5.4.1 Mishipa ya damu ya mama na mtoto

Ili kuelewa jinsi damu ya mama na ya mtoto inavyoweza kukaribiana katika plasenta na isichanganyike, ni sharti kwanza ujifunze ukweli wa kimsingi kuhusu damu na mishipa ya damu. Mfumo wa moyo na mishipa unajumuisha moyo, mishipa ya damu, (veni na ateri - tazama Jedwali 5.2), na damu inayozunguka mwilini. Huu ndio mfumo wa uchukuzi unaosambaza oksijeni na virutubishi vilivyofyonzwa kutoka kwa mfumo wa tumbo na utumbo hadi kwenye seli zote, tishu na viungo vyote vya mwili wa mama na wa mtoto anayekua. Oksijeni na virutubishi husaidia mama na mtoto kupata nguvu wanayohitaji kutekeleza majukumu yao. Mfumo huu pia hurudisha dioksidi ya kaboni, ambayo ni mabaki ya pumzi, kwenye mapafu ambapo huondolewa. Utaratibu wa kikemikali unaofanyika mwilini hutolesha taka kwa wingi. Taka hizi husafirishwa kwa damu hadi kwenye figo na ini ambapo huondolewa. Majukumu mengine ya mfumo wa damu na mishipa ni pamoja na kudhibiti kiwangojoto cha mwili na kusafirisha homoni na ajenti zinginezo zinazodhibiti majukumu ya mwili.

Kisanduku 5.2 linaonyesha baadhi ya vidokezo muhimu kuhusu mwingiliano wa mifumo ya moyo na mishipa ya mama na mtoto, na jinsi unavyohusiana na kuzunguka kwa damu katika plasenta.

Kisanduku 5.2 Vidokezo muhimu kuhusu kuzunga kwa damu ya fetasi, mama na plasenta

Damu yenye oksijeni: Damu inayopeleka oksijeni na virutubishi vya kutosha hadi kwenye seli, tishu na ogani za mwili ili kuziwezesha kutekeleza majukumu yake ifaavyo.

Damu isiyo na oksijeni: Ni damu iliyo na kiasi kidogo cha oksijeni na kiasi kikubwa cha taka zilizoyeyuka na dioksidi ya kaboni kuzidi damu yenye oksijeni.

Ateri za kiambakitovu: Kwa kawaida, ateri husafirisha damu yenye oksijeni, lakini ateri zote mbili za kiambakitovu (tazama Mchoro 5.4) huchukua damu isiyo na oksijeni kutoka mwilini mwa fetasi hadi kwenye plasenta. Damu iliyo katika ateri za kiambakitovu husambazwa kwenye plasenta na moyo wa fetasi.

Vena za mama: Vena za mama huchukua damu isiyo na oksijeni kutoka kwenye plasenta. Damu inapopitia kwenye ini na figo, taka zilizoyeyuka hutolewa, ikiwa ni pamoja na zile zilizochukuliwa na vena za endometria kutoka kwenye plasenta. Damu isiyo na oksijeni inapofika katika moyo wa mama husambazwa kwenye pafu zake ili kupata oksijeni zaidi.

Ateri za mama: Ateri za mama husafirisha damu yenye oksijeni ambayo husambazwa na moyo wake mwilini kote. Ateri zake za endometriamu\2 huleta damu kwenye uterasi na kisha kwenye plasenta, huku zikileta damu na virutubishi kutoka kwenye mfumo wa mama wa umeng’enyaji.

Vena ya kiambakitovu: Kwa kawaida, vena husafirisha damu isiyo na oksijeni, lakini vena ya kipekee ya kiambakitovu (tazama Mchoro 5.4) husafirisha damu yenye oksijeni na virutubishi kutoka kwenye plasenta hadi moyo wa fetasi, ambao huisambaza kote katika mwilini mwa fetasi.

Mchoro 5.4 Mzunguko wa damu kwenye fetasi na plasenta. Kumbuka kwamba kuna ateri mbili na vena moja ya kiambakitovu.

5.4.2 Mzunguko wa damu kwenye plasenta