatu ya Leba

Kipindi cha 6 kinaeleza jinsi ya kudhibiti kikamilifu utaratibu wa kutoa plasenta na mambo yanayofaa kuepukwa.

 • Je, mbinu sahihi ya kuhusika kikamilifu katika kusaidia kutoa plasenta imepewa jina gani?

 • Mbinu hii huitwa kuvuta kambakitovu taratibu.

  Mwisho wa jibu

 • Je, ni hatua gani isiyo sahihi ambayo mkunga anapaswa kuepuka katika awamu ya tatu ya leba inayoweza kusababisha kuvuja damu baada ya kuzaa?

 • Usijaribu kutoa plasenta kabla haijatengana na pembezo za uterasi. Usiisukume fandasi ya uterasi unapovuta kambakitovu. Unapaswa kungojea mkazo kabla ya kuvuta kambakitovu taratibu. Unapaswa kuweka shinikizo pinzani kwenye fumbatio ya mama. (Soma Kipindi cha 6 tena ikiwa una tashwishi kuhusu jinsi ya kutekeleza mbinu ya kuvuta kambakitovu taratibu.)

  Mwisho wa jibu

11.2 Kuvuja damu baada ya kuzaa kunakohusiana na mikazo

11.3 Kuvuja damu baada ya kuzaa kunakohusiana na jeraha