6.2.1 Ukubwa na umbo la pelvisi

Ukubwa na umbo la pelvisi ni muhimu katika leba na kuzaa. Wanawake wenye nguvu na afya nzuri, waliotumia lishe bora katika kipindi chao cha kukua cha utotoni, kwa kawaida huwa na pelvisi pana iliyoumbika vyema kumpitisha mtoto wakati wa kuzaa. Pelvisi ina ukingo wa duara na nyuti fupi, butu,za iskiamu. (Madaktari na wakunga huliita umbo hili pelvisi ya ‘jinaesidi’.) Sehemu hii hupelekea matatizo machache zaidi wakati wa kuzaa, almuradi fetasi ina ukubwa wa kawaida na njia ya uzazi haina ukuaji wa tishu zisizo za kawaida zinazozuia utaratibu wa kuzaa.

Kuna tofauti kubwa kati ya maumbo mbali mbali ya pelvisi, ambapo baadhi yake husababisha matatizo katika leba na kuzaa. Pelvisi nyembamba inaweza kupelekea ugumu wa mtoto kupitia katika njia ya pelvisi. Ukosefu wa madini muhimu kama iodini katika chakula wakati wa utotoni unaweza kusababisha matatizo ya ukuaji wa pelvisi. Kudumaa (kuwa mfupi kuliko wastani ikilinganishwa na umri) kwa sababu ya lishe bovu na/au magonjwa ya kuambukiza kunaweza pia kupelekea pelvisi nyembamba.

Pili, tutatazama umbo la njia ya pelvisi kwa kina, kisha tutofautishe kati ya kiingilizi cha pelvisi (uwazi mgumu wa umbo la duara ambapo kichwa cha mtoto huingia katika pelvisi - Mchoro 6.3), na kitokezi cha pelvisi (uwazi mgumu wa umbo la duara ambapo kichwa cha mtoto hutokea nje ya pelvisi. Kama utakavyoona katika kifungu kinachofuatia, kiingilizi na kitokezi cha pelvisi hazina usawa wa ukubwa.

6.2.2 Kiingilizi cha pelvisi