Utangulizi
Utunzaji katika Ujauzito
Utangulizi wa Moduli ya Utunzaji katika Ujauzito
Shirika la Afya Duniani linakadiria kuwa zaidi ya wanawake 1,500 hufariki kila siku kutokana na matatizo yanayohusiana na ujauzito, na vingi vya vifo hivi hutokea katika nchi zinazostawi. Uwiano wa vifo vya kina mama wajawazito ulimwenguni haujaboreshwa hasa kwa sababu ya idadi kubwa ya vifo katika nchi zinazostawi. (Uwiano wa vifo vya kina mama kutokana na ujauzito ni sehemu ya wanawake wanaofariki kutokana na matatizo katika ujauzito au kuzaa.) Uwiano huu uko chini ya 10 kwa kila watoto 100,000 waliozaliwa wakiwa hai katika nchi zilizostawi na zaidi ya 1,000 kwa kila watoto 100,000 waliozaliwa wakiwa hai katika nchi maskini. Ripoti za Utafiti wa Demografia na Afya chini ya Sahara zinaonyesha kuwa uwiano wa vifo vya kina mama kutokana na ujauzito ulikuwa 871 kwa kila watoto 100,000 waliozaliwa wakiwa hai katika mwaka wa 2000 na 673 kwa kila watoto 100,000 katika mwaka wa 2005 (kalenda ya Uropa). Kwa kifupi, hatari ya kufariki kutokana na ujauzito katika maisha ya mwanamke ni 1 kwa 7,300 katika nchi zilizostawi na 1 kwa 75 katika nchi maskini.
Takriban asilimia 80 ya vifo vya kina mama wajawazito katika nchi zinazostawi vinaweza kuepukika au kutibika. Vifo hivi husababishwa na uavyaji mimba usio salama, kutokwa na damu, eklampsia, maambukizi na leba iliyozuilika (imeelezewa kwa kina katika Moduli hii au itakayofuata). Kuboresha afya ya kina mama ni mojawapo ya Malengo manane ya Milenia ya Maendeleo yaliyopitishwa na jumuiya ya kimataifa katika Mkutano wa Milenia wa Umoja wa Mataifa mwaka wa 2000. Serikali za nchi zilizo kusini mwa Sahara zimejitolea kutimiza Malengo ya Milenia ya Maendeleo, yakiwemo kuboresha afya ya kina mama, kupunguza vifo vya kina mama vitokanavyo na ujauzito kwa asilimia 75 (Lengo la 5 la Milenia la Maendeleo), na kupunguza vifo vya watoto chini ya miaka 5 kwa asilimia 66 (Lengo la 4 la Milenia la Maendeleo.
Uzuiaji wa magonjwa na huduma bora ya kiafya inafaa kuanza kabla ya ujauzito. Utunzaji bora katika ujauzito ni muhimu kwa sababu:
- Huwawezesha wataalamu wa afya kutathmini ikibali ya mama ya kifiziolojia na kisaikolojia.
- Inaweza kuonyesha matatizo ya kiafya yaliyopo na kuzuia baadhi yayo.
- Huwawezesha wanawake na familia zao kujizoesha na kituo hicho cha afya.
- Huwahimiza wanawake kukubali kutembelewa nyumbani na wataalam wa afya.
- Huwaelimisha wanawake kuhusu ishara za hatari za matatizo yanayoweza kuibuka baadaye na kuwasaidia kujiandaa kwa vitendo na kifedha kwa hali za dharura.
Lengo la utunzaji katika ujauzito ni kudumisha afya ya mama na mtoto kwa kumakinikia afya ya mwanamke huyo na fetasi na kuwasaidia katika leba na kuzaa. Jukumu lako la kutoa huduma bora katika ujauzito kwenye kituo cha afya au nyumbani ni kubwa mno. Kwa hivyo, lazima uelewe dhana na utoshelevu wa huduma ya utunzaji katika ujauzito jinsi ilivyopendekezwa katika Moduli hii na jinsi inavyofundishwa katika mpango wa mafunzo ya ujuzi tendaji. Afya na kuongoka kwa wawanawake wajawazito na watoto wachanga katika eneo lako hutegemea dhana na utoshelevu wa huduma hii.
Moduli hii inatoa kanuni za kimsingi na utekelezaji wa utunzaji katika ujauzito kituoni mwa afya na nyumbani. Ina vipindi 22 vilivyogawanywa katika sehemu mbili.
Katika sehemu ya 1, utajifunza kuhusu:
- Uendelezaji na upangaji wa huduma ya utunzaji katika ujauzito.
- Fiziolojia ya mfumo wa viungo vya uzazi wa kike.
- Mabadiliko ya kifiziolojia katika ujauzito.
- Uchunguzi wa mara kwa mara kwa mwanamke mjamzito na fetasi.
- Mbinu za kutathmini ujauzito wa kawaida unavyokua na kutambua matatizo yanayotokea sana.
Katika sehemu ya 2, utajifunza kuhusu:
- Ufafanuzi wa utunzaji bora katika ujauzito.
- Kuwashauri wanawake wajawazito kuhusu kuishi kwa afya, kula vizuri kwa gharama nafuu, na ishara za hatari.
- VVU na kuzuia maambukizi kutoka kwa mama hadi kwa mtoto.
- Leba ya mapema.
- Matatizo ya kihipatensheni ya ujauzito.
- Uavyaji mimba.
- Kuvuja damu mwishoni mwa ujauzito na matatizo mengine yanayotokea sana.
Sehemu ya 2 inahitimisha kwa nadharia mbili kuu za utaratibu tendaji: kuanzisha matibabu ya kudunga sindano ya viowevu kwenye mshipa kabla ya rufaa kwa wanawake walio katika mshtuko, na kuingiza katheta ya kuondoa mkojo kwenye kibofu cha mwanamke mjamzito.