11.4.3 Hatua za dharura katika na baada ya awamu ya tatu ya leba

Kwa wanawake wasio na hatari zinazojulikana, unaweza kupunguza hatari ya kuvuja damu baada ya kuzaa. Ili kufanya hivyo, dhibiti awamu ya tatu ya leba kwa umakinifu (Kipindi cha 6). Kwa muhtasari, kumbuka vidokezo hivi vikuu:

 • Baada ya mtoto kuzaliwa, hakikisha hakuna mtoto mwingine uterasini. Mpe mama dawa ya misoprostol mikrogramu 600 ya kumeza au 10 (vipimo vya kimataifa) vya oxytocin kwa kuidungia ndani ya misuli. Dawa hizi huisaidia uterasi kujikaza.
 • Usisukume fandasi ili kusaidia kutolewa kwa plasenta.
 • Isugue uterasi punde tu baada ya plasenta kutolewa. Ili kuhakikisha kuwa uterasi imejikaza vyema, isugue kwa angalau kila dakika 15 kwa saa 2 za kwanza baada ya kuzaa. Mfunze mama kupapasa na kuchunguza uterasi yake ili kuiweka dhabiti. Mwambie atafute usaidizi ikiwa uterasi yake ni laini au ikiwa kiwango cha kuvuja damu kitazidi (Mchoro 11.2).
Mchoro 11.2 Isugue uterasi ili kuchochea mikazo ya uterasi baada ya plasenta kutoka.
 • Chunguza kwa umakinifu ili kutambua kama kuna michibuko ya uke, periniamu au kinyeo.
 • Chunguza kwa umakinifu kama plasenta imetoka yote (Kipindi cha 6).
 • Msaidie mama kunyonyesha mtoto punde tu atakapozaliwa. Anza kunyonyesha hata kabla ya plasenta kutoka (Mchoro 11.3). Mtoto akinyonya, mwili wa mama hutolesha oksitosini. Oksitosini huchochea uterasi kujikaza na vichirizi vya maziwa kujikaza ili kutiririsha maziwa kinywani mwa mtoto. Kunyonyesha husaidia kutolewa kwa plasenta na kupunguza kuvuja damu baada ya kuzaa.
Mchoro 11.3 Anza kunyonyesha punde tu mtoto atakapozaliwa ili kupunguza kuvuja damu baada ya kuzaa.
 • Mhimize mwanamke ahakikishe kuwa kibofu chake ni kitupu baada ya kuzaa. Uterasi inaweza kuwa laini kwa sababu kibofu cha mama kimejaa. Mama akikosa kukojoa, chururiza maji vuguvugu juu ya fumbatio lake. Hatua hii isipofaulu, anaweza kuhitaji kuingizwa katheta (neli ya plastiki) kibofuni mwake ili kumsaidia kukojoa.

Ulijifunza kuhusu jinsi ya kutumia katheta katika Kipindi cha 22 cha Moduli ya Utunzaji wa Wakati wa Ujauzito, na katika mafunzo yako ya kiutendaji.

 • Kwa haraka, orodhesha hatua za dharura unazoweza kuchukua kabla, wakati wa na baada ya leba ili kupunguza hatari ya kuvuja damu baada ya kuzaa.

 • Ili kudhibitisha jinsi ulivyojibu, soma tena Vifungu vya 11.4.1, 11.4.2 na 11.4.3.

  Mwisho wa jibu

Hata hivyo, kumbuka kuwa hata ukichukua hatua za dharura zozote zile, kuvuja damu baada ya kuzaa kunaweza kutokea baada ya kuzaa kokote kule. Kila wakati unafaa kuwa tayari kuchukua hatua ya dharura.

11.4.2 Hatua za dharura katika awamu ya pili ya leba

11.5 Udhibiti wa dharura wa kuvuja damu baada ya kuzaa