8.2.1 Dalili zinazoweza kuashiria ujauzito

Dalili zinazoweza kuashiria ujauzito zinazoripotiwa sana na wanawake mwanzoni mwa ujauzito pia huitwa ‘ishara za kukisiwa’ kwa sababu mara nyingi ujauzito ‘hukisiwa’ na mhudumu wa afya kwa msingi wa ripoti hizi za dhahania. Lakini ni muhimu kukumbuka kuwa hizi ni ishara zinazoweza tu kuashiria ujauzito.

Kukosa kipindi cha hedhi (amenorea)

Kukosa kipindi cha hedhi mara nyingi huwa ndiyo dalili ya kwanza ambayo wanawake hutambua wanapokuwa wajawazito. Ikiwa mwanamke atakuambia kuwa amekosa kipindi cha hedhi (amenorea) au alikoma kupata hedhi kwa miezi kadhaa, hii ni ishara nzuri ya ushikaji mimba kwa wanawake ambao huwa na mzunguko wa hedhi wa kawaida. Visababishi vingine vya amenorea vinaweza kuwa lishe duni, matatizo ya kihisia, au ukomohedhi (mabadiliko katika maisha) kwa wanawake wakongwe.

Mabadiliko kwa matiti

Wanawake wajawazito wanaweza kuripoti kuhisi matiti kuwa laini, yaliyojaa, yanayonywea, utanukaji na areola (tishu nyeusi ya mviringo inayozunguka chuchu) kuwa nyeusi. Mwanzoni mwa ujauzito tezi za areola hutanuka kutokana na uchochelezi wa homoni na ukubwa wa matiti huongezeka polepole kujitayarisha kutengeneza maziwa ya mtoto. Lakini kumbuka kuwa ukubwa wa matiti mara nyingi huongezeka muda tu kabla ya kipindi cha hedhi cha kila mwezi kwa wanawake wasio wajamzito.

Kichefuchefu na kutapika

Dalili hii inayotokea sana hutokea katika takriban asimilia 50 ya ujauzito katika miezi mitatu ya kwanza. Huwa kali zaidi asubuhi na ndiyo sababu iliyopelekea hisia hii kuitwa maradhi ya asubuhi. Lakini inaweza kutokea wakati wowote na inaweza kuchochewa na harufu za upishi na za viungo vya upishi. Wanawake wengine wajawazito huhisi kichefuchefu siku nzima. Visababishi vingine vya dalili hii vinaweza kuwa maradhi au vimelea. Kutapika sana mara kwa mara ni dalili ya hatari kwa sababu mwanamke huyo anaweza kupoteza uzani kwa haraka. Utajifunza mengi kuhusu haya katika Kipindi cha 12.

Uchovu

Mwanzoni mwa ujauzito wanawake wanaweza kuripoti kujihisi wachovu na wenye usingizi wakati wa mchana na kutaka kupumzika mara kwa mara kuliko kawaida wanapofanya kazi zao. Visababishi vingine vinaweza kuwa anemia (tazama Kisanduku 8.1), lishwe duni, matatizo ya kihisia, au kazi nyingi za sulubu.

Kisanduku 8.1 Anemia

Anemia ni ugonjwa wa damu ambao unaweza kumfanya mtu ajihisi mchovu kila wakati. Damu huwa na chembe nyekundu ambazo hubeba oksijeni kuzunguka mwili, zikipeleka kwa misuli na ogani ambapo hutumika kutengeneza nguvu. Mtu aliye na anemia hana chembe nyekundu za damu za kutosha na kwa hivyo mwili wake hupungukiwa na oksijeni na hauwezi kutengeneza nguvu za kutosha kufanya kazi ya kawaida. Kuna visababishi kadhaa vya anemia lakini kile kinachojulikana sana ni ukosefu wa ayoni kwenye mlo. Ayoni huhitajika kutengeneza upya chembe nyekundu za damu. Anemia husababisha matatizo katika ujauzito na kuzaa lakini inaweza kuzuiliwa kwa kula vyakula vya kutosha vilivyo na protini na ayoni. Wanawake wajawazito huhitaji ayoni nyingi na kwa hivyo kidesturi hupewa tembe za ayoni. Utajifunza kuhusu lishe na ujauzito katika Kipindi cha 14. Utambuzi na matibabu ya anemia vimeelezewa katika Kipindi cha 18.

Kukojoa mara kwa mara

Wanawake wajawazito mara nyingi huripoti kuwa wao huhitaji kukojoa mara kwa mara, hasa katika miezi mitatu ya kwanza na mwezi mmoja au miwili ya mwisho wa ujauzito. Visababishi vingine vya dalili hii vinaweza kuwa mfadhaiko, maambukizi ya kibofu au kisukari (ugonjwa wa sukari kwa damu). Utajifunza kuhusu utambuzi wa kisukari katika Kipindi cha 9 na maambukizi ya kibofu katika Kipindi cha 18.

Ishara za kwanza za uhai wa mtoto zinazohisiwa na mama

Wanawake wengi wajawazito huanza kuhisi mtoto wao akisonga kwa mwendo mwepesi ndani yao kabla ya kutimiza nusu ya muda wa ujauzito. Hisia hii hujulikana kama mtoto kutoa ishara za kwanza za uhai. Wanawake ambao wamepata mtoto hapo awali huwa makini kwa mienendo hii midogo mapema kuliko wanawake walio wajawazito kwa mara ya kwanza. Kutambulika kwa kwanza kwa mienendo hii ya fetasi kwa kawaida hutokea katika juma la 18-20 la ujauzito kwa primigravida (wanawake wenye ujauzito wa kwanza) lakini inaweza kuwa mapema kama juma la 14-16 kwa maltigravida (wanawake waliowahi kuwa na ujauzito hapo awali). Kisababishi kingine cha dalili hii kinaweza kuwa gesi kwenye tumbo.

Kloasma (au ‘barakoa ya ujauzito’)

Weusi wa ngozi kwenye paji la uso, sehemu juu ya pua, au vitefute huitwa kloasma. Hupatikana sana kwa wanawake weusi (Mchoro 8.2). Madoadoa meusi yanaweza kutokea kwa titi na tumbo, hasa kwenye mstari wa kati chini ya kitovu. Kwa kawaida dalili za kloasma hutokea baada ya majuma 16 ya ujauzito (ujauzito wa miezi minne) na huongezeka kwa kuwepo kwa mwanga wa jua. Hata hivyo, mabadiliko haya ya ngozi si viashiria vya kuegemewa vya ujauzito.

Mchoro 8.2 Kloasma inaweza kuashiria ujauzito lakini pia inaweza kuwa ni athari ya mwanga wa jua.
  • Je, unaweza kuamua kuwa mwanamke ni mjamzito awapo na dalili zote zilizo hapo juu?

  • Hauwezi kuwa na uhakika kuwa ana ujauzito kwa sababu mabadiliko mengine ya mwili ya kawaida au matatizo ya afya hujitokeza sawa na dalili hizi zinazoweza kuashiria ujauzito.

    Mwisho wa jibu

8.2 Kutambua iwapo mwanamke ni mjamzito

8.2.2 Dalili na ishara zinazoelekea kuashiria ujauzito