8.2.3 Dalili chanya za ujauzito

Utambuzi chanya wa ujauzito unaweza kufanywa kwa msingi wa dalili hizi ambazo wakati mwingine huitwa dalili ‘hakika’. Kamwe haziwezi kutambulika hadi baada ya miezi mitatu ya kwanza ya ujauzito.

Mipigo ya moyo wa fetasi

Mchoro 8.3 fetoskopu ya sikio moja

Kiwango cha kawaida cha mpigo wa moyo wa fetasi ni mipigo 120-160 kwa dakika. Mpigo wa moyo unaweza kugunduliwa baada ya majuma 18-20 ya ujauzito kwa kuweka fetoskopu (Picha 8.3) kwenye fumbatio la mama na kusikiza. Utajifunza jinsi ya kufanya hivi katika Kipindi cha 11 na masomo yako ya ujuzi tendaji. Wakati mwingine hospitali huwa na mashine inayoitwa Doppler ya kushika kwa mkono inayoweza kutambua mpigo wa moyo wa fetasi mapema hata kama baada ya majuma kumi ya ujauzito.

Utomasaji wa fetasi

Unapaswa kuweza kuhisi (kutomasa kwa mikono yako) fetasi ikisonga kupitia kuta za fumbatio la mama, ujauzito ukiwa na takriban majuma 18, na baada ya majuma 22, umbo la mtoto linaweza kuhisika. Utajifunza jinsi ya kufanya hivi katika Vikao vya 10 na 11 vya Somo na katika masomo yako ya ujuzi tendaji.

Uchunguzi wa kutumia mawimbisauti

Uchunguzi wa kutumia mawimbisauti (au uchunguzivijisauti) ni mojawapo ya visaidizi bora sana vya kiufundi katika kutambua na kufuatilia ujauzito, hata hivyo, unaweza kufanywa tu katika kituo cha afya kwa kutumia vifaa mwafaka. Mawimbi makali sana ya sauti usiyoweza kuyasikia hupitishwa kwenye fumbatio la mama kwa mashine hiyo na kurushwa kurudi nyuma mbali na mtoto. Tarakilishi hugeuza mawimbi haya ya sauti kuwa picha ya umbo la fetasi; plasenta na kiungamwana pia zinaweza kuonekana. Hali njema ya fetasi inaweza kufuatiliwa kwa kutumia vijisauti ujauzito unapoendelea.

  • Je, ni zipi kati ya ishara na dalili za ujauzito zilizo katika Sehemu 8.2.1 hadi 8.2.3 unazoweza kutumia katika kebele yako kukusaidia kutambua ujauzito katika jamii?

  • Unaweza kutegemeza utambuzi wako kwa mchanganyiko wa dalili zinazoweza kuashiria ujauzito ambazo wanawake wanakueleza (amenorea, mabadiliko ya matiti, kichefuchefu na kutapika, hasa magonjwa ya asubuhi, kukojoa mara kwa mara, uchovu wakati wa mchana, ishara za kwanza za uhai wa fetasi, na kloasma); na ishara na dalili zinazoelekea kuashiria ujauzito za kutanuka kwa fumbatio na mwanamke kuwa na minyweo ya uterasi isiyo na maumivu. Ishara chanya unazoweza kutambua katika kiwango cha jamii majuma 18-22 baada ya utungisho ni kusikiza mpigo wa moyo wa fetasi kwa fetoskopu na kutomasa fetasi kupitia ukuta wa fumbatio la mama.

    Mwisho wa jibu

Zoezi 8.1 Kuuliza maswali kuhusu ishara zinazoweza kuashiria ujauzito

Tenga takriban dakika 10 kwa zoezi hili.

Andika katika Shajara yako ya Masomo maswali ambayo ungemwuliza mwanamke ikiwa unajaribu kujua iwapo huenda awe na ujauzito. Kumbuka kutumia lugha ya heshima na maneno anayoweza kuelewa.

Jadili maswali yako na Mkufunzi wako katika Mkutanao saidizi wa Masomo utakaofuata.

Zoezi hili linahusiana na Swali la Kujitathmini 8.5 mwishoni mwa Kipindi hiki.

8.2.2 Dalili na ishara zinazoelekea kuashiria ujauzito

8.3 Kutambua mambo yanayoweza kusababisha hatari katika ujauzito