10.3.3 Uterasi inakua polepole sana

Ukuaji wa pole pole wa uterasi unaweza kuwa dalili ya mojawapo ya matatizo haya:

  • Huenda mama ana kiasi kidogo cha maji (kiowevu cha amnioni) kwenye uterasi. Wakati mwingine ni kiasi kidogo cha maji kuliko kawaida na kila kitu bado kiko SAWA. Wakati mwingine, kiasi kidogo sana cha maji kinaweza kumaanisha kuwa mtoto si wa kawaida, au anaweza kuwa na matatizo katika leba.
  • Huenda mama huyo hupata lishe duni. Chunguza chakula ambacho mama amekuwa akila. Ikiwa hana uwezo kabisa wa kupata chakula kizuri cha kutosha, jaribu kupata njia ya kumsaidia yeye na mtoto wake. Kina mama na watoto wenye afya huimarisha jamii.
  • Huenda mama ana shinikizo la juu la damu (hipatensheni). Shinikizo la juu la damu linaweza kumfanya mtoto asipate lishe anayohitaji ili kukua vizuri. Ulijifunza jinsi ya kuchunguza shinikizo lake la damu katika kipindi kilichopita.
  • Huenda mama hunywa pombe, huvuta sigara au hutumia madawa. Haya yanaweza kufanya mtoto kuwa mdogo. Jaribu kutafuta mbinu za kumsaidia kuacha mienendo hii inayodhuru.
  • Huenda mtoto amefariki. Watoto waliofariki hawakui na kwa hivyo uterasi hukoma kukua.

Ikiwa huna kifaa kinachofaa kuchunguza shinikizo lake la damu, na uterasi inakua pole pole sana, mpe rufaa aende katika kituo cha afya kilicho karibu kwa uchunguzi.

Jinsi ya kujua ikiwa mtoto amefariki

Ukishuku kuwa huenda mtoto amefariki, mpe mama rufaa aende katika kituo cha afya kwa uzazimfu.

Ikiwa mama ana ujauzito wa miezi 5 au zaidi, mwulize ikiwa amemsikia mtoto akisonga hivi karibuni. Ikiwa mtoto hajasonga kwa siku mbili, huenda kuna tatizo. Ikiwa mama ana ujauzito wa zaidi ya miezi saba, au ikiwa ulisikia mpigo wa moyo wa mtoto katika safari ya awali, sikiza mpigo huo tena.

Mwanake akiripoti kutosonga kwa fetasi na huwezi kuusikia mpigo wa moyo, huenda mtoto amefariki. Iwapo hivyo, ni muhimu kwa mtoto aliyekufa (uzazimfu) kuondolewa haraka kwa sababu huenda mwanamke huyo akatokwa na damu kuliko kina mama wengine, na yuko katika hatari zaidi ya maambukizi.

Mama anapompoteza mtoto, anahitaji upendo, utunzaji na kueleweka (Mchoro 10.8). Hakikisha kuwa hapitii leba pekee yake. Akizaa mtoto mfu hospitalini, mtu anayemwamini anafaa kukaa naye wakati wa uzazi huo.

Mchoro 10.8 Mama anapompoteza mtoto wake, anahitaji upendo, utunzaji na kueleweka.

10.3.2 Uterasi inakua haraka sana

10.4 Hitimisho