13.1 Dhana na kanuni za utunzaji maalum katika ujauzito

Kihistoria, kielelezo cha kitamaduni cha utunzaji katika ujauzito kilianzishwa miaka ya kwanza ya 1900. Kielelezo hiki huchukulia kuwa ziara za kila mara na kuwaainisha wanawake wajawazito katika viwango vya hatari ya chini na hatari ya juu kwa kutabiri matatizo kabla ya wakati, ndiyo njia mwafaka ya kumtunza mama na fetasi. Utunzaji maalum katika ujauzito ulichukua nafasi ya mtazamo wa kitamaduni wa utunzaji katika ujauzito - huu ni mtazamo wa kimalengo uliopendekezwa na watafiti mnamo mwaka wa 2001 na kuanza kutumiwa na Shirika la Afya Duniani mnamo mwaka wa 2002.

Kusudi la utunzaji maalum katika ujauzito ni kukuza afya ya kina mama na watoto wao kupitia ukaguzi uliolengwa kwa wanawake wajawazito ili kusaidia:

  • Utambuzi na utabibu wa ugonjwa uliothibitishwa
  • Ugunduzi wa mapema kuhusu matatizo na shida zingine zinazoweza kuathiri matokeo ya mimba
  • Proflaksisi na matibabu ya anemia, malaria na magonjwa ya zinaa ikijumuisha VVU, maambukizi ya mfumo wa mkojo na pepopunda. Profilaksisi ni hatua za kuingilia kati zinazolenga kuzuia ugonjwa au matatizo.

Pia, utunzaji maalum katika ujauzito hukusudia kumpa kila mwanamke utunzaji wa kibinafsi ili kudumisha hali ya kawaida ya kuendelea kwa ujauzito kupitia uelekezi na ushauri wa wakati unaofaa kuhusu:

  • Maandalizi ya kuzaa (yalioelezwa baadaye katika kipindi hiki),
  • Lishe, chanjo, usafi wa mwili na upangaji uzazi (Kipindi cha 14)
  • Ushauri kuhusu dalili za hatari zinazoashiria kuwa mwanamke mjamzito anapaswa kupata usaidizi mara moja kutoka kwa mtaalamu wa afya (Kipindi cha 15).

Katika utunzaji maalum katika ujauzito, wahudumu wa afya husisitiza makadirio ya kibinafsi na hatua zinazohitajika ili mhudumu na mama mjamzito waweze kufanya uamuzi kuhusu utunzaji katika ujauzito. Hivyo basi, badala ya kufanya ziara za kila mara za kitamaduni za utunzaji katika ujauzito kuwa desturi kwa wote, na kuwaainisha wanawake kwa kuzingatia kiashiria hatari cha kidesturi, wahudumu wa utunzaji maalum katika ujauzito huongozwa na hali ya kibinafsi ya mwanamke.

Mtazamo huu pia hufanya utunzaji katika ujauzito kuwa jukumu la familia. Mhudumu wa afya hujadili na mwanamke na mumewe kuhusu matatizo ambayo mama anaweza kukumbana nayo; pamoja wanapanga kujitayarishia kuzaa na kujadili utunzaji wa baada ya kuzaa pamoja na maswala ya uzazi wa baadaye. Wanawake wajawazito hupata utunzaji wa asili wakiwa nyumbani na katika kituo cha afya; familia pamoja na wahudumu wa afya hutambua matatizo mapema; na hatua za kuingilia kati huanzishwa kwa wakati unaofaa hivyo kuwa na matokeo bora zaidi kwa akina mama na watoto wao.

Kisanduku 13.1 kinatoa muhtasari wa kanuni za kimsingi za utunzaji maalum katika ujauzito.

Kisanduku 13.1 Kanuni za kimsingi kuhusu utunzaji maalum katika ujauzito

  • Wahudumu wa utunzaji katika ujauzito hufanya utathmini mkamilifu wa mwanamke mjamzito ili kutambua na kutibu matatizo yaliyoko ya kiukunga na kitabibu.
  • Wao huendesha proflaksisi kama ilivyoashiriwa, kama vile hatua za kuzuia malaria, anemia, upungufu wa lishe, magonjwa ya zinaa ikijumuisha kuzuia kusambazwa kwa VVU kutoka kwa mama hadi kwa mtoto (tazama Kipindi cha 16), na pepopunda.
  • Wakiwajumuisha kina mama, wahudumu hawa huamua mahali pa kufanyia ziara fuatilizi za utunzaji katika ujauzito, jinsi ziara hizo zitakavyofuatana, mahali pa kuzalishia na atakayehusika katika utunzaji wa ujauzito na wa baada ya kuzaa.
  • Mradi tu kiwango cha utunzaji kimetiliwa mkazo katika kila ziara na wachumba wanafahamu hatari zinazoweza kutokea wakati wa ujauzito, mimba nyingi huendelea bila matatizo.
  • Hata hivyo hakuna ujauzito unaoweza kuwa 'bila hatari' hadi udhibitishwe, kwa sababu matatizo yanayohusiana na ujauzito, yakiwemo yenye athari mbaya na yasiyo na athari mbaya huwa hayatabiriki pamoja na matukio ya awamu za mwisho ya ujauzito.
  • Mwanawake mjamzito na mumewe huaminika kuwa 'wagunduzi wa hatari' baada ya kupata ushauri kuhusu dalili za hatari na pia 'washiriki' wa huduma ya afya kwa kukubali na kutekeleza mapendekezo yako.

Malengo ya Somo la Kipindi cha 13

13.1.1 Manufaa ya utunzaji maalum katika ujauzito