19.1.2 Athari za hipatensheni ya mama kwa fetasi

Aina yoyote ya hipatensheni katika ujauzito ina athari kubwa kwa ukuaji na kuishi kwa fetasi. Hii hutendeka kutokana na kupungua kwa kiasi cha damu ya mama, jambo ambalo baadaye hupunguza uletaji wa damu kutoka kwa ateri za endometria hadi kwa plasenta. Ateri za endometria huleta damu ya mama kwa plasenta, na kuleta oksijeni kutoka kwa mapafu na virutubishi kutoka kwa mfumo wake wa umeng'enyaji hadi kwa fetasi. (Unaweza kuyaona ukitazama nyuma katika Mchoro 5.5 katika Kipindi cha 5.)

  • Je, ukuaji wa fetasi utaathiriwa vipi iwapo kiasi cha damu ya mama inayoingia kwenye plasenta kitapungua?

  • Upelekaji wa oksijeni, virutubishi, na viowevu kwenda kwa mtoto utapungua na kwa hivyo hatakua kikawaida. Ukuaji wa fetasi unaweza kuzuiliwa (hipatensheni katika ujauzito ni mojawapo ya visababishi vikuu vya uzuiaji wa ukuaji kwenye uterasi).

    Mwisho wa jibu.

Kiwango cha kiowevu cha amnioni kinachozunguka fetasi pia kitakuwa kidogo kuliko kawaida kwa sababu damu inayofika kwenye figo za mtoto imepungua na kwa hivyo hutengeneza kiasi kidogo cha mkojo. Mwishoni mwa ujauzito, kiasi kingi cha kiowevu cha amnioni hutoka kwa mkojo wa mtoto. Fetasi inaweza kufariki kutokana na ukosefu wa oksijeni na virutubishi, au kutokana na kupungua kwa kiowevu cha amnioni. Iwapo fetasi itaishi muda mrefu kwenye uterasi huku ikipata oksijeni kidogo, ubongo unaokua unaweza kuathiriwa vibaya sana. Kutokana na hayo, mtoto huyu anaweza kuwa punguani baadaye iwapo atazaliwa akiwa hai na kuongoka katika maisha ya mapema utotoni.

Pia fetasi inaweza kufariki kwa sababu plasenta huzeeka mapema sana na kusababisha usambazaji duni wa damu kwa fetasi, kwa hivyo plasenta inaweza kujitenga mapema na kuta za uterasi. (Mtengo wa mapema huitwa kuachia kwa plasenta na utajifunza kuuhusu katika Kipindi cha 21.) Leba ya mapema inaweza kuanza yenyewe (Kipindi cha 17) na maisha ya mama pia yanaweza kuwa hatarini kutokana na kuachia kwa plasenta ambapo damu nyingi inaweza kupotezwa.

19.1.1 Athari kwa mishipa ya damu na viowevu vya mwili

19.1.3 Matatizo yanayotokea sana ya priklampsia kali kwa mama