8.3.5 Je, amewahi kupata matatizo yoyote ya kuzaa au ujauzito wa awali?

Ikiwa mwanamke amekuwa akipata matatizo ya kuzaa au ujauzito hapo awali, anaweza kupata matatizo hayo tena. Mwambie mama akuhadithie kuhusu kuzaa na ujauzito wa awali. Mhimize akueleze kila kitu: mazuri na mabaya. Kisha uliza maswali haya ili kujua zaidi kuhusu matatizo ya awali katika ujauzito na jinsi ya kujitayarisha kwa ujauzito huu. Nakili utakayojifunza. Matatizo haya yote yameelezewa kwa kina katika vikao vingine vya somo katika Moduli hii.

Je, alikuwa mchovu, mdhaifu au mwenye anemia?

Kuchoka sana au udhaifu katika ujauzito kwa kawaida husababishwa na anemia (tazama Jedwali 8.1). Ikiwa alikuwa na anemia katika ujauzito wa awali, kuna uwezekano wa kupata tena wakati huu.

Je, alikuwa na shinikizo la juu la damu, kuvimba au matukutiko?

Ikiwa alikuwa na shinikizo la juu la damu katika ujauzito wa hapo awali, kuna uwezekano wa kupata tena. Shinikizo la juu la damu linaweza kuwa dalili ya priklampsia (tazama Jedwali 8.2). Chunguza shinikizo la damu na dalili zingine za priklampsia mara kwa mara na ujitayarishe kumpa rufaa kwenda hospitalini.

Ikiwa alikuwa na matukutiko katika kuzaa au ujauzito wa hapo awali, huenda alikuwa na eklampsia (Jedwali 8.2) na ni dhahiri kuwa anafaa kuzalia hospitalini.

Je, alikuwa na kisukari melitasi?

Ikiwa alikuwa na kisukari melitasi (sukari nyingi sana kwenye damu) katika ujauzito wa awali, kuna uwezekano wa kuupata tena. Kiwango cha sukari kinapokuwa juu sana kwenye damu, kiasi fulani huingia kwenye mkojo damu inapochujwa kwenye figo. Unafaa kupima mkojo wa mwanamke mjamzito ili kubaini iwapo kuna sukari. (Tutakufunza jinsi ya kufanya haya kwenye Kipindi cha 9). Kipimo cha kutegemewa kinaweza kufanywa katika kituo cha afya. Kisukari melitasi kinaweza kuwa kisababishi cha kuharibika kwa ujauzito au matatizo mengine kwa mama au mtoto baada ya kuzaa.

Je, alikuwa na leba iliyokaa muda mrefu sana au awamu ndefu ya kusukuma mtoto?

Je, leba yake ilichukua zaidi ya saa 24 kwa mtoto wa kwanza au zaidi ya saa 12 kwa watoto wengine? Je, alisukuma mtoto kwa zaidi ya saa mbili? Je, mtoto alikuwa katika nafasi yenye ugumu au alikuwa mkubwa sana? Je, alikuwa na woga mwingi? Uliza ikiwa hiyo leba yake iliyokaa kwa muda mrefu ilisababisha matatizo kwake au mtoto wake. Ikiwa uzazi ulikuwa salama kwa mama na mtoto, basi huenda asiwe na tatizo katika kuzaa. Ikiwa kulikuwa na ugumu wa kuzaa, uliza ikiwa anajua kisababishi cha leba kuchukua muda mwingi. Je, alikuwa na anemia?

Je, alikuwa na fistula?

Je, ikiwa alipata leba kwa muda mrefu, ilisababisha fistula (mwanya usio wa kawaida, baina ya uke na labda kibofu cha mkojo, rektamu, urethra au ureta)? Kuna uwezekano wa hili kutokea kwa wanawake waliopitia desturi inayodhuru ya ukeketaji walipokuwa watoto. Mkojo au kinyesi hupita kwenye fistula hadi kwenye uke na kuvuja kwa mfululizo, isipokuwa fistula izibwe kwa njia ya upasuaji.

Historia ya fistula hapo awali inamaanisha ni dhahiri kuwa anapaswa kuzalia hospitalini.

Je, alipata uchungu wa kuzaa (leba) kwa muda mfupi sana (chini ya saa 3)?

Ikiwa mama alipata leba ya muda mfupi sana hapo awali, hakikisha yeye pamoja na familia yake wanajua la kufanya iwapo utachelewa kumfikia na hawawezi kumpeleka katika kituo cha afya. Unaweza kuifunza familia jinsi ya kuzalisha mtoto kwa hali ya dharura. Utajifunza jinsi ya kufanya haya kwenye Moduli inayofuata ya Utunzaji katika Leba na Kuzaa.

Je, alizaa mapema kabla ya muda?

Ikiwa alipata mtoto aliyezaliwa mapema kwa mwezi mmoja, chunguza ikiwa mchozo ulitoka ukeni mwake. Hii inaweza kuwa dalili ya maambukizi kwenye uke ambayo yanaweza kusababisha kuzaa kabla ya muda kamili wa ujauzito kukamilika. Kuwa tayari ikiwa mtoto atawasili kabla ya muda na umakinikie dalili za leba zilizoelezewa kwenye moduli inayofuata ya Utunzaji katika Leba na Kuzaa.

Je, alipata mtoto mdogo (chini ya kilo 2.5 au pauni 5)?

Chunguza ikiwa mtoto alizaliwa mapema (ni kawaida kwa watoto wanaozaliwa mapema kuwa na uzani wa chini). Ikiwa mtoto alikuwa mdogo lakini alizaliwa kwa wakati unaofaa, chunguza ikiwa mama alikuwa na anemia ( Jedwali 8.1), shinikizo la juu la damu au priklampsia (Jedwali 8.2). Chunguza pia ikiwa alipata chakula cha kutosha, ikiwa alivuta sigara au kutumia madawa. Moja ya mambo haya huenda lilisababisha mtoto huyo kuwa na uzani wa chini.

Chunguza ukubwa wa fumbatio lake ili kuona ikiwa mtoto anakua kikawaida. (Utajifunza jinsi ya kufanya haya kwenye Kipindi cha 11). Ukifikiri kuwa huenda mtoto huyu ana uzani wa chini ikilinganishwa na umri wa ujauzito, mama anastahili kuzalia hospitalini kwa sababu watoto wadogo wanaweza kupata matatizo mengi ya kiafya kuliko walio na uzani wa kawaida. (Moduli ya Utunzaji wa baada ya kuzaa itaelezea sababu na jinsi ya kutoa usaidizi).

Je, alipata mtoto mkubwa (zaidi ya kilo 4 au pauni 9)?

Chunguza ikiwa alikuwa na matatizo wakati wa kuzaa. Iwapo hakupata, labda uzazi huu utakuwa salama pia. Lakini, kuwa na mtoto mkubwa kunaweza kuashiria kuwa mama anaugua kisukari melitasi. Chunguza kwa makini uone ikiwa mtoto huyu anaonekana kuwa mkubwa pia. Pima sukari kwenye mkojo wa mama na ikiwezekana aweze kupimwa kisukari melitasi kwenye kituo cha afya.

  • Je, unaweza kueleza ni kwa nini mtoto anaweza kuwa mkubwa iwapo mama ana kisukari?

  • Hapo awali tulisema kuwa mama kuugua kisukari melitasi husababisha ongezeko la sukari kwenye damu. Mtoto hulishwa virutubishi kutoka kwa damu ya mama na kwa hivyo anapata sukari nyingi na huenda akanenepa.

    Mwisho wa jibu.

Je, alivuja damu nyingi kabla au baada ya kuzaa?

Ikiwa alivuja damu nyingi hapo awali kabla au baada ya kuzaa, kuna uwezekano wa kutokea tena. Mhimize akueleze yote anayokumbuka kuhusu kuvuja huko kwa damu. Je, alihitaji usaidizi wa kiafya? Je, alipata anemia baadaye? Je, alikuwa mdhaifu hadi kushindwa kusimama? Majibu ya haya maswali yatakusaidia kujitayarisha kwa yanayoweza kutokea wakati huu. Kuwa tayari kumtibu ikiwa atavuja damu sana baada ya kuzaa. Utajifunza jinsi ya kufanya haya katika Moduli ya Utunzaji katika leba na kuzaa.

Ikiwezekana, mwanamke aliyevuja damu hapo awali anafaa kuzalia hospitalini.

Je, alikuwa na matatizo ya plasenta (baada ya kuzaa)?

Itakuwa vyema ikiwa mwanamke ambaye plasenta yake ilisalia ndani baada ya kuzaa hapo awali atazalia kwenye hospitali ujauzito utakaofuata.

Ikiwa plasenta ya mwanamke huyo haikutoka kwa urahisi hapo awali, tatizo hilo linaweza kutokea tena. Mwambie amakinikie dalili za kuvuja damu katika ujauzito huu na kutafuta usaidizi mara moja kutoka kwa mtaalam wa afya haya yakitokea.

Je, alikuwa na joto jingi mwilini au maambukizi kwenye uke au uterasi?

Kuzaa huku kunaweza kuwa sawa. Lakini ikiwa alikuwa na maambukizi kwenye uke au uterasi katika au baada ya kuzaa hapo awali, kuna hatari ya maambukizi tena wakati huu. Kuwa tayari kuchunguza dalili za maambukizi ya uke. (Kipindi cha 9 kitakufundisha jinsi ya kufanya haya).

Je, alihuzunika (alipata dipresheni) baada ya kuzaa?

Dipresheni ya baada ya kuzaa ni tatizo kubwa sana la kiafya. Kwa hivyo, ni lazima apewe rufaa aende katika kituo cha afya cha kiwango kinachofuata.

Ikiwa mwanamke huyo alipata dipresheni hapo awali baada ya kuzaa, inaweza kutokea tena. Kuwa tayari kutoa usaidizi haya yakitendeka. (Ushauri umeangaziwa katika Kipindi cha 14.)

Je, mtoto aliugua au kufariki kabla, katika na baada ya kuzaliwa?

Ukidhani kuwa kutakuwa na hatari kwa mtoto wake atakayefuata, mpe rufaa aende katika kituo cha afya kilicho karibu.

Chunguza visababishi vya mtoto huyu kuugua au kufariki. Je, wataalam wa afya walimwambia kisababishi iwapo alihudumiwa nao? Je, anayo maoni yake kuhusu yaliyotendeka?

Je, mtoto wake alikuwa na kasoro za kuzaliwa?

Kasoro zingine za kuzaliwa hutokea tu na hakuna anayejua sababu. Zingine ni za kifamilia (za kurithiwa). Uliza kuhusu aina ya kasoro na ikiwa kuna mtu yeyote kwenye familia ya mama au ya babake mtoto aliye na kasoro hiyo ya kuzaliwa. Huenda mtoto anayefuata akawa na matatizo hayo hayo. Kasoro zingine husababishwa na maradhi kama vile hepesi au rubela. Ikiwa mwanamke alikuwa na hepesi au rubela katika ujauzito wa awali, mhakikishie kuwa huenda maambukizi haya yasisababishe kasoro za kuzaliwa katika ujauzito huu. Wanawake wajawazito wanapaswa kujaribu wasitangamane na watu wagonjwa. Visababishi vingine vya kasoro za kuzaliwa ni kutangamana na kemikali zenye sumu, madawa au dawa, au zinaweza pia kutokana na lishe duni katika ujauzito. Ulaji wa lishe bora katika ujauzito umeangaziwa katika Kipindi cha 14.

Je, alifanyiwa upasuaji (kuzaa kwa njia ya upasuaji)?

Katika upasuaji wa kuzaa, daktari hukata na kufungua fumbatio na uterasi ya mwanamke ili kumtoa mtoto. Wakati mwingine upasuaji hufanywa kwa sababu mtoto hatoshei kwenye pelvisi ya mama. Vile vile, wakati mwingine hufanywa kwa sababu mtoto yumo hatarini na ni lazima azaliwe kwa haraka. Baada ya mtoto kutoka, daktari hushona uterasi na kufunga fumbatio. Kovu hubaki kwenye uterasi na la pili kwenye fumbatio (Mchoro 8.5).

Ni salama kabisa kwa mwanamke aliyefanyiwa upasuaji awali kuzalia hospitalini tena katika ujauzito utakaofuata.

Mchoro 8.5 Upasuaji wa kuzaa huacha kovu moja kwenye fumbatio (kushoto) na kovu jingine kwenye uterasi (kulia).

Wanawake wengi wanaweza kuzaa kwa njia ya kawaida kupitia ukeni hata ikiwa walizaa kwa njia ya upasuaji hapo awali. Lakini, kuna uwezekano mdogo kuwa kovu lililo kwenye uterasi linaweza kupasuka wakati wa leba. Haya yakitokea, mwanamke pamoja na mtoto wake wanaweza kufariki kutokana na mama kuvuja damu ndani ya mwili.

8.3.4 Je, amewahi kutoa mimba?

8.3.6 Je, anayo matatizo mengine yoyote ya kiafya?