7.4.2 Kiasi cha damu

Kiasi cha damu (kiasi cha jumla cha damu inayozunguka, kwa kipimo cha lita) huongezeka polepole kwa asilimia 30-50 katika mwanamke mjamzito. Hivyo basi, kufikia hatima ya ujauzito mwanamke huyu atakuwa na takriban lita 1.5 zaidi kuliko wakati hana mimba. Mwili huhitaji kiasi kikubwa cha damu inayozunguka ili kuwepo kwa damu ya ziada itakayopitia katika plasenta ili lishe na oksijeni ifikishwe kwenye fetasi. Ongezeko la kiasi cha damu husababishwa na mabadiliko mawili:

  • Kuongezeka kwa plazma ya damu (kiowevu cha damu).
  • Kuongezeka kwa seli nyekundu za damu katika mzunguko.

Kiwango cha plazma ya damu huongezeka baada ya takriban wiki ya sita ya ujauzito. Kuongezeka kwa damu hufikia kilele chake cha takriban asilimia 50 zaidi kuliko wakati mwanamke hana mimba ifikapo awamu ya pili ya ujauzito ambapo itabaki hivyo hadi hatima ya ujauzito.

Kiasi cha jumla ya seli nyekundu huongezeka kwa takriban asilimia 18 wakati wa ujauzito, kufuatia kuhitajika kwa oksijeni ya ziada katika tishu ya mama, plasenta na fetasi. Seli nyekundu za damu zina dutu inayosafirisha oksijeni, iitwayo hemoglobini, ambayo ina wingi wa elementi muhimu aina ya ayoni (tazama Jedwali 7.1). Matumizi ya dawa yenye elementi ya ayoni wakati wa ujauzito yanaweza kupelekea ongezeko la seli nyekundu za damu hadi asilimia 30 zaidi kuliko wakati mwanamke hana mimba.

Hemoglobini hutamkwa ' hem mo glo bini'

Jedwali 7.1 ayoni, hemoglobini, na anaemia

Ayoni hupatikana katika seli zote na ina kazi nyingi muhimu. Ayoni ni kipengele muhimu sana cha dutu hii inayosafirisha oksijeni yaani hemoglobini, ambayo hupatikana katika seli nyekundu za damu. Ni ayoni hii katika hemoglobini inayofanya seli hizi ziwe nyekundu. Ikiwa lishe lina kiwango cha chini sana cha ayoni, mtu hawezi kuzalisha seli nyekundu za kutosha. Pia, ayoni huhusika katika kuhifadhi na kutoa oksijeni kwenye misuli.

Anemia inafasiliwa kifasaha kuwa ukolezi duni wa hemoglobini katika damu, ingawa mara nyingi hujulikana kama ukolezi duni wa seli nyekundu za damu. Kiasi kidogo cha ayoni katika chakula ndicho kisababishi kikuu cha anemia.

Kipimo cha hemoglobini huonyeshwa kwa kutumia ishara zake za kemikali (Hb) na uzito wake kwa gramu (gm) kwa desilita (dl) moja ya damu. Desilita moja ni sawa na mililita (ml) 10. Shirika la Afya Duniani linapendekeza kuwa hemoglobini ya mwanamke mjamzito haipaswi kuwa chini ya gramu 11 ya hemoglobini kwa desilita moja ya damu (Hb 11g/dl). (Utajifunza mengi kuhusu anemia na matibabu yake katika Kipindi cha 18)

Ingawa kuna ongezeko endelevu katika idadi ya seli nyekundu za damu wakati wa ujauzito, ongezeko la kiasi cha plazma ni kubwa zaidi. Hata ingawa mwanamke mjamzito ana idadi kubwa zaidi ya seli nyekundu za damu kuliko alipokuwa bila mimba, seli hizi huzimuliwa katika kiasi cha plazma ya damu ambacho kwa sasa ni kikubwa.

  • Je, uzimulizi huu huathiri vipi ukolezi wa seli nyekundu na hemoglobini katika damu ya mwanamke mjamzito ikilinganishwa na wakati akiwa hana mimba?

  • Ukolezi wa seli nyekundu za damu na hemoglobini hushuka kwa sababu vipengele hivi huwa vimezimuliwa zaidi, hivyo basi damu ya mwanamke huyu itakuwa na kiwango kidogo cha hali ya anemia.

    Mwisho wa jibu

Athari hii hujulikana kama anemia ya kifiziolojia. Hivyo basi, tukio hili hueleza umuhimu wa chembechembe za ayoni kwenye chakula au kutokana na tembe wakati wa ujauzito.

7.4.3 Shinikizo la damu katika ujauzito