Maswali ya Kujitatmini ya Kipindi cha 5

Jitathmini jinsi ulivyojifunza kwa kujibu maswali haya. Andika majibu yako katika Shajara yako ya Masomo na uyajadili na Mkufunzi wako katika Mkutano Saidizi unaofuata. Unaweza kulinganisha majibu yako na maandishi kuhusu Maswali ya Kujitathmini yaliyo mwishoni mwa moduli hii.

Swali la Kujitathmini 5.1 (linatathmini Malengo ya Somo 5.1, 5.2 na 5.3)

Kati ya maelezo yafuatayo, ni lipi lisilo sahihi? Katika kila kauli, eleza ni kwa nini si sahihi.

  • A.Nguvu zinzosongesha mkia wa mbegu ya kiume hutoka kwenye chembe za kijenetiki zilizo katika kichwa chake.
  • B.Mikazo katika misuli ya pembezoni mwa uterasi na mishipa ya falopio husaidia mbegu za kiume kusongea kuelekea kwenye ova.
  • C.Upandikizaji hutokea blastosisti inapoingia kwenye endomitriamu na kufanikiwa kuumba plasenta ya mwanzo.
  • D.Vena ya kiambakitovu husafirisha damu isiyo na oksijeni kutoka katika fetasi hadi plasenta.
  • E.Plasenta hufanya kazi kama kichungi kwa kuzuia dutu zote hatari kutoka kwa mwili wa mama hadi katika mfumo wa damu ya fetasi.

Answer

A si sahihi. Nguvu za kusongesha mkia wa mbegu za kiume hutoka kwenye mitokondria katika sehemu ya kati ya kichwa na mkia.

B ni sahihi. Mikazo katika misuli ya pembezoni mwa uterasi na mishipa ya falopio husaidia mbegu za kiume kusonga kwa kasi kuelekea kwenye ova.

C ni sahihi. Upandikizaji hutokea blastosisti inapoingia kwenye endomitriamu na kufanikiwa kuumba plasenta ya mwanzo.

D si sahihi. Vena ya kiambakitovu husafirisha damu yenye oksijeni kutoka kwa plasenta kurudi kwenye fetasi. Damu isiyo na oksijeni husafirishwa hadi kwenye plasenta na ateri mbili ya kiambakitovu.

E si sahihi. Plasenta haiwezi kuzuia kuvuka kwa dutu zote hatari kutoka kwa mwili wa mama hadi katika mfumo wa damu ya fetasi. Kwa mfano, pombe, dawa na kemikali zingine zinaweza kuvuka kupitia plasenta.

Mwisho wa jibu.

Swali la Kujitathmini 5.2 (linathmini Malengo ya Somo 5.2)

Soma Mfano 5.1 kisha uyajibu maswali yanayofuata.

Mfano 5.1 Ushauri kwa Bi. A baada ya kufanya ngono bila kinga.

Bi. A alifanya ngono bila kinga (bila kondomu) siku 17 baada ya siku ya kwanza ya hedhi ya mwisho. Amekuja kituoni kubaini kama ametungika mimba.

Mweleze Bi. A uwezekano wake wa kutungika mimba kwa lugha anayoweza kuelewa.

Answer

Bi. A alifanya ngono bila kinga katika siku ya 18 ya muhula wake wa hedhi. Ovulesheni hutokea kwa wanawake wengi karibu siku ya 14, hivyo basi kuna uwezekano kuwa alifanya ngono katika siku tatu hadi nne baada ya ovulesheni. Ova husalia hai kwa saa 12 – 24 isipotungishwa. Kwa hivyo, ikiwa ovulesheni ilitokea kama inavyotarajiwa katika siku ya 14, basi hakuna uwezekano kuwa ova ilikuwa hai siku ya 18 alipofanya ngono. Hivyo basi, hakuna uwezekano kuwa ana mimba kwa wakati huu. Hata hivyo, ikiwa ovulesheni yake ilitokea ikiwa imechelewa, kuna uwezekano ametungika mimba. Mshauri kuhusu hatari za kufanya ngono bila kinga: yaani mimba isiyotakikana na maambukizo ya zinaa.

Mwisho wa jibu

Swali la Kujitathmini 5.3 (linatathmini Malengo ya Somio 5.3)

Soma Mfano 5.2 kuhusu Bi. P, kisha uyajibu maswali yanayofuata.

Mfano 5.2 Bi. P anataka kujua jinsi pombe na miraa inavyoweza kudhuru fetasi yake

Bi P ni mwanamke mjamzito wa umri wa miaka 38 aliye na uraibu wa pombe na kutafuna miraa. Alizuru kituo chako kuhudhuria Kipindi cha elimu ya afya kwa wajawazito kabla ya kuzaa. Alisikiliza ukieleza kuwa damu ya fetasi na ya mama haiguzani moja kwa moja. Baada ya mazungumzo, alikuuliza, “ Kwa nini unaniambia nikomeshe kunywa pombe na kutafuna miraa ikiwa damu yangu haiguzani moja kwa moja na damu ya mtoto wangu? Ikiwa damu yangu haiguzani na ya mtoto, basi pombe na miraa haiwezi kumfikia mtoto.”

Jibu lako ni nini? Mweleze kwa lugha anayoweza kuelewa.

Answer

Unapaswa kumwelezea Bi P kuwa ingawa damu yake haiguzani moja kwa moja na ya mtoto wake, damu yake na ya mtoto imepakana kwa karibu katika plasenta. Ni wembamba wa mishipa ya damu ya mtoto tu unaowagawanya. Kuta hizi za mishipa ni nyembamba sana hivi kwamba vidutu vidogo kama vya pombe na miraa vinaweza kuvukia kutoka damu yake hadi ya mtoto. Mfahamishe kuwa utaratibu huo ndio unaotumika kupitisha dutu muhimu kama oksijeni na virutubishi kutoka kwa damu yake hadi ya mtoto. Hivyo basi, kudumisha afya njema na kula chakula tosha ni muhimu kwa ukuaji wa mtoto. Akikomesha kunywa pombe na kutafuna miraa, mtoto wake atakuwa na afya njema zaidi. Akiendelea kutumia vitu hatari, mtoto anaweza kuzaliwa akiwa na hitilafu au hata afe.

Mwisho wa jibu.

Muhtasari wa Kipindi cha 5