7.4.3 Shinikizo la damu katika ujauzito

Awali tulijadili kuwa projesteroni husababisha ligamenti na jointi kulegea wakati wa ujauzito. Vile vile, homoni hii pamoja na kemikali zingine asilia mwilini husababisha pembezo za mishipa ya damu kulegea kidogo. Malengo yake ni kuwa mzunguko wa damu mwilini utafanyika bila kuzuiliwa sana, kwa sababu kiasi kile kile cha damu kinazunguka kupitia mishipa pana kiasi. Shinikizo la damu (SD) humaanisha jinsi ambavyo damu 'husukuma' pembezo za mishipa mikuu ya damu inapozunguka mwilini inapopigwa na moyo.

  • Ulegevu kiasi wa pembezo za mishipa ya damu unaathiri vipi shinikizo la damu la mwanamke mjamzito?

  • Shinikizo la damu la mwanamke huyu liko chini kuliko hali yake kabla ya kupata mimba, kwa sababu kiasi chicho hicho cha damu kina nafasi kubwa zaidi ya kuzungukia.

    Mwisho wa jibu

Shinikizo la chini la damu ni kawaida hususan katika kipindi cha mwanzo wa ujauzito. Wanawake wengi hukumbwa na kizunguzungu mara kwa mara katika kipindi cha kwanza cha ujauzito, kwa sababu kiwango kidogo cha damu na oksijeni hufikishwa kwenye ubongo. Projesteroni pia inaweza kusababisha ulegevu mkuu wa ghafla katika mishipa ya damu, hivyo kusababisha hisia za kizunguzungu za ghafla au hata kupoteza fahamu kwa muda mfupi.

Kisababishi kingine cha kizunguzungu kinaweza kuletwa na kulala chali. Jambo hili hufanyika mara nyingi baada ya wiki 24 ya ujauzito, lakini linaweza kutokea mapema kwa mwanamke aliyebeba mapacha au hali zozote zinazoongeza wingi wa kiowevu cha amniotiki (maji yanayozingira fetasi) Mwanamke mjamzito anapolala chali, uzito wa uterasi na vyote vilivyomo hufinya mishipa mikuu ya damu (vena kava) inayotoka upande wa chini wa mwili wake kuelekea moyoni. Mishipa ya damu inapojibana, uwezekano wa damu kusambaa nyuma hadi moyoni hupunguzwa, tukio ambalo litasababisha mkondo wa damu nje ya moyo hadi sehemu mbalimbali za mwili kupunguka.

  • Ikiwa kuna upungufu wa ghafla wa damu inayotoka moyoni, ni nini kitakachofanyikia shinikizo la damu la mwanamke, na je, atahisi vipi kufuatia tukio hili?

  • Kulala chali kunaweza kusababisha shinikizo la damu kushuka kighafla. Kizunguzungu au kupoteza fahamu kunaweza kutokea kwa sababu hakuna oksijeni ya kutosha inayofikia ubongo. Baada ya kukamilisha trimesta ya kwanza, wanawake wajawazito wanapendekezwa wasilale chali.

    Mwisho wa jibu

7.4.2 Kiasi cha damu

7.4.4 Mazoezi na mtiririko wa damu wakati wa ujauzito