6.1.3 Mifupa ya kinena na simfisisi ya kinena

Mifupa ya kinena katika kila upande huunda sehemu moja ya pelvisi. Mifupa yote miwili ya kinena huungana kwenye simfisisi ya kinena. (Simfisisi ni kiunga imara sana.) Simfisisi ya kinena iko punde chini ya kifusi kilichofunikwa kwa nywele ambacho hukinga sehemu za nje za uke (kama ilivyoonyeshwa kwenye Mchoro 3.2, iwapo utahitaji kukirejelea).

Kuhisi sehemu ya juu ya simfisisi la kinena ni hatua muhimu sana unapolichunguza fumbatio la mwanamke mjamzito. Katika Kipindi cha 10, utajifunza jinsi ya kukadiria urefu wa uterasi kutoka kwenye simfisisi ya kinena hadi kwenye fandasi (sehemu ya juu ya uterasi - tazama Mchoro 3.3 iwapo utahitaji kujikumbusha kuhusu nafasi ya fandasi. Vipimo hivi vitakusaidia kukadiria kipindi cha ujauzito, yaani, idadi ya wiki ambazo ujauzito huu umechukua, na iwapo fetasi hii inakua kwa kiwango cha kawaida.