10.1 Je, kupima urefu wa uterasi ya mama hutueleza nini?

Lengo la kupima urefu wa uterasi ya mama ni kubaini iwapo mtoto anakua kikawaida katika kila kipindi cha ujauzito. Unapopima uterasi, unachunguza kujua ilipo sehemu ya juu ya uterasi.

Ishara bora

  • Urefu wa uterasi hulingana na umri wa ujauzito, yaani, idadi ya majuma au miezi ya ujauzito.
  • Sehemu ya juu ya uterasi huinuka kwenye fumbatio la mama kwa takriban upana wa vidole viwili au sentimita 4 kila mwezi.

Ishara za hatari

  • Urefu wa uterasi haulingani na idadi ya majuma au miezi ya ujauzito.
  • Sehemu ya juu ya uterasi inainuka zaidi ya au chini ya upana wa vidole viwili au sentimita 4 kila mwezi.
  • Je, unakumbuka jina la sehemu yenye umbo la kuba juu ya uterasi? (Ulisoma haya katika Kipindi cha 3.)

  • Huitwa fandasi.

    Mwisho wa jibu

Unapopima sehemu ya juu ya uterasi ilipofika kwenye fumbatio la mama, unapima urefu wa fandasi. Hii ni njia sahihi zaidi ya kukadiria ukuaji wa fetasi kuliko kupima uzani wa mama. Kupima urefu wa fandasi hukuonyesha mambo matatu:

  • Idadi ya miezi ambayo mwanamke huyo amekuwa mjamzito.
  • Tarehe anayotarajiwa kuzaa. Iwapo uliweza kujua tarehe anayotarajiwa kuzaa tangu hedhi yake ya mwisho, kupima urefu wa sehemu ya juu ya uterasi kunaweza kukusaidia kujua ikiwa tarehe anayotarajiwa kuzaa ni sahihi. Iwapo hukuweza kujua tarehe anayotarajiwa kuzaa kutoka kwa kipindi chake cha mwisho cha kawaida cha hedhi, kupima urefu wa fandasi kunaweza kukusaidia kujua tarehe anayotarajiwa kuzaa. Hii inafaa kufanywa katika uchunguzi wa kwanza wa utunzaji katika ujauzito.
  • Kiwango cha ukuaji wa mtoto. Katika kila uchunguzi katika ujauzito, pima urefu wa fandasi ili kujua ikiwa mtoto anakua kwa kiwango cha kawaida. Iwapo anakua haraka sana au polepole sana, huenda kuna tatizo.

Mtoto anapokua ndani ya uterasi, unaweza kuhisi uterasi ikikuwa kubwa kwa fumbatio la mama. Sehemu ya juu ya uterasi husonga takriban upana wa vidole viwili au sentimita 4 zaidi kila mwezi (Kisanduku 10.1).

Kisanduku 10.1 Mabadiliko kwa urefu wa fandasi katika ujauzito wa kawaida

Baada ya takriban miezi mitatu (majuma 13-14), sehemu ya juu ya uterasi huwa juu ya mfupa wa kinena wa mama (ambapo vuzi huanzia).

Baada ya takriban miezi mitano (majuma 20-22), sehemu ya juu ya uterasi huwa kwenye kitovu cha mama.

Baada ya takriban miezi tisa (majuma 36-40), sehemu ya juu ya uterasi karibu inafikia sehemu ya chini ya mbavu za mama.

Watoto wanaweza kuteremka chini katika majuma machache kabla ya kuzaliwa. Unaweza kutazama Picha 7.1 katika Kipindi cha 7 uone mchoro wa urefu wa fandasi katika majuma tofauti ya umri wa ujauzito.

Malengo ya Somo la Kipindi cha 10

10.2 Jinsi ya kupima urefu wa fandasi