21.3 Privia ya plasenta

Kisababishi kingine cha kuvuja damu katika awamu za mwisho za ujauzito ni privia ya plasenta. Katika hali hii, plasenta huwa imejibandika karibu sana na seviksi, au hata kuifunika (Mchoro 21.2). Seviksi inapoendelea kupanuka, ncha ya plasenta inaweza kutengeka na kuanza kuvuja damu. Mwanamke mwenye hali hii kwa kawaida huwa na damu yenye rangi ng'avu nyekundu inayovujia ukeni. Kiwango cha damu inayovuja kinaweza kuwa cha chini ikilinganishwa na ile inayovuja kufuatia kutengeka kwa plasenta, lakini katika baadhi ya matukio, hali hii inaweza kuwa kali na hatari kwa maisha. Kuvuja damu mara nyingi huwa hakuandamani na uchungu, hivyo mwanamke anaweza kutotambua kwa muda mrefu, kwa mfano, usiku akilala. Kuvuja damu kunaweza kuanzishwa na ngono na kunaweza kurejea kila mara (kukikoma kisha kuanza tena).

Mchoro 21.2 Privia ya plasenta imeainishwa kulingana na jinsi ncha ya plasenta imekaribia seviksi. (a) Privia ya chini ya plasenta, lakini haikuziba seviksi.(b) Privia ya plasenta ya kadri. (c) Privia ya plasenta kamilifu.

Katika mwanamke aliyevuja damu katika awamu za mwisho za ujauzito kufuatia privia ya plasenta, uterasi mara nyingi huwa laini kwa kumpapasa fumbatio. Hali hii ni kinyume na uterasi iliyo gumu wakati kuvuja damu kumesababishwa na kutengeka kwa plasenta.

Kwa kijumla, kichwa cha fetasi hakiko katika sehemu ya chini ya uterasi, ambayo utahisi ikiwa tupu. Hali hii ya mtoto kutanguliza vibaya inaweza kuwa dalili ya privia ya plasenta. Kwa kawaida, hali ya fetasi ni ya kawaida, hivyo unaweza kuhisi mpigo wa moyo wa fetasi ukisikiliza kwa fitoskopu. Mama pia huhisi fetasi ikicheza kama kawaida — lakini hali hii huwa tofauti wakati mwingine.

Utambuzi wa privia ya plasenta unaweza tu kuthibitishwa kwa kumchunguza mama kwa mtambo wa pichatiba unaoweza kuonyesha hali ya plasenta, au kwa kuchunguza uke katika chumba cha upasuaji. Kwa hivyo, unapaswa kumpendekezea rufaa hadi kituo cha afya kilicho na vifaa vinavyohitajika kufanyia utambuzi.

Wanawake wanaoshukiwa kuwa na privia ya plasenta wanapaswa kuhamishwa hadi katika Hospitali ya Wilaya au Kituo cha Afya chenye mtambo wa pichatiba au chumba cha upasuaji.

Usimchunguze uke wewe mwenyewe iwapo mwanamke anavuja damu katika awamu za mwisho za ujauzito. Hatua hii huzidisha hali hii na kuongeza hatari kwake na fetasi.

21.2.3 Kushindwa kwa moyo

21.4 Uterasi iliyopasuka