21.2 Kutengeka kwa plasenta:

Kutengeka kwa plasenta: humaanisha kutengeka kwa kipande cha plasenta au plasenta yote iliyojibandika kwenye sehemu ya thuluthi mbili za juu ya uterasi kabla ya wakati. Kwa kawaida, plasenta hutengana na uterasi baada ya kutolewa kwa fetasi, katika awamu ya tatu ya leba (Utajifunza kuhusu haya yote katika Moduli ya Utunzaji wa Leba na Kuzaa). Mama na mtoto wanaweza kufa ikiwa sehemu ambapo plasenta ilitengana na pembezoni mwa uterasi itaanza kuvuja damu.

  • Ni kwa nini kuna uwezekano wa kuvuja damu sana ikiwa plasenta itatengana na pembezoni mwa uterasi kabla ya wakati? Ni kwa nini tukio hili huhatarisha maisha ya mama na fetasi? (Rejelea uliyoyasoma kuhusu muundo wa plasenta katika Kipindi cha 5 au uutazame tena Mchoro 5.5 katika Utunzaji kabla ya Kuzaa, Sehemu ya 1.)

  • Damu ya mama hutiririka hadi kwenye nafasi kubwa katika plasenta; sehemu zinazopakana na mishipa ya damu ya fetasi (Mchoro 5.5). Ikiwa plasenta itatengeka kutoka pembezoni mwa uterasi, damu ya mama itatiririkia kwenye uwazi wa uterasi, hivyo anaweza kufa kufuatia kupoteza damu nyingi. Kiwango cha virutubishi na oksijeni kinachoifikia fetasi kutoka katika damu ya mama kitapunguka, hivyo fetasi inaweza kufa au ubongo wake kuharibika.

    Mwisho wa jibu

Damu nyingi inayovuja kwenye sehemu ambapo plasenta imetengana na pembezoni mwa uterasi inaweza kupitia seviksi kisha kutiririkia ukeni. Damu hii kwa kawaida huwa na uweusi kwa kukosa oksijeni ya kutosha. Hii ni dalili kuu ya hatari.

Mchoro 21.1 Kuvuja damu kufuatia kutengeka kwa plasenta pembezoni mwa uterasi.

Hata hivyo, katika baadhi ya matukio, damu yote kutoka katika sehemu ambapo plasenta imejitenga inaweza kusalia ndani ya uterasi, kisha kuanza kujaa (Mchoro 21.1) Damu haitaonekana ikitokea ukeni kwa sababu kiasi kidogo sana cha damu hupenyeza na kutokea ukeni. Hata hivyo, mwanamke ataonyesha ishara za kuvuja damu ndani ya uterasi, ziitwazo mshtuko unaohusiana na kuvuja damu. Tulijadili hali hii kwa muhtasari katika Kipindi cha 20 kuhusu kuvuja damu katika nyakati za mwanzo za ujauzito. Tutarudia habari inayofuata hapa (Kitengo 21.2.1) kwa sababu kuna hatari zaidi ya mshtuko huu kutokea ikiwa mwanamke atavuja damu katika awamu za mwisho za ujauzito.

Dalili zingine za kutengeka kwa plasenta ni pamoja na:

  • Ikiwa mama tayari yuko katika leba, tambua kama ana uchungu kati ya mikazo, ambao unazidi kuwa mbaya wakati upitapo.
  • Fumbatio lake ni gumu, lina kidonda na ni chungu likiguswa.
  • Mpigo wa moyo wa mtoto unaweza kuwa wa kasi mno (zaidi ya midundo 180 kwa dakika), au wa chini sana (chini ya midundo 100 kwa dakika), au ikiwa mpigo wa moyo wa fetasi hausikiki, mtoto anaweza kuwa amekufa.
  • Mtoto hasikiki akicheza au anacheza mara chache.

21.1 Kuvuja damu katika awamu za mwisho wa ujauzito husababishwa na nini?

21.2.1 Mshtuko unaohusiana na kuvuja damu