19.5.1 Matukutiko katika eklampsia

Tukutiko katika eklampsia ni sawa na tukutiko kwa watu walio na kifafa. Kama tukutiko la kifafa, lina awamu nne:

Awamu ya utulivu

Sifa bainifu ya awamu ya kwanza ni kipindi cha utulivu (huenda kisichukue zaidi ya sekude 20) mtu anapokuwa na udhaifu wa misuli kwenye mwili wote, mkazo na mshtuko wa misuli, na macho yanayokodoa.

Awamu ya toni

Hii inaweza kudumu hadi sekunde 30 na huonyeshwa kwa aina kali ya mikazo ya misuli kwenye mwili wote ambapo misuli ya miguu na mikono hunywea sana na hata kuonekana thabiti kama kijiti kikavu. Katika awamu ya toni, mwanamke hukoma kupumua na kukosa oksijeni. Pia kuna kugeuzageuza macho na unaweza kuona sehemu ya juu ya sklera (sehemu nyeupe ya jicho).

Awamu ya kiklonasi

Awamu ya tatu inaweza kuchukua hadi dakika 2 na hasa ni mwendo wa mshtuko wa mwili wote kutokana na kunywea na kulegea kwa misuli. Katika awamu hii mwanamke anaweza kupumua na pia kutoa mate na mkojo.

Kipindi cha koma

Baada ya awamu ya kiklonasi, katika kisa dhahiri, mwanamke hupoteza fahamu kabisa kwa muda usiojulikana. Hata hivyo, mwanamke huyo anaweza kwenda katika koma mwanzoni kabisa (yaani, bila tukutiko hata moja). Muda wa hali ya koma hutegemea:

  • Idadi ya matukutiko ya hapo awali: Idadi ya matukutiko inavyokuwa kubwa ndivyo muda wa koma unavyokuwa mrefu, ambao hata unaweza kusababisha kifo. Kuwa na historia ya zaidi ya matukutiko kumi ni mojawapo ya ishara ya matokeo mabaya. Kwa hivyo, tukutiko linapodhibitiwa mapema ndivyo matokeo yatakavyokuwa bora kwa mama na mtoto.
  • Ukali wa edema ya ubongo: Nafasi kati ya fuvu la kichwa na ubongo ni ndogo sana. Kwa hivyo, hata ongezeko dogo kwa ukubwa wa ubongo wa mama kutokana na edema au kutokwa na damu litakuwa na athari kwa seli za ubongo kwa sababu shinikizo kwenye ubongo (shinikizo ndani ya kichwa) huongezeka sana.
  • Kiasi cha kutokwa na damu ndani ya kichwa (tazama hapa chini katika kipindi hiki): Jinsi ilivyoelezwa kuhusu edema ya ubongo, kutokwa na damu kwenye nafasi ndani ya kichwa kutaongeza shinikizo la ndani ya kichwa kwenye seli za ubongo. Pia, inaweza kusababisha kutoka zaidi kwa damu na kuweza kuleta mzunguko wa hali hii tena na tena.
  • Hipoglisimiahusika (kiwango cha chini cha sukari kwa damu): Kila tukutiko huhitaji nguvu. Hii ni kwa sababu karibu misuli yote ya skeletoni hunywea na kulegea mara mingi katika awamu za toni na kiklonasi. Matukutiko ya mara kwa mara humaanisha kutumika kwa nguvu nyingi, inayotoka kwenye sukari katika damu, ini na tishu. Mwanamke aliye na eklampsia hawezi kurudisha sukari iliyotumiwa na misuli haraka ifaavyo na kwa hivyo hukumbwa na kiwango cha chini cha sukari kwenye damu (hipoglisimia kali) ambayo baadaye hujionyesha kwa koma. Kwa kuwa kiwango chake cha sukari kwenye damu kiko chini, mwanamke aliye na eklampsia atapata nguvu kutoka kwa protini kwenye misuli yake kila wakati ili kumweka uhai. Usagaji wa protini hutoa ketoni ambazo zinaweza kutumika kama chanzo cha nguvu na zingine zitaonekana kwenye mkojo wake. Unaweza kupima kuwepo kwa ketoni kwa dipstick.

19.5 Dalili za kiafya za eklampsia

19.6 Je, unaweza kufanya nini ukitambua ugonjwa wa kihipatensheni kwa mwanamke mjamzito?