Maswali ya kujitathmini ya Kipindi cha 8

Kwa kuwa umekamilisha Kipindi hiki, unaweza kutathmini jinsi ulivyofanikisha malengo ya mafunzo kwa kujibu maswali yanayofuata utafiti kifani 8.1. Andika majibu yako kwenye shajara yako ya masomo na ujadiliane na mkufunzi wako katika Kipindi saidizi cha masomo kitakachofuata. Unaweza kulinganisha majibu yako na muhtasari juu ya maswali ya kujitathmini mwishoni mwa moduli hii.

Utafiti kifani 8.1 Je, Bi X ni mjamzito?

Bi X ana umri wa miaka 39 na ameishi katika ndoa kwa miaka 15. Amejaliwa mtoto ambaye alizaliwa miaka kumi iliyopita na ana matumaini kuwa yeye ni mjamzito tena. Bi X anasema kuwa yeye na mumewe hawajatumia uzuiaji mimba na hafikirii kuwa ujauzito wake umewahi kuharibika kwa wakati huo. Hajapata hedhi kwa majuma tisa yaliyopita. Unapomhoji kuhusu mabadiliko kwenye mwili wake tangu hedhi ya mwisho, anasema kuwa hajagundua chochote, lakini amekuwa akihisi uchefuchefu anapoamka asubuhi na yeye huwa na uchovu mwingi sana. Bi X anakuambia kuwa mtoto wake wa kwanza alizaliwa baada ya leba ya saa 30 na alikuwa na uzani wa kilo 4. Pia anakumbuka kuwa alipewa tembe za ayoni lakini hajui sababu.

Maswali ya kujitathmini 8.1 (yanatathmini Malengo ya Somo 8.1, 8.2 na 8.4)

 • a.Je, ni nini kibaya na kumwuliza Bi X ikiwa alipata priklampsia katika ujauzito uliopita?
 • b.Je, kumwuliza swali kwa kutumia maneno hayo kunawezaje kuharibu uaminifu wake kwako?
 • c.Andika swali hili tena ili kuepuka kusababisha matatizo uliyotambua.

Answer

 • a.Mtu ambaye si mtaalam wa afya hawezi kuelewa maana ya priklampsia. Kwa hivyo, hawezi kuelewa swali hilo. Anaweza kusema ‘la’ kwa sababu hataki ufikiri kuwa hajui. Unaweza kukosa kujua habari muhimu kuhusu visababishi vya hatari ikiwa maswali yako hayaeleweki.
 • b.Anaweza kuwa na wasiwasi kuwa unaweza kufikiria yeye ni mjinga kwa sababu hajui neno hili la kitiba.
 • c.Hatujui jinsi ulivyoandika tena swali hilo (kuna njia nyingi bora za kulisema) lakini huenda ulitumia maneno kama;

‘Je, katika ujauzito uliopita, mtaalam wa afya aliwahi kukuambia kuwa una shinikizo la juu la damu au kuwa una protini kwenye mkojo? Je, uliwahi kupitia maumivu makali ya kichwa, kichefuchefu au kutapika na kuvimba nyayo, mikono au uso?’

Mwisho wa jibu

Maswali ya kujitathmini 8.2 (yanatathmini Malengo ya Somo la 8.3)

 • a.Je, ni dalili zipi zinazoweza kuashiria ujauzito zilizo katika utafiti kifani wa Bi X?
 • b.Je, kuna lolote katika historia yake linaloashiria kuwa huenda hana ujauzito?
 • c.Je, angewezaje kujua kwa haraka iwapo huenda ana ujauzito?

Answer

 • a.Bi X anaripoti dalili tatu zinazoweza kuashiria ujauzito: amenorea (kukosa hedhi kwa majuma tisa); kichefuchefu asubuhi na uchovu usio wa kawaida wakati wa mchana.
 • b.Ametaka mtoto mwingine kwa miaka kumi iliyopita lakini hata kwa kutotumia uzuiaji mimba, bado hajashika mimba, na kwa hivyo huenda asiwe na ujauzito.
 • c.Njia ya haraka ya kujua iwapo ana ujauzito inaweza kuwa kuenda katika kituo cha afya kilicho karibu ambapo wanaweza kupima ujauzito kwa kutumia mkojo wake kuchunguza ikiwa una homoni ya korioni ya gonadotropini ya binadamu, ambayo hutolewa na kiinitete na plasenta. Kipimo hiki si ushahidi wa mwisho, bali kinaweza kuashiria ujauzito.

Mwisho wa jibu.

Maswali ya kujitathmini 8.3 (yanatathmini Malengo ya Somo 8.5)

Je, kuna lolote kwenye historia ya Bi X linaloonyesha kuwa anafaa kushauriwa kuzalia kwenye kituo cha afya wakati huu ikiwa ujauzito wake utadhibitishwa? Eleza ni kwa nini ndivyo au sivyo.

Answer

Ikiwa Bi X ni mjamzito, anafaa kushauriwa kuzalia kwenye kituo cha afya wakati huu kwa sababu ya umri wake (ni mama mkongwe kidogo wa miaka 39), alikuwa na leba kwa muda mrefu (zaidi ya saa 24), na mtoto wake wa kwanza alikuwa mkubwa (kilo 4). Visababishi vyote vitatu vya hatari vinaonyesha kuwa huenda akawa na ugumu katika kuzaa mtoto wake wa pili.

Mwisho wa jibu

Swali la kujitathmini 8.4 (linatathmini Malengo ya Somo 8.1 na 8.5)

Eleza ni kwa nini Bi X alipewa tembe za ayoni katika ujauzito wa hapo awali. Je, hii ni ishara kuwa alikuwa na kisababishi kikali cha hatari wakati huo?

Answer

Bi X alipewa tembe za ayoni katika ujauzito wake wa kwanza kama utaratibu wa kumkinga dhidi ya kupata anemia (upungufu wa seli nyekundu za damu). Ayoni huongeza usambazaji wa seli nyekundu za damu ambazo hubeba oksijeni kwenye mwili wake na ule wa mtoto anayekua. Wanawake wote wajawazito wanafaa kupewa tembe za ayoni. Kwa hivyo hiki si kisababishi cha hatari kwa Bi X.

Mwisho wa jibu

Swali la Kujitathmini 8.5 (linatathmini Malengo ya Somo la 8.4)

Je, ni maswali yapi uliyoandika katika Shajara yako ya Masomo ulipokamilisha zoezi 8.1? Je, ulitumia lugha ambayo wanawake kwenye jamii yako wataelewa?

Answer

Hatuwezi kutabiri maswali uliyoandika kwenye Shajara yako ya Masomo wala maneno uliyotumia. Kwa hivyo, maswali yako yanaweza kuwa tofauti kidogo na yetu, na bado yawe bora. Kilicho muhimu ni kuwa lugha uliyotumia inafaa kueleweka kwa wanawake kwenye jamii yako. Unafaa kuuliza maswali kama;

 • Je, hedhi yako ya mwisho ilikuwa lini? Je, umekosa kwa mwezi mmoja?
 • Je, matiti yako yamekuwa makubwa hivi karibuni au yamekuwa laini?
 • Je, umeugua, hasa asubuhi unapoamka?
 • Je, umehisi uchovu usio wa kawaida au kuhisi usingizi wakati wa mchana?
 • Je, umehisi kutaka kukojoa zaidi ya kawaida?
 • Je, umehisi kitu kikisonga kwenye fumbatio lako?
 • Je, fumbatio lako limekuwa kubwa hivi karibuni?

Mwisho wa jibu

Muhtasari wa Kipindi cha 8