2.4.3 Kuhusisha kila mmoja

Makinikia yale yanayoweza kufanywa na kutimizwa kwa muda uliopo wa hafla hiyo. Usijaribu kutoa habari mpya zote kwa pamoja, kwani watu wanaweza kujihisi wachovu kisha waache kusikiliza.

Kumbuka, mawasiliano ya kutoa na kupokea habari ndiyo njia bora zaidi! Washiriki wanafaa kuhimizwa kushiriki elimu na waliyoyapitia kisha watoe maoni na mapendekezo yao kwa uhuru.

Himiza kushiriki kikamilifu hasa kwa wanawake kwa sababu ndio wanaopaswa kuhimizwa kutumia huduma za utunzaji katika ujauzito. Watu wengine wana uzoefu wa kuzungumza katika vikundi wakati wengine huenda wawe wenye haya au woga. Kwa hivyo, unapaswa kuwahimiza wale wanawake ambao hunyamaza waweze kutoa mawazo yao.

Hakikisha kuwa kila mtu anapata nafasi sawa ya kushiriki. Kwa mfano, ikiwa kikundi cha wanawake fulani kinataka kujifunza kuhusu watakachokula wakati wa ujauzito na baada ya kuzaa, unaweza kuuliza kwanza kila mmoja wao aseme anachokijua. Wanawake wengi tayari wanajua kuhusu lishe bora kutoka vitabuni au madarasani, kwa kuzungumza na wanawake wengine au kutokana na waliyoyapitia. Hata hivyo wanawake wengine wanaweza kuwa wamepotoshwa kwa mfano kuhusu vyakula wanavyofikiri havifai kutumiwa katika ujauzito, angali kwa kweli vyakula hivyo ni bora kwa wanawake wajawazito ikiwa wanaweza kumudu kuvinunua (Picha 2.8).

Picha 2.8 Hafla za elimu ya kiafya zinaweza kufichua maoni mengi tofauti, kwa mfano juu ya lishe bora katika ujauzito.

2.4.4 Kuhitimisha hafla