13.5.1 Ziara ya kwanza ya utunzaji maalum katika ujauzito

Ziara ya kwanza ya utunzaji maalum katika ujauzito inapaswa kutendeka kabla ya wiki 16 za ujauzito. Unapaswa kutimiza malengo yafuatayo:

 • Tambua historia ya mwanamke huyu ya kitabibu na kiukunga (ukitumia mbinu ulizojifunza katika Kipindi cha 8) ili upate ushahidi ikiwa anafaa kufuata kipengele cha kimsingi au utambue iwapo anahitaji utunzaji maalum na/au rufaa katika kituo cha juu zaidi cha afya.
 • Fanya uchunguzi wa kimsingi (mpigo wa moyo, shinikizo la damu, kiwango cha pumzi, joto, kuparara, na kadhalika).
 • Unapokisia kuwa ujauzito umepitisha trimesta ya kwanza, jaribu kutambua umri wa ujauzito kwa kupima urefu wa fandasi kwa kutumia mbinu ulizojifunza katika Kipindi cha 10.
 • Toa ushauri wa lishe na nyongeza ya kidesturi ya madini ya ayoni na foleti (vipimo vyake vimeelezwa katika Kipindi cha 14) Ni muhimu pia kutoa ushauri dhidi ya fikra potofu kuhusu chakula. Kwa mfano, katika baadhi ya sehemu za Afrika, watu huwaza kuwa kula mayai na nyama wakati wa ujauzito husababisha veniksi (unyeso mzito mweupe unaofunika ngozi ya mtoto anapozaliwa), na kwamba veniksi ni chafu. Kwa hakika, mayai na nyama ni asili muhimu za protini kwa mama na fetasi inayokua, na veniksi ni muhimu kwa mtoto kwani huikinga ngozi yake.
 • Toa ushauri kuhusu VVU na huduma za kuzuia kusambazwa kwa VVU kutoka kwa mama hadi kwa mtoto (utajifunza jinsi ya kufanya hivi katika Kipindi cha 16).
 • Toa ushauri wa jinsi ya kuzuia malaria na inapohitajika uwape neti zilizotiwa dawa ya kuua wadudu. Utajifunza mengi kuhusu kuzuia na kutibu malaria katika Kipindi cha 18.
 • Pima kiwango cha sukari kwenye mkojo wake kwa kutumia kijiti cha kupimia kama ulivyojifunza katika Kipindi cha 9, au umpe rufaa hadi kwenye kituo cha afya ukikisia kuwa anaanza kuwa na kisukari.
 • Mshauri yeye na mwenziye kuweka hakiba ya fedha ikiwa utahitaji kumpa rufaa, hasa iwapo jambo la dharura litakalohitaji asafirishwe hadi kwenye kituo cha afya litatokea. Mwanamke huyu anaweza pia kuhitaji fedha zaidi za dawa na matibabu. Usaidizi wa kifedha unaweza kupatikana katika mashirika ya jamii kama vile vikundi vya kina mama.
 • Toa majibu mahususi kwa maswali au mashaka ya mwanamke mjamzito au yale ya mwenziye.
 • Inamaanisha nini ikiwa kuna tofauti ya wiki kadhaa baina ya umri wa ujauzito uliokadiriwa kwa kutumia kipimo cha urefu wa fandasi na kadirio la kipindi cha mwisho cha hedhi ya kawaida?

 • Kama ulivyojifunza katika Kipindi cha 10, hii inaweza kumaanisha kuwa mwanamke hajakumbuka vyema tarehe ya kipindi cha mwisho cha hedhi ya kawaida, lakini inaweza pia kumaanisha kuwa fetasi haikui kwa njia ya kawaida (urefu wa fandasi ukiwa chini ya kadirio la kipindi cha mwisho cha hedhi ya kawaida) au pia inawezekana kuna kiowevu cha amniotiki kingi zaidi kinachoizingira fetasi, au kuna ujauzito wa pacha au mtoto mkubwa zaidi (urefu wa fandasi ni zaidi ya kadirio la kipindi cha mwisho cha hedhi ya kawaida.)

  Mwisho wa jibu

13.5 Malengo na taratibu katika kila ziara ya utunzaji maalum katika ujauzito

13.5.2 Ziara ya pili ya utunzaji maalum katika ujauzito