4.2.2 Awamu ya lutea: siku ya 15 hadi ya 28

Awamu hii ndiyo kipindi cha shughuli ya kopasi luteamu ambapo uterasi huandaliwa kwa ujauzito iwapo utatokea. Baada ya ovulesheni, kopasi luteamu huanza kutoa projesteroni pamoja na kiwango cha chini cha estrojeni. Projesteroni hudumisha uterasi katika hali thabiti inayofaa kwa kupokea na kukistawisha kiinitete. Bitana ya uterasi (endometriamu) hunenepa na kustawishwa na mishipa ya damu kwa wingi na kuwa pokezi sana kwa ova iliyotungishwa. Projesteroni pia husitisha utolewaji zaidi wa Homoni Chochelezi ya Foliko na homoni ya lutea kutoka katika tezi ya pituitari.

Ovulesheni hivyo hufuatwa kwa haraka na ongezeko la kiwango cha projesteroni huku kopasi luteamu ikichukua jukumu la kutoa homoni hii. Projesteroni huenea katika damu mwilini kiwango chake kinapoongezeka. Kiwango cha juu cha homoni hii kinapoifikia hipothalamasi kwenye ubongo, utoaji wa homoni itoayo gonadotropini kutoka kwa hipothalamasi husitishwa.

  • Je, ni nini kitakachofanyika hipothalamasi inapoacha kutoa homoni itoayo gonadotropini? (Tazama mchoro 4.1)

  • Tezi ya pituitari itakoma kutoa Homoni Chochelezi ya Foliko na Homoni ya Lutea.

    Mwisho wa jibu

  • Je, hii itakuwa na athari gani kwa ovari?

  • Upevukaji wa ova zaidi utakomea hapo.

    Mwisho wa jibu

Aina hii ya mfumo dhibiti ambapo kuongezeka kwa kemikali moja ya mwili (kwa muktadha huu projesteroni) husitisha kutolewa kwa kemikali nyingine ya mwili (kwa muktadha huu homoni itoayo gonadotropini) huitwa mwitiko hasi kwa utaratibu wa utendaji. Hata hivyo, kopasi luteamu ina maisha mafupi na kwa hivyo, baada ya kukoma kutoa projesteroni, mwitiko huu hasi kwa hipothalamasi husita na kuiwezesha tena kuanza kutoa homoni itoayo gonadotropini. Hivyo basi mzunguko wa ovari huanza tena.

4.2.1. Awamu ya foliko: siku ya 1 hadi ya 14

4.3 Mzunguko katika uterasi