6.3.1 Mifupa ya fuvu la fetasi

Mifupa ya fuvu hufunga na kukinga ubongo, ambao ni laini sana na unaweza kupata shinikizo wakati kichwa cha fetasi kinashuka katika njia ya uzazi. Kutanguliza kipenyo cha fuvu la fetasi katika kipenyo kikubwa zaidi cha pelvisi ya mama ni muhimu sana ikiwa ataendelea kuzaa kwa kawaida. Ikiwa kipenyo cha fuvu linalotanguliza ni kipana zaidi ya kile cha pelvisi ya mama, itahitaji uangalifu mkuu sana ili mtoto azaliwe kwa njia ya kawaida ya uke.

Unaweza kutazama mifupa mikuu ya fuvu katika Mchoro 6.5.

Mchoro 6.5 Mifupa ya fuvu la fetasi - kwa mtazamo wa kutoka kushoto.

Mifupa ya fuvu la fetasi ni kama ifuatavyo:

  • Mfupa wa mbele, unaounda paji la uso. Katika fetasi, mfupa wa mbele uko katika nusu mbili, ambazo huungana na kuwa mfupa mmoja baada ya umri wa miaka 8.
  • Mifupa miwili ya parieta, ambayo huwa katika pande zote mbili za fuvu huchukua takriban nafasi yote ya fuvu.

Parieta hutamkwa kama ‘pa-ri-eta’.

  • Mfupa wa oksipitasi, unaounda sehemu ya nyuma ya fuvu na pia sehemu ya msingi wake. Mfupa huu huungana na vetebra ya seviksi (mifupa ya shingo katika safu ya uti wa mgongo, au uti wa mgongo).
  • Mifupa miwili ya panja, mmoja katika kila upande wa kichwa, iliyo karibu zaidi na sikio.

Kuelewa sehemu muhimu na vipimo vya fuvu la fetasi kutakusaidia kutambua tangulizi za kawaida na zisizo za kawaida za fetasi wakati wa uchunguzi wa kabla ya kuzaa, leba na kuzaa.